Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Finale ya Alikiba inavyocheza jirani na Arsenal

FINALE Pict


JINA la Alikiba kwa sasa lipo kwenye vichwa vya habari kupitia wimbo wake mpya, Finale (2026), ambao kwa sehemu pia umewagusa mashabiki wa Arsenal, timu yenye kiu kubwa ya ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL).


Katika wimbo huo uliotayarishwa na Abbah na Hendricks Sam, Alikiba kutoka Kings Music ameshirikiana na mwanachama wa zamani wa kundi la Sauti Sol kutoka Kenya, Bien, ambaye amefanya kazi na wasanii wengi wa Bongo. Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wanadai wimbo siyo wa Alikiba, bali wa Bien, lakini ukweli ni kwamba ni ushirikiano wa wote wawili; yaani hakuna aliyemshirikisha mwenzake, na ndiyo sababu katika utambulisho wake imetumika alama “X” na si “ft” (featuring).


X ambayo asili yake ni alama ya kuzidisha katika hisabati, kwenye jina la wimbo (title) ina maana ya ushirikiano kati ya wasanii wawili wenye uwezo na mchango sawa au unaolingana katika kazi husika, na si suala la mmoja kumshirikisha mwingine.

Finale ni wimbo unaohimiza starehe, ambapo Alikiba na Bien wan afurahia pamoja na wale wanaowapenda, ila zaidi unazungumzia kufika mwisho wa safari ya kusaka mapenzi ya kweli.

Mhusika mkuu wa wimbo huo ni mwanaume ambaye amepitia mahusiano mengi, lakini sasa anaamini kuwa amempata yule anayemfaa. Neno “Finale” linaashiria mwisho wa kutafuta na mwanzo wa uhusiano wa dhati wenye kujitoa kwa asilimia 100.

Wimbo huu umechanganya ladha laini ya Afropop na Bongofleva, huku ukibebwa zaidi na sauti nzuri na uwasilishaji wenye hisia, jambo linaloufanya kuwa moja ya kolabo bora katika muziki wa Afrika Mashariki.

Katika video yake iliyoongozwa na Chiki Kuruka, Bien anaonekana akijumuika na marafiki wakiwemo wasanii wenzake wa Sauti Sol pamoja na rapa Khaligraph Jones, ambapo wanatazama mechi ya Arsenal ambayo inaibuka na ushindi.

FINA 02

Marafiki zake wengi wamevaa jezi ya Arsenal, klabu inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la EPL msimu huu, ikiwa ni miaka 22 tangu walipotwaa chini ya kocha Mfaransa, Arsène Wenger, msimu wa 2003/04 bila kupoteza mchezo wowote.

Msimu wa EPL unatarajiwa kumalizika Jumapili, Mei 24, na bila shaka hadi wakati huo bado wimbo Finale utakuwa unafanya vizuri. Endapo Arsenal itafanikisha jambo lake, basi wimbo huu utakuwa na maana zaidi, na wazo la kuitumia Arsenal kama kielelezo cha ushindi litakuwa limefanikiwa kwa asilimia 100.

Hata hivyo, Alikiba yeye si shabiki wa Arsenal; katika EPL, timu yake ni majogoo wa jiji, Liverpool, ambao ndio mabingwa watetezi. Hivyo Arsenal ikibeba awamu hii ni sawa na yeye tu kuwakabidhi taji, na kubwa zaidi ni kutimia kwa kile walichotabiri kupitia kolabo yake na Bien, Finale (2026).

Ikumbukwe mapambano haya ya Arsenal ya kutwaa EPL hayatofautiani sana na yale ya Liverpool, kwani nao walingoja miaka mingi hadi msimu wa 2019/20 walipochukua chini ya kocha Mjerumani, Jurgen Klopp, ikiwa ni baada ya miaka 30.

Ushirikiano huu wa Alikiba na Bien umepokelewa vizuri na mashabiki na hata kuteka mazungumzo mtandaoni. Video ya wimbo huo inazidi kuvutia watazamaji wengi YouTube, ambapo ndani ya siku tano tangu kuachiwa kwake ilitazamwa mara milioni 4.7.

Hii ni mara ya pili kwa wasanii hao kukutana katika wimbo mmoja; awali Alikiba alishirikishwa na Sauti Sol katika wimbo wao, Unconditionally Bae (2016), ambao pia ulifanya vizuri kwa wakati huo.

FINA 01

Kwa matokeo hayo, Bien anakuwa msanii wa kwanza kutoka Kenya kushirikiana na mastaa wote wa Bongofleva wanaofanya vizuri kwa sasa, na ndio hasa wanaoutangaza muziki huo.

Mbali na Alikiba, Bien ameshafanya kazi na Harmonize (I Made It), Darassa (Nobody), Joh Makini (Formula), Marioo (Nairobi), Jux (Lucky Now), Rayvanny (Rakata), Diamond Platnumz (Katam) na kadhalika. Kolabo hizo zimekuja baada ya kuanza kufanya kazi peke yake (solo) kufuatia mafanikio makubwa akiwa na Sauti Sol tangu mwaka 2005, huku wakivuma na nyimbo zao kali kama Still The One (2013), Sura Yako (2013), Kuliko Jana (2016), Melanin (2017), Suzanna (2020) n.k.

Akiwa ametoa Extended Playlist (EP) moja, Bald Men Love Better (2021), pamoja na albamu moja, Alusa Why Are You Topless? (2023), Bien amejitambulisha kama mmoja wa waimbaji wakali zaidi Afrika Mashariki.

Ushirikiano wake na Alikiba, mshindi wa MTV EMAs 2016, ni mradi uliowaleta pamoja waimbaji wakali, kwani nao Sauti Sol waliwahi kushinda MTV EMAs 2014, tuzo za muziki ambazo hufanyika barani Ulaya kila mwaka katika nchi mbalimbali.