Prime
Sakata la Martha Mwaipaja Beatrice lafikia hapa, Shusho atajwa

Muktasari:
- Kipande cha sauti kilichosikika mitandaoni kikiwahusihsa dada hao kilitrendi na Beatrice anayedai ni dada wa Martha, alikuwa akiongea kwa maneno makali kumshutumu Martha aliyesikika akiongea kwa upole kumsihi ndugu yake huyo kuacha mara moja kumzungumzia ingawa hakufanya hivyo.
NI miezi mitano sasa imepita tangu kuibuka kwa sakata la Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Martha mwaipaja na dada yake Beatrice aliyemtuhumu mitandaoni anamiliki pesa nyingi lakini hamsaidii mama yake na amejitenga na familia.
Kipande cha sauti kilichosikika mitandaoni kikiwahusihsa dada hao kilitrendi na Beatrice anayedai ni dada wa Martha, alikuwa akiongea kwa maneno makali kumshutumu Martha aliyesikika akiongea kwa upole kumsihi ndugu yake huyo kuacha mara moja kumzungumzia ingawa hakufanya hivyo.
Baada ya hapo, Martha alikuwa kimya na hakuongea kokote juu ya sakata hilo na hata alipotafutwa na waandishi wa habari aligoma kulizungumzia na kusema anamwachia Mungu ndiye atajibu.
Katika kuhakikisha anafunguka juu ya sakata hilo, Mwanaspoti kupitia ukurasa huu wa Dakika 5 Na... lilimsaka kwa muda mrefu na kubahatika kukutana naye Mlimani City na kuzungumza naye mambo mbalimbali ikiwamo Tamasha la Mtoko wa Pasaka litakalofanyika Aprili 20, Ukumbi wa Super Dome, Masaki na sakata hilo na dada yake.

Hujawahi kutoa neno kuhusu tuhuma za ndugu yako Beatrice mitandaoni, una lipi la kusema?
"Unajua kunyamaza ndiyo kuniponya kwangu, nilikuwa na uwezo wa kuongea kila kitu lakini nimeona kutumia busara ndiyo njia pekee kwangu na sikutaka pia kuongelea kwani familia zina mambo mengi sana na vitu vya familia huwa haviwekwi wazi."
Ulikuwa na hali gani wakati Beatrice anatoa shutuma hizo?
"Wewe acha tu, hali niliyokuwa napitia ni mbaya sana, nilikuwa nakaa macho nashtuka asubuhi imefika na sijui imefikaje. Hapo ndipo nilipojua kuna watu wanajua kutukana, yaani utakuta mtu hata hakufahamu vizuri, lakini anakuongelea mambo ya uongo hadi unasema umemkosea nini huyo mtu."
"Nimejikuta nyimbo zangu nilizokuwa naimba zamani ndio zinanifariji kwa sasa, nyimbo kama 'Haufanani' 'Nifundishe kunyamaza', 'Usikate Tamaa' na nyingine ni zimenipa faraja sana kwenye matatizo niliyopata hivi karibuni."
Kumbe Christina Shusho alimfariji
"Kitu ambacho sikutegemea ni msanii mwenzangu Christina Shusho kuingia kwenye hili sakata langu na kuanza kusimama na mimi kunitetea. Ukweli nilifarijika na kushangaa. Ndipo nilipozidi kumpenda. Unajua kwenye maisha kila mtu anahitaji mtu awe upande wake, sikujua kama Christina Shusho atakuwa upande wangu, nampenda zaidi."
"Nilipigiwa simu na wachungaji wengi kunipa moyo, watu wengi alinipigia simu ila Shusho alijitokeza kunitetea hadharani na bado akasema."

Vipi, mambo yameshaisha na umemsamehe Beatrice na mama yako mzazi?
"Mimi nimezaliwa, siwezi kuweka vitu moyoni na huwa nasamehe mtu ila siwezi kuwa karibu na wewe. Hivyo nimewasamehe ila sitaweza kuwa nao karibu, unajua mwanzo nilisema familia zetu zina mambo mengi sana. Mimi nimetupiwa kila neno ila watu hawajasikia neno kutoka kwangu."
"Sijawahi kuzungumza kama yule aliyekuwa anaongea ni mama yangu au sio, kuna vitu vingi nyuma ya pazia watu hawavijui na sitasema kamwe. Pia kuhusu Beatrice sijawahi kujibu zile shutuma zake kwangu ila najua siku zote mwenye kitu ndiye anapigwa mawe."
Kuna maneno mama yako aliongea pia kutomjali hii ni kweli?
"Narudia tena, sijawahi sema yule ni mama yangu au sio mama yangu, hivyo kuna vitu nyuma ya pazia hamvijui na sitakaa kuvisema kamwe, kitu kikubwa mzazi kama mzazi anatakiwa kuwa na hekima na akili nyingi na najua kesho yangu inatengenezwa na mzazi, hivyo mimi ilipofikia nilikuwa nataka hekima ya Mungu tu.
"Kumbuka mimi ni mama, naelewa uchungu na mipaka ya wazazi. Vile utakavyomlea mtoto ndivyo akuavyo, wazazi msiwachukize watoto wenu. Mimi siwezi kufanya hicho kitendo."

Ni kweli unajitenga na Familia?
"Mimi nina asili ya kujitenga yaani niko hivyo na kama ndugu basi tujitahidi tuwe na adabu ili tupate kitu, kama ndugu huna heshima mimi huwezi kukipata yaani nakaa mbali na wewe. Wewe niheshimu ili upate kitu changu na siyo tu kwa ndugu hata kwa watu wengine mimi huwa sina watu wa kujichanganya changanya sana."
Una lolote la kuongea kuhusu Beatrice?
"Mimi niseme tu kitu kimoja, ameongea sana mambo ya uongo na kunidhalilisha, sijanyanyua mdomo wangu wala kwenda sehemu yeyote kufungua kesi, ila wakirudia tena nitaenda kuwafungulia kesi sitakaa kimya."
Vipi kuhusu kuimba umeacha?
"Hapana sijaacha kuimba, niwaambie tu mashabiki zangu kazi mpya zinakuja nyingi tu, wasikatishwe tamaa na yaliyotokea juu ya familia yangu na wala sioni aibu kwa yaliyotokea na kushinda, ni lazima mapambano yanaendelea kwenye kazi."
Una watoto?
"Ndio nina watoto wawili wa kike na wa kiume, wa kiume sio mtu wa kujitokeza sana ila wa kike ni huyu Joan ambaye alikuwa anapambana na watu kwenye mitandao na wanamtukana sana mwanangu. Mimi kama mzazi naumia sana, sema nashukuru nimepata watoto wenye kunipenda sana mimi."

Huyu Joan ni mtoto wako wa kumzaa?
"Ndio ni mtoto wangu kabisa wa kumzaa, najua mwanangu anapigwa sana vita na vile tu ni mdogo hawezi kubeba mambo kama mimi. Ndiyo maana anajibu jibu sana watu kwenye mitandao wale wanaomtukana."
Neno moja kwa watu wa mitandaoni
"Neno langu kwa wale watu watukanaji, niwaombe waache roho chafu za kutukana watu ili Mungu awabariki, wasipende kushadadia vitu ambavyo hawavijui ukweli wake."