Bab’kubwa… Dili Hizi zimelipa Ligi Kuu!

Muktasari:
- Watetezi Yanga wapo kileleni wakikusanya pointi 58, nyuma ya watani wao wa jadi Simba mwenye 57, baada ya zote kucheza michezo 22, huku matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC waliocheza mechi 23, wakishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 48.
LIGI Kuu Bara imesimama baada ya Ijumaa kupigwa mechi ya kiporo kati ya Simba na Dodoma Jiji, ili kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa zinazochuana kusaka tiketi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026.
Watetezi Yanga wapo kileleni wakikusanya pointi 58, nyuma ya watani wao wa jadi Simba mwenye 57, baada ya zote kucheza michezo 22, huku matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC waliocheza mechi 23, wakishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 48.
Singida Black Stars iliyocheza pia michezo 23, ni ya nne kwa pointi 44, KenGold inaburuza mkiani ikiwa na pointi 16, ikifuatiwa na Tanzania Prisons iliyo ya 15 na pointi 18, wakati Kagera Sugar iko ya 14 na pointi 19, zikipambana kutoshuka daraja.
Wakati Ligi Kuu ikienda mapumziko hadi Aprili Mosi, wapo baadhi ya mastaa waliojiunga na timu mbalimbali katika dirisha dogo la Januari mwaka huu na kuonyesha kiwango bora cha kuwavutia mashabiki kama Mwanaspoti linavyowaelezea, tiririka!

JONATHAN SOWAH (SINGIDA BS)
Huenda huu ndio usajili bora wa Januari kwa timu zote 16, zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, baada ya mshambuliaji huyu raia wa Ghana kuonyesha kiwango bora akiwa na Singida Black Stars, hali inayomfanya kuchochea zaidi vita ya ufungaji bora.
Sowah aliyejiunga na Singida Black Stars akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, amekuwa na kiwango bora na timu hiyo ambapo hadi sasa amefunga mabao saba katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara, akiwa na wastani wa kufunga bao moja kwa kila mechi.
Nyota huyo raia wa Ghana, ameendeleza kiwango bora kwani hata alipokuwa na Al-Nasr Benghazi FC aliyoichezea kwa miezi sita, alihusika na mabao saba na kikosi hicho, baada ya kufunga matano na kuasisti mawili kwenye mechi tisa.
Sowah alijiunga na Al-Nasr Benghazi Januari 27, 2024, akitokea Medeama ya kwao Ghana ambako pia alionyesha kiwango bora na kuzivutia klabu mbalimbali, ikiwamo Yanga baada ya kuwasumbua kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi.
Akiwa na Medeama aliyojiunga nayo Januari 11, 2023, akitokea Danbort FC, alicheza michezo 20 ya Ligi Kuu ya Ghana akifunga mabao 16, huku katika Ligi ya Mabingwa Afrika alifunga matatu kwenye mechi zake saba alizochezea kikosi hicho.
Katika michuano ya FA ya Ghana alifunga mabao matatu katika michezo saba na Medeama na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, huku akijumuishwa katika kikosi cha mwisho cha Ghana kwenye fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2023, zilizofanyika Ivory Coast.

SELEMANI BWENZI (KENGOLD)
Licha ya KenGold kuburuza mkiani mwa msimamo kwa pointi 16, baada ya mechi 23, mojawapo ya nyota anayefanya vizuri ni Seleman Bwenzi, kutokana na kiwango kizuri anachoendelea kukionyesha tangu ajiunge na miamba hiyo ya Mbeya.
Nyota yake ilianza kung’aa wakati alipomfunga kipa wa Yanga, Djigui Diarra bao la shuti la mbali kutokea katikati ya uwanja katika ushindi wa kikosi hicho cha Jangwani wa mabao 6-1, Februari 5, mwaka huu.
Hadi sasa amechangia mabao sita ya Ligi Kuu Bara katika kikosi hicho, baada ya kufunga matano na kuasisti moja ambapo kabla ya hapo alikuwa Mbeya Kwanza inayoshiriki Championship aliyoifungia pia bao moja na kuasisti mengine mawili.

MATHEW MOMANYI TEGISI (PAMBA JIJI)
Unapotaja miongoni mwa washambuliaji walioleta mageuzi makubwa katika kikosi cha Pamba Jiji, hutoacha kulitaja jina la Mkenya Mathew Momanyi Tegisi, kutokana na kiwango kizuri anachoendelea kukionyesha hadi sasa katika michezo ya Ligi Kuu.
Momanyi aliyetokea Shabana FC ya kwao Kenya, tangu ajiunge na timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya miaka 23, tangu iliposhuka rasmi daraja mwaka 2001, amehusika kwenye mabao sita, akifunga manne na kuasisti mawili.
Mshambuliaji huyo ni kama ameendeleza pale alipoishia wakati akiwa na Shabana FC, kwani kabla ya kujiunga na Pamba alikuwa amefunga mabao matano kwao Kenya, nyuma ya nyota mwenzake, Brian Michira aliyekuwa anaongoza wakati huo na saba.

ELIE MPANZU (SIMBA)
Elie Mpanzu Kibisawala ni winga aliyeanza maisha yake ndani ya kikosi cha Msimbazi taratibu huku baadhi ya mashabiki wakiwa hawamuelewi, japo msemo wa subira huvuta heri kama wasemavyo walimwengu ndicho kinachoonekana sasa.
Nyota huyo alijiunga na Simba tangu Oktoba mwaka jana akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo, japo hakuweza kuitumikia timu hiyo kwa wakati huo, kutokana na dirisha la usajili lilikuwa tayari limefungwa na kusubiria hadi Januari mwaka huu.
Akiwa na Simba, ameifungia mabao matatu ya Ligi Kuu Bara na kuasisti mengine manne, huku akiwa ni mwiba mkali kwa safu ya ulizi ya wapinzani, kutokana na kasi yake uwanjani akitokea pembeni au nyuma ya mshambuliaji.

ZIDANE SERERI (AZAM FC)
Licha ya ushindani wa nafasi katika eneo la ushambuliaji katika kikosi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam, ila kiungo mshambuliaji, Zidane Sereri ameongeza chachu kwa nyota wenzake kikosini kutokana na kiwango anachokionyesha.
Nyota huyo aliyejiunga na Azam, Januari mwaka huu akitokea Dodoma Jiji, hadi sasa amefunga mabao mawili na timu hiyo ingawa kiujumla ametupia kambani matano, kwani kabla ya hapo alikuwa ameshakifungia kikosi cha ‘Walima Zabibu’ matatu.
Zidane aliongeza umaarufu zaidi wa jina lake baada ya kutokea benchini katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba na kufunga bao la kusawazisha katika dk88 hivyo, kuifanya mechi hiyo iliyopigwa Februari 24, mwaka huu kuisha sare ya 2-2.

AMAS OBASOGIE (SINGIDA BS)
Kipa huyu raia wa Nigeria, tangu ajiunge na kikosi hicho cha Singida Black Stars, ameonyesha kiwango kikubwa na kupindua upya ufalme wa Metacha Mnata aliyekuwa ni panga pangua kikosini humo, tangu msimu huu umeanza.
Obasogie aliyejiunga na Singida akitokea Fasil Kenema ya Ethiopia, amekuwa panga pangua kwa sasa ndani ya kikosi hicho, ambapo amejikusanyia ‘clean sheets’ tatu za Ligi Kuu Bara, nyuma ya mwenzake, Metacha Mnata anayeongoza akiwa na saba.
Wengi walitarajia kumuona Metacha akiendeleza ufalme wake langoni baada ya awali kumshinda kipa, Mohamed Nbalie Kamara aliyemsugulisha benchi tangu ajiunge nao akitokea Horoya AC ya Guinea, hadi kupelekwa kwa mkopo Pamba Jiji dirisha dogo.

ABDOULAYE CAMARA (PAMBA JIJI)
Mshambuliaji huyo raia wa Guinea, unaweza kusema taratibu anaanza kujipata akiwa na kikosi hicho cha Pamba Jiji ambacho anakitumikia kwa mkopo, baada ya kushindwa kuwika akiwa na Singida Black Stars aliyojiunga nayo Agosti 14, mwaka jana.
Tangu ajiunge na Pamba, Abdoulaye Camara amekuwa katika kiwango bora hadi sasa ambapo amechangia mabao mawili ya Ligi Kuu Bara msimu huu, akifunga moja wakiilaza Coastal Union 2-0 Februari 15.
Alitoa asisti kwa Deus Kaseke wakiiua Azam 1-0, CCM Kirumba Mwanza Februari 9 na pia alifunga moja wakiichapa 3-0 Kiluvya United katika 32-bora FA.
Kwa mara ya kwanza, Camara alitua nchini akitokea Milo FC, ambapo msimu uliopita aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21 na kuwavutia mabosi wa Singida, huku akizichezea pia, AS Ashanti Golden Boys na Wakriya AC zote za kwao Guinea.