Abdul Usangi afichua alivyomnasa manara Kombolela
Muktasari:
- Kwa nini wameshtuka? Hakuna aliyetarajia Manara kuingia katika uigizaji akicheza kama ‘Mr. Chande’ na baadhi wakisema ‘ghafla sana’ na huko amefanya mambo makubwa na kuvutia mashabiki wanaoendelea kuifuatilia tamthilia hiyo.
ALIYEKUWA msemaji wa Klabu ya Yanga na sasa mtangazaji wa redio, Haji Manara wiki chache zilizopita alishtua mashabiki wa filamu Bongo baada ya kuibuka katika Tamthilia ya Kombolela inayorushwa na kituo cha Azam Medi katika chaneli ya Sinema Zetu.
Kwa nini wameshtuka? Hakuna aliyetarajia Manara kuingia katika uigizaji akicheza kama ‘Mr. Chande’ na baadhi wakisema ‘ghafla sana’ na huko amefanya mambo makubwa na kuvutia mashabiki wanaoendelea kuifuatilia tamthilia hiyo.
Hata hivyo, wengi hawajui nyuma ya ujio wa Manara kuna nani.
Si mwingine ni mtunzi na mwandishi wa tamthilia hiyo, Abdull Usangi.
Sasa ili kufahamu kuhusu ujio wa Manara katika Kombolela, safu hii ya Dakika 5 Na... ilimsaka na kupata ukweli wa mambo.
Abdull anaelezea safari ngumu ya kumshawishi na hofu alizokuwa nazo Manara, na kwa nini aliona yeye ndiye mtu sahihi zaidi kwa nafasi hiyo.
MWANASPOTI: Hongera sana kwa kazi kubwa unayoifanya. Tunaona mawimbi ya Kombolela yanazidi kuwa makubwa. Leo tunataka utupe undani kidogo; uliwezaje kumpata Haji Manara na nini kilikufanya uone yeye ndiye anafaa?
ABDUL USANGI: Asante sana. Haji Manara ameingia hivi karibuni kama mshiriki mpya akicheza uhusika wa Mr. Chande, ambaye ni fundi chereani. Hili lilikuwa wazo ambalo nililifikiri kwa muda mrefu sana. Nilihitaji mtu mwenye ‘ujazo mkubwa’ (big figure), lakini zaidi nilitafuta mtu ambaye ana asili ya upwani kwa asilimia kubwa kutokana na asili ya uhusika wenyewe.
Ukiangalia asili ya Haji na uzoefu wake, ni mtu mwenye ushawishi mkubwa na ana hiyo asili ya upwani ambayo niliihitaji.
MWANASPOTI: Ilikuwa rahisi kumshawishi aingie kwenye uigizaji?
ABDUL USANGI: Haikuwa rahisi hata kidogo, ilikuwa kazi ngumu. Nakumbuka mara ya kwanza nilimfuata maeneo ya mjini wakati Mwezi wa Ramadhani unakaribia. Nilipomdokezea wazo hili, alinitolea nje moja kwa moja. Aliniambia wazi hajawahi kuigiza na alikuwa anaogopa sana kuharibu hadhi yake (status).
Nilielewa wasiwasi wake si kila kitu angeweza kukurupuka na kufanya, hivyo ilibidi nitumie muda mrefu kumsaka na kumwomba vikao.
MWANASPOTI: Baada ya hapo, nini kiliendelea hadi akakubali?
ABDUL USANGI: Mambo yalizidi kuwa magumu hasa baada ya kuona ameteuliwa kujiunga na Wasafi; nilihisi sasa kumpata itakuwa ndoto. Lakini siku moja usiku, nilikutana naye Mlimani City, nikamkimbilia. Alinitambua na kuniuliza, “Wewe tena?”, nikamwambia, “Kaka, naomba unisaidie”. Tulikaa chini na nikaanza kumuelezea kwa kina uhusika wa Mr. Chande na jinsi stori ilivyo.
MWANASPOTI: Haji hakuwa na wasiwasi na uwezo wake wa kukabiliana na kamera au kushika mistari (scripts)?
ABDUL USANGI: Alikuwa na wasiwasi sana na suala la kukumbuka mistari ya majibizano ‘dialogues’. Lakini mimi nilimtoa hofu kuhusu kukabiliana na kamera. Nilimwambia, Kukabiliana na kamera siyo tatizo kwako kwa sababu kamera ni sehemu ya maisha yako tangu ukiwa msemaji wa klabu za mpira. Nilimhakikishia timu nzima itakuwepo kumsaidia na kumwelekeza pale anapokwama (cut along the way), na hapo ndipo alipokubali na tukaanza kazi.
MWANASPOTI: Kwa nini ulimweka Haji katika nafasi ya fundi chereani, mazingira ambayo yanaonekana ni ya watu wa hali ya chini sana?
ABDUL USANGI: Hiyo stori nilikuwa nimeshaiandika na nilitafuta mtu sahihi kabisa wa kuvaa uhusika huo. Nilitaka kufanya vitu viwili vikubwa: Kwanza, nilitaka kutengeneza hali ya sintofahamu na msisimko (suspense) kwa watazamaji, wajiulize mtu mkubwa kama Haji atawezaje kuigiza katika mazingira hayo. Pili, tamthilia ya Kombolela inagusa maisha ya watu wa hali ya chini na Haji ana muonekano halisi wa kipwani unaoendana na mazingira hayo.
MWANASPOTI: Waigizaji wengine wa Kombolela waliupokeaje ugeni huu wa Manara?
ABDUL USANGI: Walimpokea vizuri sana na kumpa ushirikiano mkubwa sana wakati wa kurekodi.
MWANASPOTI: Tangu aanze kuonekana, mwitikio wa mashabiki umekuwaje? Je, malengo yako ya kutengeneza “gumzo” yametimia?
ABDUL USANGI: Muitikio umekuwa wa kipekee na wa tofauti sana. Kumeingia mjadala mkubwa mtaani; baadhi ya mashabiki walikuwa na wasiwasi kama kweli angeweza, lakini hilo ndilo nililokuwa naliitaji kutengeneza gumzo. Nashukuru nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kadiri wanavyozidi kumuona, wanaanza kuelewa kwanini alikuwa anafaa kuwa Mr. Chande na sasa wameanza kumkubali sana.
MWANASPOTI: Kumuweka sehemu nafasi moja na kina Mwadawa (Bi Star), hili nalo lilipangiliwa vipi?
ABDUL USANGI: Of course, mara baada ya kuingia kwenye nyumba ya Mzee Kikala, haiepukiki kukutana na wahusika kama hao kutokana na mtiririko wa hadithi yenyewe.