UNA HELA WEWE? CHEKI WATU WANAVYOPIGA MISHAHARA HUKO ULAYA

LONDON, ENGLAND. VIJANA wa mjini wanakwambia tafuta pesa upunguze kujieleza. Wahenga walisema, pesa ni sabuni ya roho.
Supastaa, Lionel Messi baada ya kuwapunguzia mshahara wake Barcelona na bado wakashindwa kumpa dili jipya, aliamua kutimkia zake Paris Saint-Germain, mahali ambako analipwa mshahara wa kufuru.
Kwenye kikosi hicho cha miamba ya soka ya Ufaransa amesaini mkataba wa miaka miwili, huku kwa mwaka akidaiwa kupokea zaidi ya Pauni 54 milioni. Si mchezo.
Je, mshahara anaolipwa Messi huko PSG kuna mchezaji mwingine wa soka duniani anayemzidi?
Wakati ukiwa unajiuliza swali hilo, hii hapa orodha ya mastaa 10 wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi duniani kwa mwaka huu wa 2021. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti za L’Equipe, Forbes na vyanzo vingine. Namba hizo zinahusu mshahara tu, kabla haujakatwa kodi na hazihusishi bonasi, ada nyingine pamoja na dili za kibiashara. Ni mshahara peke yake wanaolipwa kila wiki.
Dili lake la kwenda kutafuta pesa PSG limemfanya Messi kuendelea kushika namba moja ya mastaa wa soka wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.
Anashika namba moja juu ya mpinzani wake wa miaka yote, Cristiano Ronaldo, ambaye huko Juventus analipwa Pauni 60,000 kwa wiki pungufu ya kiwango anacholipwa Messi.
Supastaa wa Kibrazili, Neymar anashika namba tatu na baada ya hapo, wanafuatia wakali wawili wa La Liga, Luis Suarez na Antoine Griezmann.
Gareth Bale haonekani kuwa na maajabu Real Madrid, lakini anashika namba sita huku Kylian Mbappe, ambaye ni namba tatu kwa mshahara kwenye kikosi cha PSG, jina lake lipo kwenye orodha hii ya wakali 10 wenye mishahara mikubwa duniani.
Kevin De Bruyne ndiye anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England, akimzidi kipa wa Manchester United, David De Gea huku Robert Lewandowski wa Bayern Munich akikamilisha orodha hiyo.
Kwa kifupi orodha hiyo ya wachezaji wenye mishahara mikubwa duniani, watatu wanatoka kwenye Ligue 1, watatu kwenye La Liga, wawili kwenye Ligi Kuu England na mmoja kutoka Serie A na Bundesliga.
10.Robert Lewandowski
Timu: Bayern Munich
Mshahara: Pauni 350,000 kwa wiki
Chelsea ilihusishwa na mpango wa kunasa saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiagazi, lakini Bayern Munich iliweka msisitizo haiwezi kumruhusu straika wao namba moja, Robert Lewandowski aondoke.
Hakuna ubishi, kama kuna mafowadi matata kabisa kwenye soka la Ulaya kwa sasa basi Lewandowski ni mmoja wao huku Bayern wakilipia huduma yake mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki.
9.David De Gea
Timu: Man United
Mshahara: Pauni 375,000 kwa wiki
Makosa yake mengi ya siku za karibuni anapokuwa kwenye goli yameibua mjadala kuhusu mshahara wake anaolipwa huko Manchester United. Hii inamhusu kipa David De Gea.
Mhispaniola huyo ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa duniani, huku akishika namba moja kwenye kikosi cha Man United huko Old Trafford. De Gea kwa nguvu ile ya kuokoa mashuti analipwa mshahara wa Pauni 375,000 kwa wiki.
8.Kevin De Bruyne
Timu: Man City
Mshahara: Pauni 385,000 kwa wiki
Manchester City ilifanikiwa kumtuliza supastaa wao Kevin de Bruyne kwa kumpa mkataba mrefu na wenye malipo makubwa ya mshahara. Kwa sasa, KDB ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa kwenye Ligi Kuu England na hilo litabadilika kama Harry Kane atakwenda kutua kwenye kikosi hicho cha Man City. Kwa huduma matata kabisa ya KDB inawafanya Man City kumlipa mshahara wa Pauni 385,000 kwa wiki.
7.Kylian Mbappe
Timu: PSG
Mshahara: Pauni 410,000 kwa wiki
Kinachosemwa kuhusu mshambuliaji Kylian Mbappe kwa sasa ni mpango wake wa kwenda Real Madrid. Fowadi huyo Mfaransa anadaiwa anataka kukutana na rais wa Paris Saint-Germain ili iwasikilize mabosi wa Real Madrid juu ya dili la kwenda kujiunga na timu hiyo. Mkataba wa Mbappe utafika tamati mwakani, huku fowadi huyo akiwa mmoja wa wanaolipwa pochi nene kwenye mshahara, Pauni 410,000 kwa wiki.
6.Gareth Bale
Timu: Real Madrid
Mshahara: Pauni 500,000 kwa wiki
Msimu uliopita, Los Blancos iliamua kumrudisha Gareth Bale kwenye klabu yake ya Tottenham Hotspur kwenda kucheza kwa mkopo. Lakini, sasa amerudi Bernabeu kwenda kumalizia mwaka wa mwisho wa mkataba wake, huku miamba hiyo iliyomsajili kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia mwaka 2013, Pauni 85 milioni ilisaini dili la mshahara mrefu, ikimlipa Pauni 500,000 kwa wiki bila kujali anacheza au hachezi.
5.Luis Suarez
Timu: Atletico Madrid
Mshahara: Pauni 575,000 kwa wiki
Alipopigwa chini Barcelona na kuamua kutimkia zake Atletico Madrid jambo hilo lilimsikitisha sana Lionel Messi huko Nou Camp.
Hakika Luis Suarez amewalipa Barcelona kwa kwenda kuwapa Atletico Madrid ubingwa wa La Liga katika msimu wake wa kwanza tu. Atletico ilitambua huduma ya mchezaji waliyemnasa kutoka Barcelona na hivyo waliamua kumpa mshahara wa Pauni 575,000 kwa wiki.
4.Antoine Griezmann
Timu: Barcelona
Mshahara: Pauni 575,000 kwa wiki
Baada ya kuondoka Lionel Messi kwenye kikosi cha Barcelona, Antoine Griezmann sasa anabeba majukumu ya kuipaisha timu hiyo ili kuhakikisha mashabiki wake wamsahau supastaa wao wa zamani.
Baada ya Antoine Griezmann kutua Barcelona akitokea kwa mahasimu wao wa La Liga, Atletico Madrid walimshawishi kwa mshahara mkubwa, wakimlipa Pauni 575,000 kwa wiki kutokana na huduma yake anayotoa uwanjani.
3.Neymar
Timu: PSG
Mshahara: Pauni 606,000 kwa wiki
Mbrazili, Neymar alivunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho wakati aliponaswa na Paris Saint-Germain kwa ada ya Pauni 298 milioni. Kama ilivyo kwa ukubwa wa ada iliyolipwa kupata saini yake, hata mshahara wake Neymar pia ipo vizuri kwelikweli, ambapo mkali huyo analipwa Pauni 606,000 kwa wiki na kumfanya awe mchezaji namba tatu kwa wanaokunja mkwanja mrefu kwenye malipo ya mishahara duniani.
2.Cristiano Ronaldo
Timu: Juventus
Mshahara: Pauni 900,000 kwa wiki
Kinachosemwa kuhusu supastaa wa Kireno, Cristiano Ronaldo kwa sasa ni kuhusu hatima yake kwenye kikosi cha Juventus, akihusishwa na kuachana na miamba hiyo ya Turin.
Wakati dirisha la uhamisho likiwa bado halijafungwa, haijulikani ni wapi Ronaldo atakwenda - lakini kwa wakati huu akiwa Juventus, amekuwa akilipwa mshahara mkubwa kwelikweli, Pauni 900,000 kwa wiki hapo hujaweka bonasi wale malipo mengine.
1.Lionel Messi
Timu: PSG
Mshahara: Pauni 960,000 kwa wiki
Supastaa, Lionel Messi haingii dili za ovyo ovyo. Kiwango chake matata cha ndani uwanjani kimekuwa kikimweka kwenye daraja la juu kabisa na timu zote zinazohitaji saini yake ni lazima zifungue pochi.
Messi alikuwa akivuna mshahara mrefu tangu alipokuwa Nou Camp na sasa analipwa Pauni 960,000 kwa wiki - huo ni mshahara tu bila ya bonasi nyingine huko kwa wababe wa Ligue 1, Paris Saint-Germain.