Prime
Bili ya Diamond italipwa na Ali Kiba
JUMAMOSI, Machi 21 (siku ya sikukuu ya Idd), nyota mkubwa zaidi wa muziki hapa nchini, Nasseb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz aliachia wimbo mpya, HAPPY. Ni wimbo fulani wa furaha, sherehe na raha za dunia...bonge moja la wimbo! Ndani yake kuna mstari ambayo Diamond Platnumz anasema,
Where’s Bel Air?
Bring me Don Julio
Casamigo
Big sio junior
Bel Air iko wapi?
Niletee Don Julio
Casamigo
Kubwa sio ndogo.
Hapa Diamond Platnumz alizitaja aina mbalimbali ya pombe za bei mbaya. Kama lilivyo jina la wimbo, HAPPY...yaani furaha, basi hizo pombe ameagiza ili kuiendeleza furaha aliyonayo.
Siku chache baadaye, Jumatano, Machi 25, Ali Kiba kwa kushirikiana na Bien wa Kenya naye akaachia wimbo mpya, Finale! Kama Happy ya Diamond Platnumz, huu nao ni wimbo wa kufurahia maisha... kula raha za dunia...wimbo mzuri sana! Ndani yake kuna mistari ambayo Ali Kiba anasema:
Leo silali, it’s your birthday tonight AGIZIA DORIME
Bili ya Ali, hakikisha hiyo bili asipewe mwingine.
SHIDA NI DORIME
Ali Kiba anasema AGIZIA DORIME...sasa maana ya hii Dorime ndio kisa cha andiko hili. Dorime ni neno la kulia bata huko Nigeria lenye maana ya kibebeo cha pombe za bei mbaya. Yaani mtu akienda kwenye starehe nchini Nigeria, anaangiza Dorime. Ndani yake kunakuwa na pombe mbalimbali za bei mbaya...anastarehe!
Hivi ndivyo inavyoonekana kwenye nyinbo hizi mbili. Diamond Platnumz kaagiza pombe ya bei mbaya kabisa. Hizo pombe atakapoletewa lazima ziwekwe kwenye DORIME. Na hapo ndipo Ali Kiba anapoingilia kati na kusema yeye atalipa hiyo bili.
Yaani Diamond Platnumz anywe tu pombe alizoagiza kwenye dorime, Ali Kiba atalipa! Hii ni moja ya migongano mikubwa ya matukio kuwahi kutokea. Unaweza kudhani labda Ali Kiba alimjibu Diamond baada ya kusikia wimbo, lakini inawezekanaje ule wimbo ukawa umerekodiwa ndani ya muda mfupi namna hiyo? Labda tu imetokea, lakini ni kitu kikubwa sana.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Ali Kiba na Diamond kupasuana kwenye nyimbo zao. Mwaka 2017, Diamond Platnumz alitoa wimbo wa Hip Hop alioimba na Fid Q ulioitwa Fresh. Ndani yake Diamond Platnumz alirusha mishale kadhaa kwa Ali Kiba;
Ukinichukia sikosi hela kwa hiyo kwangu sio kesi
Kuni-compare na Cinderella ahhh hiyo haiwezi kuwa fresh
Simba kutoka mbuga ya Tandale.
Naona wanafosi wanataka tuwe saresare
Viuno vidogo wanataka pensi ya Pepe Kale
Si walitaka kiti, wape kitanda wakalale.
Cinderella ni wimbo maarufu wa Ali Kiba, kwa hiyo hapo moja kwa moja Diamond Platnumz alimaanisha hapaswi kulingalishwa na Ali Kiba. Halafu anaposema SI WALITAKA KITI, KITANDA WAKALALE.
Hapo alimlenga Ali Kiba ambaye wakati ule alikuwa anasema anakalia kiti cha mfalme wa BongoFlava. Kwa hiyo sio kiti tu...apewe kabisa na kitanda akalale. Hii mishale ilikuwa ya moto na haikupaswa kuachwa ipite hivi hivi.
Ali Kiba akajibu kupitia chapisho la kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, akisema; The King I’ll always be a King. Je umeshanitandikia kitanda malkia wangu?
Japo hili jibu lilikuwa la kibabe sana, lakini ni kama Ali Kiba aliona haitoshi, lazima amjibu kwenye mistari. Ndipo 2020 akatoa wimbo wa Mediocre, yaani mtu wa kawaida sana. Wimbo huu kwa tafsiri za kimuziki ulikuwa jiwe kwa Diamond Platnumz, hasa mstari huu. Ushamba mwiko kwa mtoto wa Kariakoo. Sichezi na dada zangu, nacheza na dada’ako.
Hapa Ali Kiba alimchapa Diamond Platnumz kupitia dada yake, Queen Darleen. Zamani Queen Darleen alikuwa kwa Ali Kiba na wakaimba pamoja wimbo wa Nakupenda, mwaka 2005. Wakati huo Diamond Platnumz bado hajatoka na hajui atatoka lini. Kwa kifupi Ali Kiba alimcharaza sana Diamond Platnumz humo.
Hali kama ikatulia hivi, hadi hivi juzi kati, 2004. Diamond alitoa wimbo MAPOZI akishirikiana na Mr Blue na Jay Melody. Ndani yake Diamond Platnumz alisikika akiimba; “Matikiti kudondoka.”
Wimbo ukapokelewa vizuri na ukakimbiza sama YouTube. Lakini siku chache baadaye Nandy akatoa wimbo wa Dah, akimshirikisha Ali Kiba. Wimbo huu ukateka soko na kuushusha kwenye YouTube wimbo wa Diamond Platnumz.
Ali Kiba akaandika kwenye Instagram akimwambia Nandy, “umeangusha matikiti ya watu”.
Hapa moja kwa moja alileta kitendo cha wimbo huo kufanya vizuri zaidi ya wimbo wa Diamond Platnumz wenye mistari ya matikiti. Hayo ndio yamekuwa maisha ya wawili hawa kama wasanii wakubwa hapa nchini.
Japokuwa historia inaonyesha kwamba awali walikuwa pamoja, lakini maisha yakawatenganisha na kila mmoja kupita njia yake. Tangu hapo ni vijembe na mafumbo huku wakiwagawa mashabiki wa muziki. Na sasa HAPPY na FINALE zinaleta hadithi nyingine. Diamond Platnumz aagize tu DORIME, bili ni ya Ali Kiba.