Van Dijk ategwa kwa mkwanja tu

Muktasari:

  • Liverpool inajiandaa kuwa na maisha mapya chini ya kocha Arne Slot msimu ujao na Mdachi huyo anatua Anfield na kukutana na hali ya sintofahamu ya mustakabali wa maisha ya Van Dijk kutokana na beki huyo kuingia kwenye mwaka wake wa mwisho wa mkataba huko Liverpool.

LIVERPOOL,ENGLAND: BEKI wa kati na nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk amepewa ofa ya mkataba wa kibabe kabisa utakaomfanya awe beki anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani huko Al-Nassr, endapo kama atakubali kujiunga na miamba hiyo ya Saudi Arabia, imeelezwa.

Liverpool inajiandaa kuwa na maisha mapya chini ya kocha Arne Slot msimu ujao na Mdachi huyo anatua Anfield na kukutana na hali ya sintofahamu ya mustakabali wa maisha ya Van Dijk kutokana na beki huyo kuingia kwenye mwaka wake wa mwisho wa mkataba huko Liverpool.

Hata mwaka haujapita tangu Liverpool ilipogomea ofa ya pesa nyingi ya kumhusu Mohamed Salah kutoka Saudi Arabia na sasa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, kuna kasheshe jingine linawahusu juu ya hatima ya beki wao, Van Dijk anayewindwa Saudi Pro League.

Wawakilishi wa beki huyo Mdachi wameripotiwa kukutana na meneja mkuu wa klabu ya Al-Nassr.

Na hilo lilifichuliwa na gazeti la Marca la Hispania, ambapo kikao cha kwanza kilifanyika usiku wa Jumanne iliyopita. Kinachoelezwa ni kwamba Al-Nassr imeweka mezani ofa ya mshahara mnono kwa ajili ya Van Dijk, ambapo atakwenda kuwa beki anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani.

Al-Nassr inatafuta mastaa kwa ajili ya kuondoa pengo la ubora baina yao na mahasimu wao Al-Hilal. Tayari kwenye kikosi chao kuna mastaa kama Cristiano Ronaldo, Sadio Mane na Aymeric Laporte, hivyo wanamtaka Van Dijk na kipa Wojciech Szczesny kumaliza kazi kabisa.

Licha ya kutumia pesa nyingi kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, Al-Nassr iliyosheheni mastaa wa kutosha ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Saudi Pro League. Lakini, kitu kibaya zaidi kwao ni kumaliza pointi 14 nyuma ya vinara Al-Hilal, ambao walinyakua ubingwa wa ligi, huku wakiwa wamecheza msimu wote bila ya kupoteza. Mabadiliko yanatarajia kutokea Anfield kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.