Tupogo wa Ommy Dimpoz watamba klabuni Chelsea

Ommy Dimpoz.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
- Kwa sasa chipukizi hao wa Chelsea wanashindana kucheza wimbo huo kwa staili za msanii huyo wa nchini wanazofundishwa na Nditi.
BEKI wa kushoto wa timu ya vijana ya Chelsea, Mtanzania Adam Nditi, amekuwa akitangaza nyimbo za Kitanzania kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya Stamford Bridge na amekuwa akiwafundisha wenzake jinsi ya kucheza wimbo ‘Tupogo’ wa msanii Ommy Dimpoz.
Kwa sasa chipukizi hao wa Chelsea wanashindana kucheza wimbo huo kwa staili za msanii huyo wa nchini wanazofundishwa na Nditi.
Mwanaspoti kupitia mitandao ya kijamii ya ‘You Tube’ na ‘Facebook’ imewashuhudia wachezaji wa timu hiyo; Alex Davey na John Swift, wakichuana kucheza ‘Tupogo’ .
Davey ambaye ni beki wa kati, alionekana kinara wa kucheza wakati Swift (kiungo) akiwa anamtazama na kucheka huku Nditi akiwa pembeni akiwashuhudia.
Beki huyo alikuwa akicheza kama anavyocheza Dimpoz, lakini akiwa amevalia jezi za Chelsea.
Nditi alizaliwa Septemba 18, 1994 visiwani Zanzibar na alijiunga timu ya watoto wa umri chini ya miaka 13 ya Chelsea akiwa beki wa kushoto na mara nyingine akicheza nafasi ya winga wa kushoto.
Kuanzia msimu wa 2011/12 wa Ligi Kuu ya Vijana wa umri chini ya miaka 21 ya England, Nditi amekuwa akicheza na anafananishwa makali na Ashley Cole ambaye ni beki wa kikosi cha kwanza cha Chelsea.
Naye Ommy Dimpoz ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Instagram akisema: “ Hivyo ndivyo wachezaji wa Chelsea wanavyocheza wimbo ‘Tupogo’ kabla ya mazoezi, nashukuru sana mdogo wangu Adam Nditi.”