Zaiylissa achomoa kwa Dulla Makabila
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Zaiylissa amesema kwa sasa hataki kuzungumzia chochote kinachohusu ujumbe huo ambao umeendelea kusambazwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram na Facebook.
MUIGIZAJI wa tamthilia nchini, Zaiylissa, amesema hana la kujibu kuhusu ujumbe mzito uliowekwa mtandaoni na aliyekuwa mume wake, Dulla Makabila.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zaiylissa amesema kwa sasa hataki kuzungumzia chochote kinachohusu ujumbe huo ambao umeendelea kusambazwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram na Facebook.
“Kwa kweli sina la kujibu kuhusu hilo,” amesema Zaiylissa kwa kifupi baada ya kuulizwa kuhusu maneno ya Dulla Makabila aliyekiri kushindwa kumtoa moyoni mpaka sasa.
Katika ujumbe huo, Dulla Makabila ameandika kwa hisia kali akieleza kuwa licha ya kupita miaka mingi tangu waachane, bado hajafanikiwa kusahau mapenzi yao na kwamba kila akijaribu kuendelea na maisha, anajikuta akimkumbuka tena Zaiylissa.
“Najua kuna watakaosema nataka kutrend au kutoa wimbo mpya, lakini ukweli ni kwamba bado sijafanikiwa kumove on,” ameandika Dulla Makabila kwenye sehemu ya ujumbe wake uliosambaa kwa kasi mtandaoni Mei 22, 2026.
Msanii huyo ameenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hata anapokuwa kwenye mahusiano mengine bado anahisi hakuna mwanamke aliyewahi kuziba nafasi ya Zaiylissa, jambo lililoibua hisia tofauti kwa mashabiki wake.
Baadhi ya watu mitandaoni wameonesha kuguswa na ujumbe huo wakisema Dulla ameandika kutoka moyoni, huku wengine wakimtaka kuachana na yaliyopita na kuheshimu maisha mapya ya Zaiylissa ambaye kwa sasa ameolewa.
Dulla Makabila na Zaiylissa waliwahi kufunga ndoa Mei 2023 iliyodumu kwa takribani mwezi mmoja, kisha wawili hao wakaachana.
Januari 24, 2024, Zaiylissa na Manara wakafunga ndoa iliyodumu kwa miezi 14 ambapo kwa mujibu wa waliyoyawekea wenyewe mitandaoni ilifikia tamati Aprili 9, 2025
Kwa sasa Zaiylissa yupo kwenye ndoa na Said ambapo mitandaoni amekuwa akijitambulisha Mrs SAID. Ndoa hiyo ilifungwa Februari 2026.