Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lupita Nyong'o: Alichati na Ferguson kabla ya kutwaa tuzo ya Oscar

Lupita ameshiriki kwenye filamu nyingi, lakini hii ilikuwa mara yake ya kwanza kunyakua tuzo kubwa kama hiyo na kumulikwa na kamera na kuonekana karibu duniani nzima.

Muktasari:

  • Wote walisema yao, lakini mwigizaji mmoja wa filamu hiyo aliyekuwa katia fora, alikuwa mrembo wa Kikenya, Lupita Nyong’o. Mrembo huyo alitoa hotuba iliyogusa mioyo ya wengi waliokuwa ukumbini hapo wakati alipoitwa jukwaani kwenda kuchukua tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike Msaidizi kupitia filamu hiyo ya ‘12 Years A Slave’

LOS ANGELES, MAREKANI

ULIKUWA usiku wa machozi ya furaha kwa washiriki na wahusika wa filamu ya ‘12 Years A Slave’, wakati filamu hiyo iliponyakua tuzo ya Oscar ya Filamu Bora juzi Jumapili usiku.

Prodyuza Brad Pitt aliwashukuru washiriki wote kwa ushindi huo, wakati mwongozaji wa filamu hiyo, Steve McQueen alimshukuru mama yake, Mary kwa kumfanya kuwa shupavu na kubainisha kwamba filamu hiyo haizungumzii tu maisha ya kimapambano bali namna ya kuishi.

Wote walisema yao, lakini mwigizaji mmoja wa filamu hiyo aliyekuwa katia fora, alikuwa mrembo wa Kikenya, Lupita Nyong’o. Mrembo huyo alitoa hotuba iliyogusa mioyo ya wengi waliokuwa ukumbini hapo wakati alipoitwa jukwaani kwenda kuchukua tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike Msaidizi kupitia filamu hiyo ya ‘12 Years A Slave’.

Amwaga machozi

Kutambua ni kipengele kilichokuwa na ushindani mkali, Lupita alishindwa kujizuia na kumwaga machozi baada ya kutajwa kuwa mshindi. Maneno yake ya huzuni aliyosema kwenye steji yaliamsha mioyo ya waliokuwapo ukumbini hapo kabla ya kutokwa na machozi na kuufanya ukumbi mzima kuzizima.

Kwenye filamu hiyo, Lupita aliigiza kama msaidizi wa kazi za nyumbani, ambaye alikumbana na matatizo ya kubakwa mara kwa mara na bosi wake. Hisia kama hizo za kwenye filamu, Lupita alizipeleka jukwaani kwenye hotuba yake na kuwafanya wengi kuingiwa na huzuni.

Kitu kingine kilichomtoa machozi Lupita ni kwamba tuzo hiyo ni kama ilikuwa zawadi kwake kwani siku moja kabla, kwa maana ya Jumamosi, alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo alitimiza umri wa miaka 31. Lupita ameshiriki kwenye filamu nyingi, lakini hii ilikuwa mara yake ya kwanza kunyakua tuzo kubwa kama hiyo na kumulikwa na kamera na kuonekana karibu duniani nzima.

Mastaa wamkubali

Mwigizaji mashuhuri, mrembo Jennifer Lawrence, ambaye alikuwa akichuana na Lupita kwenye tuzo hizo, aliwaambia marafiki zake kwa siri kwamba anataka Lupita ashinde kwa sababu anastahili.

Staa wa filamu, mrembo Angelina Jolie alionekana akitoka machozi wakati alipokuwa akimpongeza Lupita kwa ushindi wake, kabla ya prodyuza wa filamu hiyo, Brad ambaye alionekana akimfariji mrembo huyo wa Kenya kutokana na kufanya vizuri kwenye filamu na kuvuna matunda ya ushindi.

Filamu ya ‘12 Years A Slave’ tangu ilipoonyeshwa kwenye maonyesho ya filamu ya Telluride, Agosti mwaka jana, mrembo Lupita amekuwa maarufu na kuwa kivutio kwa kampuni mbalimbali na wacheza filamu mashuhuri duniani.

Azungumza na Ferguson

Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alihudhuria sherehe hizo akiwa na mkewe, Lady Cathy. Wakati Mskochi huyo akitania kwamba kwa sasa anakwenda kila mahali kwa sababu hana kitu cha kufanya, alisema alipata muda wa kuzungumza na mrembo Lupita kabla ya kuchaguliwa kuwa mshindi usiku huo na kunyakua tuzo.

“Nilikuwa kwenye upande wa siti E, palikuwa pazuri sana,” alisema Ferguson.

“Nilikuwa nimeketi mahali pazuri na kuwaona vizuri mastaa wengi wa filamu. Baadhi yao nilizungumza nao kabla ya sherehe, lakini usiku ule nilichati (kuzungumza) na Lupita na kumtakia heri na hatimaye alishinda.”

Ferguson alizitaja baadhi ya filamu anazozipenda ni ‘Gone With The Wind’, ‘The Godfather’, ‘The Searchers’ na ‘12 Angry Men’.

Aandamana na familia yake

Lupita ameingia kwenye vitabu vya kihistoria baada ya kuwa Mkenya na Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Oscar, ambazo ni maarufu zaidi duniani. Kwenye filamu hiyo, Lupita aliigiza kama Patsey.

Mrembo huyo aliandamana na familia yake, baba yake (Profesa Anyang’ Nyon’go), mama yake (Dorothy Nyong’o) na mdogo wake wa kiume na kuufanya usiku huo kuwa na hisia kubwa baada ya kuwabwaga waigizaji nguli Oprah Winfrey na Jennifer Lawrence, aliyekuwa mpinzani wake wa karibu.

Tangu kutoka kwa filamu hiyo iliyosimulia maisha ya utumwa kwa watu weusi, Lupita amekuwa akipamba majarida mbalimbali ya mitindo kote Marekani. Mbali ya kuwa mwigizaji, anafanya vizuri pia kwenye soko la mitindo kutokana na pambo ambazo amekuwa akijifunika zilizoandamana na rangi yake nyeusi.

Akikabidhiwa tuzo hiyo, mzaliwa huyo wa Mexico aliyekulia Kenya, aliachia maneno mazito yenye hisia kali yaliyomsukuma hata naye kulengwa na machozi.

“Ni fursa ya kipekee kwamba mateso na machungu ya mtu aliyewahi kuishi ndiyo yanayonipa furaha kubwa katika maisha yangu.  Nataka kumshukuru sana Patsey na Solomon Northump kwa kuelezea yaliyowasibu. Kwa mwongozaji, Steve McQueen, ninayemheshimu sana, namshukuru kwa kunipa fursa hii ambayo imekuwa ni ya fanaka tele katika maisha yangu. Kwa kumalizia, haijalishi unakotoka mtu, la muhimu ni kuhakikisha unafanikisha ndoto zako na kuishi kuona zikitimia, asanteni sana,” alisema ukumbini hapo na kuwatoa machozi wengi.