Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bibi bomba wanaupiga hadi raha

MABIBI Pict

Muktasari:

  • Hii imekuwa kazi ya Rebecca Ntsanwisi mwenye umri wa miaka 57 kutoka Afrika Kusini ambaye ameanzisha timu za soka za mabibi katika baadhi ya nchi za bara hilo kwa lengo la kuboresha afya ya akili na mwili kwa wanawake wenye umri mkubwa.

LIMPOPO, AFRIKA KUSINI: WANAWEZA wasiwe na mbinu kama Lionel Messi au Cristiano Ronaldo, lakini hilo halijawazuia mabibi hawa wa Kiafrika kujifunza mbinu za kukaba na kupiga pasi.

Hii imekuwa kazi ya Rebecca Ntsanwisi mwenye umri wa miaka 57 kutoka Afrika Kusini ambaye ameanzisha timu za soka za mabibi katika baadhi ya nchi za bara hilo kwa lengo la kuboresha afya ya akili na mwili kwa wanawake wenye umri mkubwa.

Kwa sasa, timu tano kutoka Afrika zilikuwa zinashiriki kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Mabibi Wanasoka yaliyofanyika katika Jimbo la Limpopo, Afrika Kusini na mchezaji mzee zaidi alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 80.

Wazo la kuanzisha mashindano hayo liliibuka mwaka 2007 ikiwa ni kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha afya za wanawake wenye umri mkubwa wa eneo hilo na kujenga mshikamano katika jamii. Lakini, miaka nenda rudi tangu wakati huo mashindano hayo yamekuwa yakifanyika na timu kutoka Afrika na hata nje ya bara hushiriki mashindano hayo ya kimataifa ya mabibi wanasoka.

MABI 01

Katika mashindano ya mwaka huu, Mbele Nonhlanhla alivaa viatu vya mpira vya rangi ya fedha huku kocha wake akiwapa moyo wachezaji waliokuwa na miguu iliyopinda, migongo migumu na pumzi nzito katika chumba cha kubadilishia nguo.

Akiwa na miaka 63, akivalia jezi namba 10 na nywele zake zilizopakwa rangi ya kahawia, bibi huyo mwenye wajukuu saba hakuwa mchezaji wa kawaida alipokanyaga uwanja kwa mara ya kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa.

"Najisikia kama nyota wa soka," anasema Nonhlanhla kwa tabasamu akionyesha pengo mdomoni. "Wananiita mashine ya mabao."

Lengo la Nonhlanhla lilikuwa kubwa zaidi  ndoto ya kuwa maarufu kwenye soka ilikuwa karibu kutimia.

MABI 02

"Kamwe siyo kuchelewa kufanikisha ndoto zako za utotoni. Sioni kitu chochote kitakachonizuia (kuwa maarufu)," anasema huku akitembea kutoka kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwenda kumenyana na Ufaransa.

"Nimepiga nusu hatua tayari, sivyo?" Nonhlanhla anatabasamu.

Timu yake, Vuka Soweto, inatoka katika mtaa maarufu wa Soweto uliopo nje ya Johannesburg.

Ilijiunga na zaidi ya timu 12 kutoka Afrika na maeneo mengine kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa ya mabibi wanasoka huko Limpopo.

Mashindano hayo maarufu kama Kombe la Dunia kwa Mabibi yalidumu kwa siku nne na yalifanyika kwenye uwanja uliopo kando mwa milima.

MABI 03

Mechi zilichezwa kwa dakika 30, zikigawanywa vipindi viwili, kwa kasi ya polepole lakini yenye lengo la ushindi. Kulikuwapo na timu kutoka Marekani, Ufaransa, Kenya, Togo na kwingineko.

"(Lengo) ni kuzeeka ukiwa na afya bora. Kushinda au kushindwa si muhimu... (lakini) muhimu ni kufika hapa na kubaki na afya bora," anasema Devika Ramesar mwenye umri wa miaka 62 ambaye ni mama wa watoto wawili na bibi wa wajukuu watano kutoka Afrika Kusini.

Hadi wiki hii shabiki huyo wa Liverpool hakuwahi kukanyaga uwanja wa mpira.

Naye mshambuliaji wa timu ya Kenya, Edna Cheruiyot alikuwa na miezi miwili ya kujifunza kanuni nyingi za mpira kabla ya Ijumaa iliyopita alipofunga bao lake pekee.

Cheruiyot alijipiga picha za kumbukumbu ya safari ya kwanza ya kimataifa katika soka na kuzituma kwa wajukuu zake.

"Najisikia mwepesi. Huu (nilio nao sasa) ndio uzito mdogo zaidi tangu nijifungue mtoto wangu wa kwanza mwaka 1987," anasema Cheruiyot huku akirekebisha kilemba chake cha bluu kichwani kilichofunika nywele zilizoanza kuwa kijivu.

MABI 04

Akiwa na miaka 52 ni miongoni mwa wachezaji vijana zaidi katika timu yake, ambapo mchezaji mkubwa zaidi ana miaka 87.

Wazo la mashindano hayo lilitokana na changamoto binafsi ya mwasisi wake, Rebecca Ntsanwisi, mwenye miaka 57, maarufu kama Mama Beka baada ya kugundulika kuwa na saratani ambayo ilimfanya kutumia kiti cha magurudumu.

"Wanawake wazee wanahitaji kuungana na kufurahia. Tumekuwa tukisahaulika," anasema mama huyo akiwa nje ya nyumba anayoishi na wazazi wake ambao pia ni wazee, akitarajia mashindano yajayo yafanyike Kenya.

Takwimu za serikali ya Afrika Kusini zinaonyesha karibu asilimia 40 ya watoto nchini humo wanaishi katika kaya zinazoongozwa na babu na bibi zao, hasa kutokana na umasikini, mila na uhamiaji mijini.

"Huu ni wakati wetu wa kufurahia na kupumzika," anasema Ntsanwisi. "Nitakufa nikiwa najua nilifanya jambo."

Chris Matson mwenye miaka 67, alifuata ushauri huo na kusafiri kutoka Marekani hadi Afrika Kusini ili ashiriki mashindano hayo akidai kwamba lengo lake ni "kufurahia kila sekunde ya mashindano."

"Sikuwahi kucheza nikiwa mdogo, hivyo kufanya hivi sasa ni jambo la kushangaza," anasema kipa huyo mwenye furaha wa timu ya Marekani, New England Breakers.

MABI 05

Hata hivyo, madaktari wa timu zote walikuwa na kazi kubwa ya kuwahudumia wachezaji waliokuwa wakihitaji uangalizi wa mara kwa mara, kwa mujibu wa Dk Diana Mawila wa timu ya Afrika Kusini.

Anasema maumivu na uchovu wa wachezaji wazee vilihitaji ufuatiliaji na tiba za habari ili kuwawezesha kufurahia mashindano hayo.

Baadhi ya wachezaji wa timu yake iitwayo Vakhegula Vakhegula (linalomaanisha bibi bibi) walikuwa wakipimwa presha kabla ya kila mechi.

Jina hilo linahusiana na timu ya taifa ya wanaume ya Afrika Kusini, Bafana Bafana lenye maana ya vijana vijana.

Lakini katika mahojiano na vyombo vya habari, wachezaji walitania huku wakicheka wako fiti na hawahitaji vipimo vya kila mara.

"Tuko fiti!" anasema nahodha Thelma Ngobeni, huku akibeba kwenye kichwa chake pakiti ya unga wa mahindi waliopewa baada ya mchezo.

"Sio kuhusu kushinda au kushindwa. Kilicho muhimu ni kuwa tulifika, tukafurahi na tukajitahidi."

Mashabiki waliohudhuria mechi hizo walishuhudia mambo mengi vikiwamo vituko na vimbangwa vya mabibi hao ambao kuna wakati walishika mpira makusudi ulipotakiwa kuchezwa au kupiga wakati ulipaswa kurushwa mara ulipotoka nje ya uwanja.

Hata hivyo, ilikuwa ni furaha kwa wengi, kwani walishangilia kwa nguvu timu zilipoingia uwanjani mabibi hao wakiwa wameongozana huku wameshikana mikono na watoto waliovaa sare za timu, ilhali nyimbo za mataifa yao zikichezwa.