Hawa marefa utawapenda tu

Muktasari:
- Kelele zilimalizika baada ya kijana huyu mwenye umbo hafifu kumudu mchezo kwa weledi na kuvutia wachezaji na watazamaji.
MWEZI Mei mwaka jana zilisikika kelele Zanzibar baada ya Shirikisho la Kandanda la Afrika (CAF) kumchagua kijana wa miaka 15 wa Libya, Zakaria Ibrahim Al-Ghaithy, kuchezesha michezo ya fainali ya mashindano ya shule za Bara la Afrika.
Kelele zilimalizika baada ya kijana huyu mwenye umbo hafifu kumudu mchezo kwa weledi na kuvutia wachezaji na watazamaji.
Kelele za aina hii zinasikika kila anapotokea kijana mdogo kukabidhiwa jukumu la kuchezesha michezo mikubwa ya kimataifa ya kandanda.
Mpaka mwisho wa miaka ya 1950 waamuzi wengi wa kanda walikuwa watu wa umri wa makamo na wengine vizee waliokaribia siku za kutembea kwa kutumia mkongojo.
Mpaka mwishoni wa miaka ya 1970 karibu waamuzi wengi Tanzania walikuwa wenye umri wa miaka zaidi ya 35, baadhi yao wamechoka na wakikimbia kwa kujilazimisha.
Haikushangaza kusikia kelele 1958 Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (FIFA) lilipomteua kijana wa miaka 24 wa Hispania, Juan Garay Gardezabal kuwa mmoja wa waamuzi wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Sweden.
Kijana huyu alichezesha michezo saba katika katika fainali zile na zilizofuatia 1962 na 1966 na kuvutia watazamaji wengi. Wataalamu wa kandanda, waandishi wa michezo na mashabiki ambao waliikosoa FIFA kwa uamuzi wake huo walibadili mawazo na kukiri FIFA iliona mbali.
Hapo kabla baadhi ya magazeti maarufu ya michezo yaliandika makala za kuikebehi FIFA na kusema ilikuwa inaugeuza mchezo wa kandanda kuwa ni wa kitoto.
Waandishi wengine na viongozi wa kandanda, wakiwemo wale nchi zao zilifuzu kuingia fainali za Kombe la Dunia za 1962 walimtaka Sir Stanley Rous wa Uingereza, ambaye alikuwa Rais wa FIFA ajiuzulu.
Baada ya FIFA kutangaza waamuzi wa fainali za Kombe la Dunia zilisikika taarifa za badhi ya mashabiki wa kandanda kutaka kufanya fujo Zurich, Uswisi, ambako yapo makao makuu ya shirikisho hilo.
FIFA ilibidi kueleza uamuzi wake sio wa ajabu kwani mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia wa 1934 kati ya wenyeji Italia na Czechoslovakia ulichezeshwa na kijana wa Sweden, Ivan Eklend aliyekuwa na miaka 28. Italia ilishinda 2-1.
Lakini baada ya yule kijana wa Hispania, waandishi na watazamaji waliotaka kuandamana kupinga uamuzi wa FIFA wa kumchagua kushika filimbi, waliingia barabarani kumpongeza huyu muamuzi kijana.
Baadhi ya mashabiki walibeba mabango yaliyotaka yule kijana awe muamuzi wa michezo yote iliyobakia ya fainali za Kombe la Dunia.
Tokea wakati ule waamuzi wengi wa michezo ya fainali za Kombe la Dunia wamekuwa na umri wa chini ya miaka 35.
Gardeazabal alifariki 1969 akiwa na miaka 45 kutokana na kuugua saratani ya tumbo iliyogundlika miezi mitatu kabla ya kifo chake.
Alikuwamo katika orodha ya waamuzi waliochaguliwa kwa fainali zilizofanyika Mexico 1970 na kama kifo hakijamkuta hizo zingekuwa fainali zake za nne kuzishikia filimbi.
Mazishi yake yalihudhuriwa na wachezaji, waamuzi na makocha mashuhuri, wakiwamo wachezaji aliowasimamia na waamuzi alioshirikiana nao katika mashindano ya kimataifa.
Juan Gardeazabal alizaliwa Bilbao, jimbo la Basque, ambalo limekuwa kwa miaka mingi katika harakati za kutaka kujitenga na Hispania.
Baada ya kifo chake, moja ya barabara kubwa ya jiji hilo ilipewa jina lake kwa kuheshimu mchango alioutoa katika soka.
Mpaka leo mwamuzi huyu anatajika kuwa kijana mdogo kabisa kuchezesha fainali hizi katika historia ya mshindano ya Kombe la Dunia yaliyoanza Uruguay 1930.
Baada ya kuchezesha ligi za madaraja ya chini za Hispania kwa miaka mitatu alipandishwa daraja la kumuwezesha kuchezesha ligi ya daraja la kwanza ya nchi hiyo mwishoni mwa 1952.
Katika michezo mingi aliyochezesha ya madaraja ya chini kwao Hispania alikuwa siku zote ndio mwenye umri mdogo kulio wachezaji wote uwanjani.
Kwa kawaida waamuzi wengi wa mashindano ya kimataifa na hasa katika fainali za Kombe la Dunia huwa wenye kati ya miaka 30 na 45 na uzoefu mkubwa.
Waaamuzi wenye umri mkubwa kabisa kuchezesha michezo ya fainali za Kombe la Duna hizi ni pamoja na Gorge Rcader wa Uingereza aliyeshika filimbi ya mchezo wa fainali wa mashindano ya 1950 kwenye Uwanja wa Maracana, Brazil.
Mchezo ule ulihudhuriwa na watazamaji zaidi ya 174,000 ambayo ni rekodi ya dunia ya mchezo wa kandanda ulioshuhudiwa na watazamaji wengi kuliko mwengine katika historia ya kandanda.
Mchezo huo ulikuwa wa fainali kati ya wenyeji Brazil na Uruguay. Brazil ilipokonywa kombe nyumbani kwao kwa kufungwa 2-1 na Uruguay na siku ile mpaka leo husimuliwa kama ‘Maafa ya Maracana’. Hii ilitokana na watu wengi kuiaga dunia au kuumia kutokana na kushindwa kuyapokea matokeo ya mchezo ule.
Katika miaka ya nyuma waamuzi wakongwe ndio ambao FIFA iliwaamini kuwapa michezo migumu na yenye mvutano mkubwa.
Miongoni mwa waamuzi wakongwe waliopewa kazi hiyo ni George Reader wa Uingereza aliyechezesha fainali za 1950, Rudolf Glockner wa Ujerumani Mashariki aliyekuwa na miaka 51 alikuwa muamuzi wa fainali za 1970 na Nickolaj Latychev wa Urusi akiwa na miaka 49 alichezesha fainali za 1962.
Siku hizi FIFA imeweka miaka 45 kuwa kiwango cha juu cha umri wa muamuzi kwa mashindano ya kimataifa. Hata muamuzi awe mzuri vipi akifikia miaka 45 hupuliziwa filimbi ya mwisho ya kumtaka atoke nje ya uwanja na kuwa mtazamaji.
Miongoni mwa waamuzi waliopendwa zaidi duniani ni Perluigi Collina wa Italia ambaye alitajwa “Mwamuzi Bora Duniani” na Shirikisho la Kimataifa la Historia ya Soka na Takwimu mara sita mfululizo kutoka 1998 hadi 2003.