Prime
Coy Mzungu amaliza utata, ataja sababu ya kukwepa ndoa
Conrad Kennedy 'Coy Mzungu' siyo jina geni katika tasnia ya uchekeshaji. Ni mbunifu, mwanzilishi na mkurugenzi wa jukwaa maarufu la ucheshi la Cheka Tu na amekuwa muhimu katika kukuza na kuibua sanaa hiyo ya kusimama na kuchekesha jukwaani 'Stand-up Comedy', huku pia akitoa fursa kwa wachekeshaji chipukizi.
Nje ya tasnia hiyo, Coy ana maisha binafsi yaliyojaa mafanikio, mapito ikiwamo bifu za hapa na pale, nafasi yake katika Bongo Stars Search na zaidi ni mjadala kuhusu uhusiano wake wengi wakihoji kuhusu ndoa.
Kuhusu ndoa
Hapa anafunguka kuhusu mipango yake ya ndoa na anachosisitiza ni hatatimiza jambo hilo kwa sababu ya kuwafurahisha watu bali kutokana na mipango yake binafsi.
Licha ya umaarufu wake amekuwa akilinda sana maisha yake ya mahusiano na amewahi kukiri ana mtu lakini hajaona muda sahihi wa kufunga ndoa, huku wengi wakihoji anaogopa changamoto za ndoa?
“Mapenzi yapo, siwezi kusema sina mtu, lakini ndoa ni jambo kubwa sana, siwezi kukurupuka kwa sababu ya presha ya watu au umaarufu, nataka nifanye maamuzi sahihi kwa maisha yangu, sio kwa kufurahisha watu, ndoa si mchezo, ni maisha ya mtu na familia yake, hivyo lazima nijipange vizuri kwanza.”
Utajiri na maisha ya kifahari
Kutokana na kazi hiyo, Coy amekuwa na mafanikio makubwa na anafunguka kalba alianza bila kitu na kusisitiza komedi inalipa kama utajituma na sasa ana mikataba mingi huku akitoka kwenye kufanya shoo kubwa.
“Nilianza bila kitu, leo hii watu wanaona mafanikio. Hii ni kazi ngumu sana nyuma ya pazia. Komedi inalipa, lakini lazima ujitume, uwe na nidhamu na ubunifu wa hali ya juu, sio kitu cha kubahatisha.”
Maisha yake yamekuwa somo kwa vijana wengi ambao wamejiunga na tasnia hiyo na sasa wanaanza kuona matunda.
Anaendelea kuwa mmoja wa mastaa wanaovuta hisia za wengi na maisha yake yanaonyesha kuwa nyuma ya vicheko kuna juhudi, maamuzi magumu na misimamo thabiti, ni wazi safari yake bado inaendelea na mengi zaidi yanatarajiwa kutoka kwake.
Kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia hiyo, alitunukiwa tuzo mbalimbali ikiwamo ya Game Changer aliyokabidhiwa wakati wa utoaji wa tuzo za Tanzania Comedy 2024/2025. Tuzo hiyo ilikuwa kama ishara ya kutambua mchango wake katika kubadilisha tasnia ya uchekeshaji.
Kuibua na kumiliki vipaji (Cheka Tu)
Kutokana na jukwaa la Cheka Tu, Coy amesaidia kukuza vipaji vingi vipya vya uchekeshaji. Hata hivyo, suala la umiliki wa jukwaa hilo limekuwa likizua maswali mara kwa mara.
“Cheka Tu ni zaidi ya shoo, ni ndoto niliyoiunda kutoka mwanzo, nimepitia changamoto nyingi kuifikisha hapa ilipo, watu wanaweza kusema chochote, lakini ukweli unabaki pale pale hii ni kazi yangu na ninaijua thamani yake.”
Anasimamia anachoamini, hapendi bifu
Coy Mzungu amejijengea taswira ya mtu anayesimamia anachokiamini bila kujali atamkera nani na mara kadhaa amejikuta akihusishwa na migogoro ya kimtazamo katika tasnia hiyo, hasa kuhusu masuala ya umiliki na uendeshaji wa majukwaa ya komedi.
Analiambia Mwanaspoti: "Kuna mambo mengi watu hawaelewi kwenye tasnia, mimi ninasimamia ukweli hata kama unaumiza, kama ni mali yangu, nitaisema ni yangu, kama kuna mtu anataka kuchukua sifa zisizo zake, lazima nisimame kidete, hii ni kazi kama kazi nyingine, lazima kuwe na heshima na mipaka.”
Nafasi yake Bongo Star Search
Kuteuliwa kwake kuwa jaji wa Bongo Star Search ni hatua nyingine kubwa katika maisha yake ya sanaa, wengi wameona kama ishara ya kukua kwake zaidi ya uchekeshaji na kuingia kwenye tasnia pana ya burudani.
“Kuwa jaji siyo tu kukaa na kutoa alama, ni jukumu la kusaidia kukuza vipaji, ninaamini uzoefu wangu kwenye jukwaa utanisaidia kuona vipaji halisi na kuwashauri washiriki kwa usahihi.”
"Baadhi ya wadau bado wanajiuliza kama mchekeshaji anaweza kuwa jaji mkali kwenye muziki, mimi niko pale kama jaji kwa upande wa uchekeshaji, japo kwenye muziki pia nina uwezo wa kutambua kitu."