Miaka 93 sio ishu bado anatamba na urembo
Muktasari:
- Siku zote fahari ya mwanamke ni muonekano, urembo, afya njema na kujitegemea kiuchumi ili asiwe mzigo katika jamii, inawezekana akawa na mwenza ama pekee yake, kikubwa ajiamini kufanya vitu anavyoona vitamtambulisha kwa upekee.
UMRI mkubwa hauwezi kuwa kikwazo, kuishi maisha ya ndoto zako, endapo tu ukizingatia baadhi ya vitu na kuvifanya kwa mwendelezo sahihi.
Siku zote fahari ya mwanamke ni muonekano, urembo, afya njema na kujitegemea kiuchumi ili asiwe mzigo katika jamii, inawezekana akawa na mwenza ama pekee yake, kikubwa ajiamini kufanya vitu anavyoona vitamtambulisha kwa upekee.
Ipo mifano ya wanawake wengi licha ya umri wao kuwa mkubwa, wameendelea kuonekana warembo na wenye mvuto kimuonekano na afya njema.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya vitu vitakavyomfanya mwanamke hata katika umri wake mkubwa akaendelea na urembo na muonekano mzuri anaoutaka. Kati ya vitu vinavyoshauriwa na watalamu wa afya pamoja na shuhuda za watu ambao wamefanikiwa katika hilo, lishe bora (nutrition) ni jambo muhimu la msingi kwa mwanamke, siyo kila chakula anaweza kula kama anataka azeeke na urembo na muonekano mzuri wenye mvuto.
Wikipedia imekusanya taarifa za watu mashuhuri duniani ambao wanatoa ushuhuda wa vyakula vinavyotakiwa ni vya protini (kujenga ngozi na misuli), vitamini A, C, E (kupambana na kuzeeka kwa ngozi) na omega-3 (kulinda ngozi isikauke).
Jambo lingine ni kunywa maji ya kutosha (angalau lita 1.5–2 kwa siku), kufanya mazoezi ya mara kwa mara yanayosaidia ngozi ing’ae, kupunguza uzee, kudumisha umbo, mfano ya mazoezi yanayoruhusiwa ni kutembea, yoga, Mazoezi ya nguvu (light strength training).
Mfano mzuri ni Jane Fonda mwanaharakati mwenye nguvu anayepambana licha ya kuwa na umri mkubwa alizaliwa Jane Seymour Fonda, New York City, Marekani, Desemba 21, 1937, anaamini katika lishe nzuri, mazoezi, analala muda wa kutosha kuuruhusu mwili kujitengeneza upya, mtazamo chanya wa vitu vyenye kuleta mabadiliko katika jamii, bado ni mkakamavu na uwezo mkubwa wa kuchambua mambo.
Bibi huyo anaamini asipolala usingizi wa kutosha inachangia ngozi kuchoka, mikunjo, anazingatia kutunza ngozi, anatumia moisturizer, sunscreen (kinga ya jua ) kila siku, hivyo ni baadhi ya vitu muhimu anavyovizingatia na kuwasisitiza wanawake wengine kufanya hivyo.
Mfano mwingine ni wa mwanamitindo wa zamani Christie Brinkley, anasisitiza lishe ya mimea (plant-based diet) kama siri ya ngozi yake kung’aa hata akiwa na 71.
Christie Brinkley si tu mwanamitindo wa zamani ni mfano wa mtindo wa maisha (lifestyle icon) anayewakilisha urembo, afya, na kuzeeka kwa heshima (graceful aging). Vitu vingine anavyotumia ni kahawa ya uyoga (mushroom coffee), kufanya mazoezi kama kucheza muziki (dancing), na mazoezi ya kifaa cha total gym.
Pia anafanya matibabu ya urembo yasiyo ya upasuaji kama Ultherapy, mbali na hilo anahamasisha utunzaji wa mazingira (environmentalism) na kudumisha mtazamo chanya wa “kujituma na kuchukua hatua” (go-getter attitude).
Kitu kingine kinachoweza kumpa mwanamke muonekano mzuri ni afya ya akili (mentalhealth), kwani ‘stress’ zinaathiri moja kwa moja urembo, husababisha chunusi, huchochea kuzeeka mapema, vitu vinavyoshauriwa kufanyika ni kupumzika kwa muda mrefu, kuwa na furaha.
Vitu vingine vinavyoelezwa na watalamu wa eneo hilo ni kujiamini kwani urembo hauishii kwenye ngozi pekee, mavazi yanayofaa na kuendana na mwili pamoja na kuzitunza nywele ziwe fupi ama ndefu.
Mwingine ni Carmen Dell’Orefice ni mfano wa mvuto na akiwa na umri wa miaka 93 ndiye ‘supermodel’ mzee zaidi aliye hai na anayefanya kazi duniani kote. Muonekano wake na nywele zake za rangi ya fedha zilizopambwa kwa umbo lake la kipekee ni mvuto tosha kwa mtu anayemtazama.
Dell’Orefice alianza kazi ya urembo 1946, na kupata jalada la kwanza la gazeti la Vogue akiwa na umri wa miaka 15, alikuwa supermodel maarufu katika miaka ya 1950, na kujiunga na Ford Models 1953 wakati huo urembo haukuwa kazi yenye faida kubwa, hivyo alilazimika kufanya kazi kama mshonaji ili kusaidia familia yake. Mbali na kuwa na watoto wawili, anawajukuu na vilembwe watatu (watoto wa wajukuu zake).
Mwaka 2017, akiwa na walinzi wawili, alifunga maonyesho ya haute couture ya Guo Pei g msimu wa Spring 2017 na mwaka 2019, alitembea kwenye ukumbi wa mitindo kuunga mkono mfuko wa msaada wa Fashion for Relief, pia aliandika kitabu cha kumbukumbu na ushauri wa urembo kilichopewa jina la Staying Beautiful, Beauty Secrets and Attitudes from My Forty Years as a Model.
Anawasisitiza wanawake kutokujibweteka haijalishi wanafamilia kwa maana ya watoto, kikubwa waishi katika ndoto zenye kuacha alama imara za kukumbukwa, huku akishauri baadhi ya vitu ambavyo hawapaswi kuvifanya kama sigara, pombe kupita kiasi na sukari nyingi.