SPOTI DOKTA: Balaa la mbu katika vibanda umiza

Muktasari:
- Siyo kwamba wanaotazama mpira maeneo hayo huwa makwao hakuna runinga, bali kinachowapeleka huko ni ushabiki, mabishano, utani wa furaha, uhuru, vituko vya watazamaji na matangazo katika mabango.
MOJAWAPO wa burudani nzuri inayochangamsha na kuleta furaha isiyo na kifani kwa wapenda kandanda ni kwenda kutazama soka mtaani - katika mabanda ya Uswahilini maarufu vibandaumiza au baa.
Siyo kwamba wanaotazama mpira maeneo hayo huwa makwao hakuna runinga, bali kinachowapeleka huko ni ushabiki, mabishano, utani wa furaha, uhuru, vituko vya watazamaji na matangazo katika mabango.
Vitu hivyo ndivyo ambavyo vinawavutia watu wa kawaida ambao pengine kwenda kutazama mechi uwanjani ni mbali au ni gharama kubwa.
Baadhi ya nyakati maeneo hayo ambayo mengine huwa yamejitenga au yapo katika msongamano ni kawaida kukutana na kadhia ya kung’atwa na mbu ambako huwa ni wengi.

Kesho, Ijumaa, Aprili 25 ni Siku ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya Malaria duniani chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO), na Tanzania na wadau wengine wa afya wataungana kuadhimisha siku hiyo.
Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2025 inasema ‘Malaria inamalizwa na sisi: Wazia tena, Wekeza tena, Washa tena”. Hii ni kampeni ya msingi ambayo inalenga kuongeza nguvu katika ngazi zote. Malaria husababishwa na vimelea vya Plasmodium ambao huenezwa kwa watu kwa kuumwa na mbu jike aina ya Anopheles.
Kuna aina tano za vimelea vinavyosababisha malaria kwa binadamu - P.Falciparum ndio hatari zaidi katika Bara la Afrika. Hii ni kutokana na kusababisha vifo vingi vinavyohusiana na malaria duniani kutokana na kusababisha malaria kali zaidi.
Katika kuunga mkono mapambano hayo tutaangazia vibandaumiza na baa zilizo maeneo hatarishi ambazo watu humiminika kupata burudani za soka na mengineyo kupitia runinga kubwa na zenye sauti kubwa.
Baadhi ya mashabiki wanapokuwa wanatazama burudani katika vibanda hivyo huumwa na mbu wakali hasa mida ya jioni kuanzia saa 12:00 kipindi ambacho ndio mechi nyingi huwa zinaisha au kuanza.
Baadhi ya vibandaumiza na baa huwa waungwana angalau hutoa dawa za kuchoma ili kufukuza mbu. Hatua hiyo si mbaya kwani wanaonyesha kufahamu mapambano dhidi ya malaria.
Inaeleweka kwamba baadhi ya vibandaumiza na baa vipo katika maeneo yaliyozungukwa na vichaka, mifumo mibovu ya majitaka na vidimbwi vyenye maji yaliyotuama hasa kipindi hiki cha mvuamvua.

Mazingira kama hayo ndio yanayochangia kuwepo kwa mbu wengi ambao ni wale wenye vidoa vyeupevyeupe ambao huwa sio wanaoeneza vijidudu vya malaria.
Aina hiyo ya mbu wanauma sana na kusababisha muwasho huku baadhi ya watu wakipata mtutumko wa ngozi au uvimbe. Kila mtu katika jamii angalau amewahi kuugua malaria katika maisha. Hivyo huwa ni kawaida kupata hofu anapoumwa na mbu mahala popote anapokuwepo.
BADO TISHIO
Kila mwaka malaria huwakumba zaidi ya watu milioni 200 na kuwaua zaidi ya 600,000. Vifo vingi kati ya hivyo karibu nusu milioni miongoni mwavyo ni watoto wadogo katika Bara la Afrika.
Kulingana na ripoti ya WHO ya malaria ya hivi karibuni kulikuwa na visa milioni 263 vya malaria 2023 ikilinganishwa na milioni 252 mwaka 2022.
Idadi inayokadiriwa ya vifo vya malaria ilifikia 597,000 mwaka 2023 ikilinganishwa na 600,000 ule wa 2022. Habari nzuri ni kwamba ugonjwa huo unazuilika na kutibika na muhimu kuzingatia njia za kujikinga na kuharibu mazingira yanayochochea mbu kuzaliana.

Vilevile tayari kuna chanjo za malaria ambazo zipo katika majaribio zikionyesha ufanisi mkubwa katika kukinga watu dhidi ya vimelea vya malaria.
Watoto wachanga, wale wa chini ya miaka mitano, wajawazito, wasafiri na wenye VVU au Ukimwi wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa.
JIKINGE HIVI NA MBU
Malaria inaweza kuzuiwa kwa kuepuka kuumwa na mbu na kwa kutumia dawa. Matibabu ya mapema yanaweza kuzuia malaria ya wastani kuwa kali.
Wenye vibandaumiza wanatakiwa kuhakikisha kwamba maeneo yenye vichaka yanasafishwa, kurekebisha mifumo ya majitaka na kuhahakisha wanazingatia kununi za afya kwa kuondoa madimbwi na vituamisha maji.
Pia wanaweza kutumia dawa za kupulizia katika mazingira ya vibanda vyao au baa. Kama wanatumia dawa za kuchoma wahakikishe wanatumia kwa kufuata maelekezo yaliyoandikwa.
Malaria inaweza kuzuiwa kwa kuepuka kuumwa na mbu na kutumia mafuta au cream za kupaka za kufukuza wadudu na vaa mavazi ambayo yatamnyima nafasi mbu kukung’ata.
Wamiliki wenye vibandaumiza wanaweza kuweka vijimashine vya ki-eletroniki vya kufukuza mbu vinavyotumia umeme.
Unapokuwa nyumbani kwako punguza hatari ya kupata malaria kwa kuepuka kuumwa na mbu, na vilevile hakikisha unatumia vyandarua vilivyowekwa dawa. Dawa za kujipaka ikiwamo cream, mafuta na losheni ni salama - hakikisha unanunua katika maduka ya dawa yanayotambuliwa na serikali.
MAZOEZI NA LISHE BORA
Mwili mzima wa binadamu huathiriwa kwa ujumla na mazoezi. Mazoezi huathiri fiziolojia ya kila mfumo na kusababisha mabadiliko mbalimbali ambayo kwa ujumla huathiri afya ya mwili.
Mazoezi ya mara kwa mara na lishe bora ya matunda na mbogamboga pamoja na protini vinaweza kusaidia kujenga kinga madhubuti yenye kustahimili magonjwa ikiwamo malaria.
Mbali na mazoezi kula zaidi matunda, mbogamboga pamoja na lishe yenye protini nyingi kama vile nyama, kuku, samaki na kunde kukuwezesha kukabiliana na maambukizi.

CHUKUA HII
Madume ya mbu hayawezi kuuma kwa sababu hukosa sehemu mahsusi za mdomo zinazohitajika kutoboa ngozi, hivyo hayawezi kusambaza magonjwa.
Kwa upande wa mbu jike huhitaji protini kutoka kwenye damu kwa ajili ya ukuzaji wa mayai na wana mfumo katika mdomo unaowawezesha kuuma na kufyonza damu juu ya ngozi.
Mara tu wanapojaza damu tumboni hupumzika kwa siku kadhaa kabla ya kutaga mayai. Ili kupata damu, majike hutafuta na kuuma wanyama kama vile binadamu na yanaweza kusambaza magonjwa wakati yanafyonza damu.
Taafiti zinaonyesha kuwa mbu jike wanaosambaza malaria wana tabia ya kuvizia kuuma nyakati za usiku zaidi ilhali aina ya mbu wajulikanao kama Aedes wenye vidoadoa vyeupe huuma zaidi jioni.