Studio za Barnaba Classic zateketea kwa moto, shughuli zasimama
Muktasari:
- Tukio hilo limetokea Mwananyamala, Dar es Salaam, jana saa 2:30 usiku, muda mfupi baada ya Barnaba kurejea Dar es Salaam akitokea Arusha.
Tasnia ya muziki nchini imeamka na taarifa za kusikitisha baada ya studio za uzalishaji wa muziki na filamu za HighTable Sound Entertainment zinazomilikiwa na msanii wa Bongo Fleva, Barnaba Classic, kuteketea kwa moto jana usiku.
Tukio hilo limetokea Mwananyamala, Dar es Salaam, jana saa 2:30 usiku, muda mfupi baada ya Barnaba kurejea Dar es Salaam akitokea Arusha.
Kwa mujibu wa msanii huyo, baada ya kuwasili Dar es Salaam alifika studio kusalimia kabla ya kuelekea nyumbani.
Hata hivyo, dakika chache baadaye alipokea simu ya dharura iliyomjulisha kuwa moto mkubwa ulikuwa umezuka katika studio hizo.
“Moyo unaniuma, nimelia sana kwa uchungu, nimekosa nguvu kabisa. Nasikitika kusema makao makuu yetu yamekuwa majivu,” amesema Barnaba.
Pigo hilo linaelezwa kuwa kubwa zaidi kwa kuwa ni wiki mbili zimepita tangu kufanyika ukarabati mkubwa wa studio hizo kwa gharama kubwa, ikiwa ni sehemu muhimu ya shughuli za muziki na ajira kwa vijana wengi waliokuwa wakifanya kazi chini ya HighTable Sound Entertainment.
Licha ya maumivu ya tukio hilo, Barnaba amemshukuru Mungu pamoja na vikosi vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi na majirani waliojitokeza kusaidia kudhibiti moto huo.
Msanii huyo pia amesisitiza kuwa huu si wakati wa kutafuta wa kulaumiwa, bali ni kipindi cha kukabiliana na changamoto na kuanza upya.
Kutokana na janga hilo, Barnaba ametangaza kusitisha shughuli zake zote muhimu zilizokuwa zimepangwa kufanyika leo ikiwemo mkutano wake na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam, huku uzinduzi wa filamu yake mpya ‘ Kikulacho’ na wimbo wake wa 'Siri Yangu' yakisitishwa hadi hapo itakapotangazwa tena.
Wadau wa muziki na mashabiki mbalimbali wameendelea kutuma salamu za pole na kumtia moyo msanii huyo, wakimtakia nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu baada ya kupoteza sehemu muhimu ya kazi na uwekezaji wake.