Fahyma wa Rayvanny apewa onyo
Muktasari:
- Fahyma aliliambia Mwanaspoti, wiki iliyopita alituma picha katika akaunti ya Instagram, ndipo Bodi ya Filamu walimuita na kumpa maelekezo ya sheria na kanuni kuhusu maadili.
MWANAMITINDO maarufu na muigizaji wa filamu Bongo, Fahyma maarufu Fahyvanny a.k.a 'Mrs Chui', amepewa onyo na Bodi ya Filamu Tanzania kutokana na picha jongefu zilizorushwa katika mtandao wa kijamii zikionyesha amevaa mavazi yasiyo na staha.
Fahyma aliliambia Mwanaspoti, wiki iliyopita alituma picha katika akaunti ya Instagram, ndipo Bodi ya Filamu walimuita na kumpa maelekezo ya sheria na kanuni kuhusu maadili.
"Nashukuru suala langu limeisha salama. Niseme tu, nimekoma na sitarudia tena kutuma picha ambazo hazina maadili katika mitandao," alisema mrembo huyo anayetamba katika tamthilia ya Huba, aliyeongeza;
"Hivyo nimeweza kuzifahamu baadhi ya sheria na kanuni na ninaahidi nitakuwa balozi mzuri kwa watu wengine."
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga, aliyezungumza na Mwanaspoti, alifafanua kwa kuwasihi wasanii wa filamu kuendelea kulinda maadili ya nchi katika kazi za tasnia pamoja na mienendo yao.
"Mara nyingi tumekuwa na utaratibu wa kuzungumza na wasanii, sasa Fahyma kuna picha kadhaa alizokuwa amezirusha katika mtandao wa Instagram yake hazikuwa nzuri, pia kutakiwa kuwa makini na suala la mitandao, hivyo ndiyo vitu tulivyomkumbusha tena kwa njia chanya kabisa, sisi kama Bodi ya Filamu tuna wajibu wa kuwakumbusha wasanii kabla hatujaenda kwenye upande wa adhabu," alisema DK Gervas Kasiga.
Fahyma alisema anapenda picha kuliko kitu chochote, hivyo hawezi kukaa wiki bila kupiga picha na kila akifanya hivyo huwa anatumia Sh2 milioni, ambazo hizo hela anazogharimia kulipia hoteli na mavazi pamoja na mpigapicha.
Fahyma amejaaliwa kipaji cha kuwa mwanamitindo, pia wamekuwa wapenzi kwa muda mrefu na msanii wa Bongo Fleva Rayvanny na wamepata mtoto mmoja anayeitwa Jaydan.