Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lupita Nyong'o: Mkenya anayetesa Hollywood

Muktasari:

  • Filamu hiyo imempa umaarufu mkubwa na imemsaidia kupata mataji kadhaa huku akiteuliwa kuwania Tuzo za Oscar dhidi ya nguli Oprah Winfrey.

MWIGIZAJI Mkenya, Lupita Nyong’o, anayetamba Hollywood, amewavutia maprodyuza wakimhitaji aigize kwenye filamu zao baada ya kufanya vizuri katika filamu ya ‘12 Years A Slave’ iliyoigizwa huko Marekani.

Filamu hiyo imempa umaarufu mkubwa na imemsaidia kupata mataji kadhaa huku akiteuliwa kuwania Tuzo za Oscar dhidi ya nguli Oprah Winfrey.

Oprah alimsifia Lupita akimtaja kuwa ni mwigizaji wa aina yake baada ya kumfanya abubujikwe na machozi alipoitazama filamu hiyo.

Tangu kuigiza kwenye filamu hiyo yenye hisia kali na yenye ujumbe mzito wa udhalimu kwa watu weusi ambapo alivaa uhusika wa ‘Patsey’, Lupita ameishia kuwa maarufu akipamba majarida tofauti ya mitindo katika nchi za Ulaya na Marekani.

Filamu hiyo inazungumzia matukio ya kweli ya mateso ya miaka ya 1853 waliyopitia wahusika wakuu Patsey na Solomon Northp (Chiwetel Ejior) walipokuwa watumwa kwenye shamba la pamba la lodi Edwin Epps (Michael Fassbender) baada ya kutekwa nyara.

Mwaka uliopita katika orodha ya filamu bora za BBC, ‘12 Years A slave’ ilichukua nafasi ya kwanza na katika orodha ya Jarida la Forbes 2013 ya wanawake wachanga wenye ushawishi mkubwa barani Afrika, Lupita alishika nafasi ya 15.

Lupita alizaliwa mwaka 1983 akiwa ni mtoto wa pili kati ya nduguze sita. Alizaliwa Mexico wakati wazazi wake Wakenya walipokwenda mafichoni kutokana na utawala dhalimu wa wakati huo.

Baba yake Profesa Anyang’ Nyong’o ni mwanasiasa mashuhuri nchini ambaye kwa sasa ni Seneta wa Jimbo la Kisumu.

Mwigizaji huyu aliyelelewa Kenya na kusomea Marekani, ana Shahada ya Uigizaji kutoka Chuo Kikuu cha Yale na taaluma yake ilianzia nchini alipoigiza kwenye msururu wa sinema ya ‘Shuga’ iliyoshinda MTV Awards.

Baada ya ‘12 Years A Slave’ ambayo ilikuwa filamu yake ya kwanza ya Hollywood, ameshirikishwa katika filamu nyingine chini ya ‘Non- Stop’ ambayo mwigizaji, Liam Neeson, ameigiza akiwa ndiye staa. Sinema hiyo inatarajiwa kutoka Februari 28.

Makala hii ni mahojiano na mwigizaji huyo aliyetwaa tuzo ya New Hollywood, pia mbali ya Oscar anawinda tuzo zingine za Golden Globes na British Film Academy.

Lupita anaelezea jinsi alivyojikuta akiigiza filamu hiyo ya ‘12 years A Slave’ iliyoongozwa na Steve McQueen na kutayarishwa na mwigizaji maarufu Brand Pitt.

Mwanaspoti: Unazungumziaje maisha yako ya sasa nchini Marekani ukizingatia kwamba wewe ni nyota mwenye asili ya watu weusi na uko katika taifa ambalo ubaguzi wa rangi ukiwa bado ni tatizo?

Lupita: Nilipokuwa nakua sikuwahi kufikiria kuwa mimi ni mtu mweusi. Nilijiona kuwa mtu wa kawaida kabisa msichana kama yeyote yule wa jamii yangu ya Waluo. Nilikuwa mfupi kutoka familia ya kawaida na mwenye ngozi nyeusi. Lakini tangu nipate ufahamu Marekani nimekuta mambo ni tofauti kabisa, rangi ya mtu ni suala kubwa sana tofauti na nyumbani.

Ukiwa Marekani utajikuta ukitambua kwamba wewe si mtu sawa na wengine bali Mwafrika. Rangi ya mtu Marekani ni mtihani hasa kwetu sisi Waafrika. Ni lazima ujibidiishe zaidi ili kuishi kama watu wengine.

Mwanaspoti: Ulijitambuaje kuwa una uwezo wa kuigiza hadi ukajikuta kwenye upeo huu?

Lupita: Kulingana na mama yangu, nilianza uigizaji nikiwa na umri wa miaka mitatu. Anasema siku moja alikuja mgeni nyumbani na nikaanza kumburudisha kwa kuigiza kisa kutoka kwenye kitabu kimoja cha hadithi za kubuni. Mama yangu akamweleza yule mgeni ‘huyu mtoto siku moja atakuja kuwa mtumbuizaji au sijui ‘jambazi’.

Mwanaspoti: Je ulifanya kazi yoyote ya uigizaji baada ya kufuzu Shahada ya Kwanza ya Filamu na masomo ya Kiafrika kutoka taasisi ya Hampshire jijini Massachusetts na kisha kujiunga na Chuo cha Yale kwa Shahada ya Uzamili?

Lupita: Ndiyo, nilitayarisha simulizi ya maisha ya Albino na majanga wanayopitia kwa sababu wao ni tabaka la watu wanaounganisha jamii nzima. Hii ni kwa kuwa Albino wote duniani wana rangi moja na wanapatikana katika kila pande.

Mwanaspoti: Hivyo ndivyo ulivyoamua kujitosa mzima mzima katika uigizaji wa filamu kubwa baada ya masomo yako?

Lupita:  Siku moja nikiwa nyumbani, niliwaona watayarishaji wa filamu ya ‘The Constant Gardener’ wakitafuta eneo mwafaka kwa ajili ya kushuti sinema hiyo. Nilitamani sana kushirikishwa katika utengenezaji wake na kupitia rafiki yangu mmoja, nilipewa majukumu ya mtayarishaji msaidizi.

Hapo ndipo nilianza kutengeneza uhusiano mzuri na mwigizaji mkuu wa filamu hiyo Ralph Fiennes aliyeniuliza nilikusudia kufanya nini na maisha yangu.

Nilimjibu kwamba sikuwa na uhakika kwani hadi wakati huo dhamira yangu haikufahamu kabisa ikiwa kweli nilitaka kuwa mwigizaji.

Ndipo Fiennes alinieleza, ‘Lupita igiza ikiwa unahisi kwamba huwezi kuishi bila ya kufanya hivyo lakini ikiwa una jambo jingine la kufanya bora ufuate dhamira hiyo maana taaluma hii ni ngumu.’

Ujio huo ulinifanya kutafakari majuto ambayo ningekuwa nayo nitakapohitimu miaka 60, ikiwa sikutumia fursa hiyo na kujaribu.

Mwanaspoti: Hebu simulia ni vipi uliishia kupata nafasi ya kuigiza kama ‘Patsey’ kwenye ‘12 Years A Slave’ iliyoongozwa na mkali Steve McQueen?

Lupita: Nilipata habari za majaribio ya nafasi hiyo kutoka kwa meneja wangu, Didi Rea, ambaye pia anamwakilisha Garret Dillahunt aliye kwenye filamu hiyo vilevile akiigiza kama ‘Armsby.

Rea aliniletea maelezo ya mhusika Patsey wakati ambapo nilikuwa nakaribia kufuzu kutoka Yale na alihisi ningeigiza vizuri nafasi hiyo.  Hivyo alinirekodi jijini New York kwa jaribio la kwanza kisha nikafanya nyingine jijini Los Angeles na jaribio la tatu na la mwisho lilikuwa mjini Louisiana na Steve aliyependezwa nami.

Mwanaspoti: Ilikuwa vipi kumwigiza Patsey maana ni sinema ya kuliza sana, pia ni changamoto ipi ulikumbana nayo katika utaratibu wote wa utengenezaji wa filamu hiyo?

Lupita: Hakuna kipande chochote cha filamu hiyo ambacho kilikuwa rahisi kwangu, maana yalikuwa ni matokeo ya kweli ya mateso ambayo mwanamke huyo alipitia kwani mimi binafsi hayajawahi kunitokea. Ilikuwa ni hali halisi ya kile ambacho watumwa walipitia baada yangu na Solomon kuuzwa utumwani.

Nilipopokea simu kutoka kwa Steve kunipa sehemu hiyo, nilishikwa na mchecheto fulani sijui ikiwa ulichangiwa na furaha niliyokuwa nayo kwa kupata fursa ile au uzito wa ujumbe niliopaswa kuuwasilisha, ila nahisi yote mawili yalichangia, nilikuwa nawaza ni jinsi gani ningestahimili uchungu ule wote na wa kiwango kile.

Lakini nashukuru kwamba nilifanikiwa kuichora taswira kamili ya kile kilichomtokea mwanamke huyo aliyewahi kuishi na kupitia yeye nikatokea kuwa mwigizaji kuhadithia masaibu yake.

Punde tu baada ya kupewa majukumu hayo, nilianza utafiti wa kina kuhusu kilichotokea kwa usaidizi wa elimu yangu ya miaka mitatu kule Yale kwani bila hilo nisingefanikiwa.

Mbali na kufanya mazoezi makali, nilisoma kwa kina wasifu wake kitu ambacho kilinirutubisha na kunipevusha kumwigiza kikamilifu.

Hata hivyo, kilichonishangaza kwenye wasifu huo nilipousoma, ni pale mwanamke huyo alipohitajika kuvuna kilo 227 ya pamba kwa siku, uzani mkubwa zaidi ili kujihakikishia maisha yake. Ni hali niliyokumbana nayo katika kuigiza na haikuwa rahisi ila nashukuru.

Mwanaspoti: Unamzungumziaje mwongozaji wa filamu Steve McQueen aliyekupa fursa ya kuigiza sinema yako ya kwanza ya Hollywood?

Lupita: Ukweli ni kwamba Steve ni mwongozaji wa haiba kubwa. Ana uwezo wa kumsoma mwigizaji na kufahamu ni nafasi gani anayoweza kuiigiza vyema na siyo rahisi kwake kukupa nafasi hiyo bila ya wewe kudhihirisha una vigezo.

Kila anapompa mwigizaji nafasi, mtu huyo huwa ana sifa sawa na yule anayeigizwa ili kuuleta ujumbe unaokusudiwa kikamilifu.

Kingine ni kuwa anafahamu vyema kuelezea hadithi na ndipo anapokupangia kazi, yeye hukupa uhuru wa kujipatia nasaha kwa vyovyote kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo, hata ikiwa unakosea au kupata. Ni kigezo kizuri cha kujikuza maana mtu huishia kugundua mengi katika hali hiyo.