King Kikii: Watanzania tupendane

MKE wa mwimbaji mkongwe wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ amewaomba Watanzania waendelee kumwombea mumewe ili hali yake itengemae, huku mwanamuziki huyo akivunja ukimya kwa kutamka maneno machache yenye ujumbe mzito.
Mtunzi na mwimbaji huyo wa zamani wa Marquiz du Zaire na Orchestra Double O anayemiliki bendi ya Le Capital ‘Kitambaa Cheupe’ amefanyiwa upasuaji mkubwa wa pingili za shingoni, amezungumza kwa mara ya kwanza tangu upasuaji huo ufanyike na kuhimiza amani na upendo.
Akizungumza na Mwanaspoti nyumbani kwake kwa sauti hafifu, King Kikii anasema amefurahia kupata ugeni wa Mwananchi Communications Ltd na kusisitiza kuwa kwake ni jambo kubwa na kutoa wosia akitaka watu waishi kwa amani na upendo.
“Ni vizuri tukaishi kwa upendo na amani, Watanzania waniombee ili nirejee kwenye afya yangu, asante na Mungu awatangulie mnapoondoka,” alisema King Kikii.
Awali mkewe, anayejulikana kwa jina la Costansia Kalanda, alisema hali ya mume wake haijatengemaa kwa maana hajaanza kutembea na kuongea kama alivyokuwa awali na kufichua tatizo lake lilichangiwa na kusumbuliwa na pingili za mgongo zilizoathiri zile za shingo kusagika na kufanyiwa upasuaji, huku akitiwa moyo ataimarika taratibu kabla ya kurejea kawaida.
“Nilianza kuona dalili takribani mwaka mmoja hivi, kwani alikuwa amebadilika kutembea, nikawa nachukulia labda uzee, kama wiki tatu hivi ndio akaanza kuumwa nikampeleka hospitali,” alisema mkewe huyo maarufu kama Mama Kitambaa Cheupe.
“Wakati tunakwenda hospitali alikuwa anatembea mwenyewe, akaoga mwenyewe baada ya kufika na kufanyiwa upasuaji ndio akawa hivi, daktari alituambia amepigwa ganzi kubwa itakuwa inamtoka taratibu, ikiisha na akianza kusimama ndipo atakapoanza kuongea,” alisema mkewe huyo na kuongeza kuwa King Kikii ni baba wa wengi, hivyo kama kuna mtu anataka kutoa msaada anakaribishwa kwenda nyumbani kwake au kumtumia kwa namba zake na sio kuwasikiliza wanaoongea kwenye mitandao ya kijamii.
“Niliwazuia watu kuja kumuona ila niligundua simtendei haki, King Kikii ni baba wa wengi, akiwaona anaona faraja kwangu na kwake pia.
Aliongeza kuwa watu hawapaswi kuzungumza yale yasiyokuwa mema juu yake: “Lakini sio kumtangazia kwamba karudishwa nyumbani kwa kushindwa kumudu matibabu sio kweli, watoto wake wamelimudu hilo pia kuna watu wananitumia kwenye simu yake kwani kwa sasa ninayo mimi.”
King Kikii aliyeanza muziki miaka ya 1960 nchini DR Congo kabla ya kuja nchini na kutamba makundi mbalimbali ya muziki ikiwamo Marquis du Zaire, Orchestra Safari Sound (OSS), Double O, Zaita Musica kabla ya kuunda bendi yake inayoendelea kuwapa burudani mashabiki.