Diddy aondoa jumba lake sokoni kesi ikianza tena
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Diddy aiweke nyumba hiyo sokoni, kipindi ambacho jina lake lilianza kutikiswa na tuhuma nzito za biashara ya ngono, racketeering na usafirishaji wa watu kwa ajili ya vitendo vya ngono kinyume cha sheria.
NYOTA wa muziki na mfanyabiashara maarufu duniani, Sean Combs ‘P Diddy’, ameondoa sokoni jumba lake la kifahari lililopo Holmby Hills jijini Los Angeles lenye thamani ya Dola 61.5 milioni ambazo sawa na zaidi ya Sh150 bilioni, huku giza la kesi nzito ya jinai ya shirikisho likizidi kumzingira.
Hatua hiyo imekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Diddy aiweke nyumba hiyo sokoni, kipindi ambacho jina lake lilianza kutikiswa na tuhuma nzito za biashara ya ngono, racketeering na usafirishaji wa watu kwa ajili ya vitendo vya ngono kinyume cha sheria.
Rekodi zinaonyesha kuwa jumba hilo liliondolewa rasmi kwenye orodha za mauzo Desemba 24 mwaka jana, bila kutolewa maelezo yoyote kwa umma na upande wa msanii huyo.
Nyumba hiyo ilitangazwa kuuzwa Septemba 2024, siku chache tu kabla ya Diddy kukamatwa jijini New York. Baada ya kesi ndefu iliyovuta hisia za dunia, msanii huyo alikana mashtaka yote, huku mawakili wake wakisisitiza kuwa vitendo vilivyotajwa vilifanyika kwa ridhaa.
Hata hivyo, mahakama ilimhukumu kifungo cha miezi 50 ambayo ni sawa na miaka minne baada ya kupatikana na hatia kwenye makosa mawili yanayohusiana na ukahaba, pamoja na kutozwa faini ya dola 500,000.
Jumba hilo lenye vyumba 10 vya kulala na mabafu 13, ambalo Diddy alinunua kwa dola milioni 39 mwaka 2014, liliingia kwenye historia ya vichwa vya habari Machi 2024 baada ya mawakala wa Homeland Security kulifanyia upekuzi mkubwa.
Upekuzi huo ulikuwa sehemu ya uchunguzi mkubwa uliogusa pia makazi yake mengine huko California na Florida, ikiwamo jumba lake la Miami lenye thamani ya dola milioni 48.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, nyumba hiyo ya Holmby Hills ilitumika kama kituo cha mikusanyiko iliyodaiwa kuitwa “freak off,” ambako Diddy anatuhumiwa kutumia pesa na umaarufu wake kuwadhulumu wanawake kingono.
Mahakamani, mawakala walieleza kupatikana kwa ushahidi mzito ikiwamo vipande vya silaha aina ya AR-15, viatu vingi vya kisigino kirefu, vifaa vya ngono, chupa kadhaa za mafuta ya watoto pamoja na dawa za kulevya kama cocaine na cetamine.
Vyanzo kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari vilidai kuwa nyumba za Diddy huko Beverly Hills na Miami zilipata uharibifu mkubwa wakati wa misako ya mawakala wa shirikisho.
Cha kushangaza, tangazo la mauzo ya jumba hilo halikuwahi kufichua kuwa linamilikiwa na mtu mashuhuri wala kuhusishwa na uchunguzi wa serikali, bali lilisisitiza anasa zake, ukubwa wa mita za mraba 1,579 na eneo lake la kifahari linalohesabika kuwa kati ya maeneo ghali zaidi Los Angeles.
Wataalamu wa sheria wanasema licha ya kifungo, Diddy bado ana haki ya kuuza mali hiyo akiwa gerezani. Hata hivyo, serikali inaweza kuingilia mapato ya mauzo kwa kuweka hati ya madai, jambo linaloweza kuchelewesha au hata kuzuia fedha hizo kumfikia.
Kwa sasa, jumba hilo likiwa halipo sokoni, wachambuzi wa masuala ya mali wanadai Diddy anaweza kuligeuza kuwa ‘trophy property’, ikiwamo kulikodisha kwa gharama kubwa zinazoweza kufikia dola 20,000 kwa usiku mmoja.
Nyumba hiyo ni sehemu ya orodha ndefu ya mali za kifahari zilizowahi kupita mikononi mwa Diddy, ikiwamo jumba la Star Island alilonunua mwaka 2021 kwa dola milioni 35, lililokuwa mali ya Gloria na Emilio Estefan.
Wakati joto la kesi likiwa bado halijashuka kabisa, hatma ya jumba la ‘freak off’ inaendelea kubaki kitendawili kikubwa. Je, ni mali itakayookoa heshima ya Diddy au ushahidi wa kudumu wa kuanguka kwa himaya yake?