Vinicius awakacha Waarabu

Muktasari:
- Imeripotiwa kuwa Waarabu walikuwa tayari kulipa ada ya uhamisho na kumpa Mbrazil huyu mshahara unaofiki Pauni 400 milioni kwa mwaka lakini bado Vini anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani akiwa Santiago Bernabeu.
MADRID, HISPANIA: LICHA ya kuwekewa ofa nono na matajiri wa Saudi Arabia, Vinicius Junior amekataa ofa hiyo na kukubali kusaini mkataba mpya na Real Madrid ambao utatangazwa mwishoni mwa msimu.
Imeripotiwa kuwa Waarabu walikuwa tayari kulipa ada ya uhamisho na kumpa Mbrazil huyu mshahara unaofiki Pauni 400 milioni kwa mwaka lakini bado Vini anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani akiwa Santiago Bernabeu.
Vini, 24, amekubali kusaini mkataba mpya na mabingwa hao wa Hispania ambao utakuwa wa miaka miwili au mitatu.
Mkataba wa sasa wa mchezaji huyu wa zamani wa Flamengo unaisha 2027 na Madrid ilikuwa tayari kumuuza kama angekataa ofa yao ya mkataba mpya.
Moja ya sababu ambazo zinadaiwa kumshawishi sana Vinicius akubali kuendelea kusalia ni ndoto yake ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or ambayo aliikosa mwaka jana.
Hata hivyo, kwa msimu huu mambo yanaonekana kuwa magumu kwake kufanikisha suala hilo kwani Madrid imeshatolewa katika Ligi ya Mabingwa na wana hatihati ya kuchukua taji la La Liga pia.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Vinicius amefunga mabao 20 na kutoa asisti 14 kwenye michuano yote.