Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri ya kupendeza kwa wanawake wanene, wembamba ipo hapa

Muktasari:

  • Wengine wanavaa magauni makubwa kama wanakwenda kufunika godoro, wakati ukweli ni kila mwili una staili yake na ukijijua tu unakaa bomba bila 'stress'.

WANAWAKE bwana, wana mambo yao mengi sana hasa kwenye suala la mavazi. Utakuta mwingine anavaa nguo ya kubana hadi unajiuliza anapumua kweli au anateseka kimyakimya.

Wengine wanavaa magauni makubwa kama wanakwenda kufunika godoro, wakati ukweli ni kila mwili una staili yake na ukijijua tu unakaa bomba bila 'stress'.

Siku hizi wanawake wengi wanahangaika kufuata mitindo (fashion) ya Instagram na TikTok bila kujiuliza kwanza, “Hii nguo inanifaa kweli?” Unaweza kuona nguo imempendeza mtu mwingine, lakini kwako ikageuka majanga.

Fashion siyo kushindana, ni kujitambua. Mwanamke mnene anaweza kupendeza kuliko mwembamba akijua kuvaa na mwembamba anaweza kuwaka kuliko wote akijipanga vizuri.

KWA WANAWAKE WANENE

Kwanza waachane na tabia ya kuvaa nguo zinazowabana kupita kiasi wakidhani ndiyo zinaonyesha maumbo vizuri. Hapana dada yangu, ukivaa nguo ya kubana mno unajiongezea usumbufu na wakati mwingine unafanya mwili ukae vibaya zaidi.

Nguo zinazokaa vizuri mwilini bila kubana sana ndiyo zinafaa. Magauni yenye kuachia kidogo, vitenge vya kisasa, pamoja na nguo zenye mistari ya wima huwafanya waonekane smati na wenye mvuto mkubwa.

Pia wanawake wanene wanapaswa kuwa makini na rangi. Siyo kila rangi lazima ikufae. Rangi zilizotulia kama nyeusi, bluu iliyokolea 'dark blue', kijani iliyokolea 'dark green' au kahawia 'brown' mara nyingi zinawafanya waonekane nadhifu zaidi.


ACHENI HIZO

Halafu kuna hii tabia ya kuvaa maua makubwa makubwa kwenye nguo, mwingine anakuwa kama sofa ya sebuleni au mapazia. Maua madogo na mitindo za kawaida zinafaa zaidi kuliko michoro mikubwa inayoongeza mwonekano wa mwili.

ZINGATTIA SAIZI

Kitu kingine muhimu ni kuchagua size sahihi. Wanawake wengi wanakosea hapa. Mwingine ananunua size ndogo kwa lazima eti apunguze mwili kwa macho. Mwishowe anatembea huku nguo zinampiga vita kila hatua. Hakuna ubaya kuvaa size yako halisi. Uzuri wa mwanamke haupimwi kwa kubana mwili bali kwa namna alivyojiweka.


VIMODO

Kwa upande wa wanawake wembamba, nao wana changamoto zao. Wengi huvaa nguo zinazowafanya waonekane kama fito zilizotembea. Mwanamke mwembamba anatakiwa kuvaa nguo zinazoongeza umbo kidogo na kuleta balansi. Magauni yenye mikunjo, pamoja na tops zenye puff kidogo huwafanya waonekane wenye mvuto zaidi.

Wanawake wembamba pia wanaruhusiwa kucheza na rangi kali na michoro mikubwa. Hapa ndipo unaweza kuvaa maua makubwa au rangi zinazong’aa bila shida. Tofauti na wanawake wanene ambao wanahitaji kupunguza mwonekano wa mwili, mwembamba yeye anahitaji kuongeza uhai kwenye mwonekano wake.

JIAMINI MWANAMKE

Lakini jambo kubwa kuliko yote ni kujiamini. Unaweza kuvaa nguo ya bei mbaya kiasi gani, lakini kama hujiamini bado utaonekana kawaida tu. Mwanamke anayejitambua na kuvaa kile kinachomfaa huwa anavutia hata akiwa kwenye nguo rahisi kabisa.

Mitindo sio mateso wala mashindano ya nani kabanwa zaidi. Ni sanaa ya kuufanya mwili wako ukae vizuri na ujisikie huru. Mwanamke mnene akivaa kinachomfaa anapendeza na mwembamba akijijua naye anawaka. Kikubwa ni kuacha kuiga kila trend inayopita mtandaoni na kuanza kuvaa kile kinachoendana na mwili wako.

Mwishowe, uzuri wa mwanamke hauanzi kwenye nguo bali namna anavyojibeba. Nguo ni nyongeza tu ya kuonyesha ule uzuri ambao tayari anao.