Waarabu waweka dau nono kwa Moises Caicedo

Muktasari:
- Ripoti kutoka tovuti ya Telegraph, zinaeleza kwamba Chelsea inaweza kuwa tayari kumuuza fundi huyu lakini kwa kiasi cha pesa ambacho kitakuwa zaidi ya Pauni 100 milioni.
AL-Nassr ya Saudi Arabia inahitaji saini ya kiungo wa Chelsea na timu ya taifa ya Ecuador, Moises Caicedo, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Ripoti kutoka tovuti ya Telegraph, zinaeleza kwamba Chelsea inaweza kuwa tayari kumuuza fundi huyu lakini kwa kiasi cha pesa ambacho kitakuwa zaidi ya Pauni 100 milioni.
Mkataba wa sasa wa Caicedo unatarajiwa kumalizika mwaka 2031, msimu huu amecheza mechi 37 za michuano yote na kufunga bao moja.
Mbali ya pesa nono ya uhamisho ambayo Al Nassr inataka kuitoa, pia ipo tayari kumpa Caicedo mshahara wa zaidi ya Pauni 800,000 kwa wiki.
Caicedo ni mmoja kati ya wachezaji ghali waliopo kwenye kikosi cha Chelsea kutokana na ada ya uhamisho iliyolipwa na timu hiyo ya Pauni 115 milioni kumnunua akitokea Brighton.
Xavi Simons
KIUNGO mshambuliaji wa RB Leipzig, Xavi Simons anadaiwa kuwaambia Manchester United kwamba atakuwa tayari kujiunga nao katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kama watafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao.
Simons mwenye umri wa miaka 21, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amecheza mechi 29 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Sandro Tonali
JUVENTUS imemuweka kiungo wa kati wa Newcastle na timu ya taifa ya Italia, Sandro Tonali, 24, kama kipaumbele chao kwenye usajili wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Tonali anadaiwa kushawishika sana na mpango wa kutua Juventus na hiyo imesababisha awaambie Newcastle kuwa anahitaji kuondoka. Mkataba wa Tonali unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Benjamin Sesko
RB Leipzig wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 86 milioni kwa timu itakayotaka kumsajili mshambuliaji wao na timu ya taifa ya Slovenia, Benjamin Sesko mwenye umri wa miaka 21, ambaye anawindwa na timu mbalimbali barani Ulaya ikiwa pamoja na Manchester United, Chelsea na Arsenal. Sesko ni mmoja ya mastraika waliionyesha kiwango bora katika Bundesliga kwa msimu huu.
Destiny Udogie
TOTTENHAM haitaki kusikiliza ofa kutoka timu yoyote inayohitaji saini ya beki wao wa kushoto na timu ya taifa ya Italia, Destiny Udogie, 22, ambaye tangu kuanza kwa mwaka huu vigogo mbalimbali wanahitaji huduma yake ikiwamo Manchester City.
Msimu huu Udogie amecheza mechi 30 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Goncalo Inacio
SPORTING Lisbon ipo tayari kupokea ofa kwa ajili ya kumuuza beki wao raia wa Ureno, Goncalo Inacio, 23, katika dirisha lijalo.
Inacio mara kadhaa amehusishwa na Chelsea na Manchester United.
Inaelezwa kocha wa Man United, Ruben Amorim ndio amependekeza jina lake akihitaji asajliwe mwaka ili kuboresha eneo lake la ulinzi.
Joao Felix
BENFICA wanataka kutuma ofa kwenda Chelsea ili kuipata saini ya mshambuliaji wao na timu ya taifa ya Ureno, Joao Felix, 25, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo AC Milan.
Kabla ya kwenda katika ligi tano bora barani Ulaya, Felix alikuwa akiichezea Benfica ya Ureno.
Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2031.
Kevin de Bruyne
CHICAGO Fire inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani imewasilisha ombi la kumsajili kiungo wa kati wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin de Bruyne, 33, ambaye ataondoka timu hiyo mwisho wa msimu huu ambapo mkataba wake utakuwa unamalizika. KDB ametajwa sana kuwa atatua Marekani lakini yeye anataka kubaki Ulaya.