Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KISHKAJI: Harmonize hajawaelewa wanaosema ‘hajui kizungu’

Muktasari:

  • Ingawa natambua ujumbe ule ulikuwa ni kwa wote wenye chokochoko kuhusu ‘yai’ la Harmonize, mimi nilikuwa natabasamu wakati nasoma kwani nilikuwa nahisi kama Harmonize ameniandikia ule ujumbe kwa sababu nimewahi kuzungumza jambo kuhusu Kiingereza cha Harmonize.

JUZI kati Harmonize kawaandikia mahaters wake bonge la barua kuhusu tabia ya kumwambia hajui Kiingereza. Kwenye barua hiyo Konde Boy ameng’aka maneno yanayofanana na ‘mtasema sana, mtaongea sana, lakini nitaendelea kuandika na kuimba Kiingereza.’ Tena kwa mikwara zaidi hata ujumbe huo aliutuma kwa Kiingereza - tena chenye makosa kibao ya kiuandishi.

Ingawa natambua ujumbe ule ulikuwa ni kwa wote wenye chokochoko kuhusu ‘yai’ la Harmonize, mimi nilikuwa natabasamu wakati nasoma kwani nilikuwa nahisi kama Harmonize ameniandikia ule ujumbe kwa sababu nimewahi kuzungumza jambo kuhusu Kiingereza cha Harmonize.

Lakini wakati nasoma nimegundua kitu, Harmonize hajaelewa watu wengi wanaokosoa Kiingereza chake wanamaanisha nini. Harmonize anachukia kwa sababu anadhani watu wanamwambia hajui Kiingereza lakini si kweli, watu wengi hawamwambii kwamba hajui. Na wala watu wengi hawategemei Harmonize ajue Kiingereza.

Kwanza, Harmo ni Mtanzania ambapo Watanzania lugha yetu ni Kiswahili, ila Kiingereza ni lugha ya kujifunza darasani - tena tunakutana nayo sekondari huko tukiwa matineja kabisa. Pili, Harmonize amezaliwa na kukulia Mtwara sehemu ambayo hata kuzungumza Kiswahili tu ni changamoto kwa baadhi ya wana Mtwara au wakikizungumza basi kina lafudhi nzito ya Kusini na mchanganyiko wa maneno ya lugha za makabila.

Tatu, Harmonize amekulia kwenye familia ya hali ya chini kama Watanzania wengi, na wengi tuliokulia kwenye familia hizo tunafahamu kwamba Kiingereza ni kitu kigeni sana. Wazazi wetu hawakubahatika kwenda shule kwa hiyo hawakijui, hatuna wajomba wala mashangazi wanaoikuja, hatuna TV useme tutajifunza kupitia kutazama muvi kama ambavyo watoto wa siku hizi wananyaka YES - NO mbili tatu kupitia katuni wanazotazama. Kwa kifupi, sababu ni nyingi sana zinampa Harmonize mwanya wa kujitetea kuhusu Kiingereza chake. Lakini tunarudi palepale, Harmonize hajawaelewa watu wanaokosoa Kiingereza chake wanamaanisha nini. Watu hawamwambii kwamba hajui au lazima ajue Kiingereza ila watu wanamwambia kwamba Harmonize sio yule Rajab wa Chitohori. Sasa hivi Harmonize amekuwa taasisi. Kila kitu chake kinatakiwa kuwasilishwa kwa ufasaha kama sio usahihi.

Ni aibu kubwa kuona taasisi inaandika ujumbe au taarifa kwa umma kwa uandishi wenye makosa na hii bila kujali katumia lugha gani iwe Kiingereza au Kiswahili. Inatia wasiwasi na kufanya watu wajiulize, ‘hii taasisi ina usimamizi kweli!?  Vuta picha leo hii unasoma taarifa ya Simba au Yanga yenye makosa kibao ya kiuandishi - kwenye L imewekwa R, kwenye kuweka mkato kuna nukta, kwenye kuweka herufi kubwa kuna ndogo utakuwa na maoni gani kuhusu taasisi hizo? Si taasisi inaonekana kanjanja?

Kwa hiyo watu wengi hawaongelei Kiingereza cha Konde Boy wanachosema ni ‘taasisi Harmonize’ inabidi ihariri taarifa zake kabla hazijatumwa kwa umma. Hakuna anayelazimisha Harmo azungumze Kiingereza utadhani anatoka ukoo wa Malkia wa Uingereza. Sote ni Watanzania na tunajuana Kiingereza kwetu ni kipengele na hata majirani zetu Kenya kila siku wanatutania kuhusu Kiingereza chetu.

Harmo aache kujitetea atafute wahariri wa kupitia maandishi yake kabla hayajaja kwa jamii - iwe ya Kiingereza au Kiswahili au hata Kimakonde. Kuandika vitu vyenye makosa ya kiuandishi ni kuiaibisha taasisi. Ni ushauri tu!