Monalisa: Filamu za kushirikishwa hazilipi

Yvonne Cherry ‘Monalisa.
Muktasari:
- Alianza kutamba na Kundi la Mambo Hayo mwishoni mwa miaka ya 1990, baadaye alijiingiza kwenye uigizaji filamu akianzia filamu ya Girl Friend iliyotamba mwaka 2002 ikiwa ya kwanza nchini yenye mchanganyiko wa wasanii wa muziki na uigizaji.
UNAPOWAZUNGUMZIA waigizaji mahiri wa kike nchini hautaacha kuwataja wasanii kama Yvonne Cherry ‘Monalisa’, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Wema Sepetu, Anti Ezekiel, Rihama Ally ‘Riyama’, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na wengine wengi.
Hata hivyo kwa ukongwe, Monalisa ni miongoni mwao, ametamba na filamu kadhaa nchini na hata nje ya nchi ambapo amekuwa akishirikishwa.
Alianza kutamba na Kundi la Mambo Hayo mwishoni mwa miaka ya 1990, baadaye alijiingiza kwenye uigizaji filamu akianzia filamu ya Girl Friend iliyotamba mwaka 2002 ikiwa ya kwanza nchini yenye mchanganyiko wa wasanii wa muziki na uigizaji. Katika filamu hiyo walishiriki kina TID aliyeigiza kama mpenzi wa Monalisa, King Crazy GK, Jay Moe na wengine wengi.
Monalisa, mama wa watoto wawili Sonia na Abdulwahid ana filamu tatu lakini Binti Nusa aliyomshirikisha mama yake mzazi, Suzan Lewis ‘Natasha’ na Hashim Kambi ndiyo iliyofanya vizuri zaidi.
Monalisa alisema mambo muhimu kuhusu uigizaji filamu: “Unatakiwa ujue unachotaka kufanya na kwa wakati gani ili kazi yako iwe bora na ikubalike, utulivu na ubunifu ni vitu vitakavyoifanya kazi ionekane bora.
Monalisa pia ameulalamikia usambazaji wa kazi zao kuwa haukidhi mahitaji yao kwani kiasi wanachotumia kutengenezea kazi hakiendani na fedha wanayopata baada ya mauzo.
“Wasambazaji wachache, wasanii wengi, hivyo ni vigumu kuchukua kazi zetu kwa wakati mmoja, wanachofanya ni kupokea kazi za wasanii wenye mikataba nao na wengine kuendelea kusubiri. Kazi pia zinaibiwa sana sababu ya usimamizi mbovu, COSOTA ni chama kinachosimamia kazi zetu, kimezidiwa ujanja na maharamia ndiyo maana wizi unaendelea, waongeze adhabu kwa wezi,’’ anasema.
Faida
Anasema msanii hupata faida kulingana na ubora wa kazi yake na anapotengeneza filamu nyingi kwa mwaka ndipo anapofaidika zaidi.
“Hii ni kutokana na soko lilivyo, usimamizi ungekuwa mzuri hata wenye filamu mbili kwa mwaka wangefaidika. Mimi nina filamu tatu zangu mwenyewe lakini nilizoshirikishwa ni nyingi, filamu zangu zimenipa faida kutokana na ubora ingawa faida si kubwa sana, filamu ya Binti Nusa imefanya vizuri,” anafafanua
Kuhusu kufanya kazi na mama yake mzazi, anasema: “Najisikia faraja kuigiza lakini ninapokuwa kwenye uigizaji simchukulii kama mama bali msanii mwenzangu, hii ni kazi kama nyingine, tukiweka mambo ya kifamilia hatuwezi kufanya kwa ufasaha.
Girl Friend
“Ni filamu ambayo siwezi kuisahau maishani, ni ya kwanza kuigiza, sikutarajia kama ingefanya vizuri na kukubalika kiasi kile, tulikuwa tunajaribu soko, tulifanikiwa kwa na wengine walifuata.
“Ni mwanzo mzuri kwangu na katika tasnia nzima, sasa kila mtu anatengeneza filamu na anatoka, nashukuru mawazo niliyatoa katika Girl Friend yalikubalika.”
Siri ya Mtungi
Monalisa ni miongoni mwa wasanii wanaogiza tamthiliya ya Siri ya Mtungi ambayo anadai imemkomaza zaidi.
“Siri ya Mtungi imetengenezwa katika ubora wa juu na inaonekana karibu duniani kote, najisikia faraja kuwemo kwenye filamu hiyo ya tofauti na haiwezi kufikiwa kwa ubora hapa nchini.
Mwaka huu Siri ya Mtungi inayotayarishwa na MFDI Tanzania kwa kushirikiana na JHUCCP Tanzania ni kati ya tamthiliya zilizoingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya African Magic Viewer’s Choice (AMVCA) tuzo zilizofanyika Lagos, Nigeria ingawa haikuambulia kitu.
“Hatukushinda tuzo yoyote kati ya vipengere vilivyopendekezwa lakini nimejifunza mengi kupitia Siri ya Mtungi, hiyo ni hatua katika maisha yangu ya sanaa ya uigizaji,” anasema.
Maisha nje ya sanaa
Monalisa hupendelea kushinda nyumbani, hubadilishana mawazo na rafiki zake, kuangalia filamu na kutoka ‘outing’ anapojisikia wakati huo huo akifanya mambo ambayo hayawezi kuwaumiza watoto wake kimaadili.
Kuhusu mipango ya baadaye amepanga ‘kuwashika’ mashabiki wa filamu: “Napanga kufanya makubwa ambayo watu hawataamini ila kila mtu atakubali, siwezi kuweka wazi sasa kwani kuna ambao hawapendi kuona mtu anafanya jambo zuri.
“Kingine ni kwenda mikoani kuibua vipaji kwa wasanii, nitakwenda na kampuni ya Prone Promotion hiyo ipo wazi.
Filamu alizohusika kwa namna moja ama nyingine ni Black Sunday iliyompatia tuzo ya ZIFF ya msanii bora mwaka 2010, Binti Nusa 2 & 3 iliyompatia tuzo ya mwigizaji bora wa Tanzania (Central Award Best Actress in Tanzania 2011). Nyingine ni Payback, Nimeokoka, Cellular, Wrong Number, Wedding Pressure, Behind the Scene, Who is Smarter, She is My Sister aliyoigiza na mmoja wa mastaa wa Niger, Mercy Johnson chini ya mwongozaji Femi Ogedegde wa Nollywood, Dilema, Sabrina, Girlfriend, Tell Me the Truth.
Monalisa pia ni mtaalamu wa michezo ya jukwaani, ameigiza A Man of the People, Don’t Dress for Dinner, Song of Lawino, Zawadi ya Ushindi na The Government Inspector..
“Ninaposhiriki filamu ya mtu nalipwa lakini malipo ni makubaliano ya watu wawili, mwenye filamu na mimi, siwezi kuweka wazi kwani kila filamu na bei yake, kikubwa ninachoweza kusema ni kuwa wale wote wanaotangaza kuwa wanalipwa fedha nyingi wanaposhirikishwa ni waongo,” anasema Monalisa.