Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hili ndilo anguko la Dullah Mbabe

DULLAH Pict

Muktasari:

  • Mbabe mwenye rekodi ya kucheza mapambano 51 ikiwa sawa na raundi 232, amefanikiwa kushinda 34 kati ya hayo 29 ni kwa knockout (KO) na amepigwa mara 15 kati ya hizo ni mara tatu ndiyo ameonja kichapo cha KO huku akitoka sare mara moja.

AGOSTI, mwaka 2021 ndiyo ulikuwa mwisho wa utawala wa bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Abdallah Pazi maarufu Dullah Mbabe kutokana na kupigwa kwa pointi na aliyekuwa mpinzani wake wakati huo, Twaha Kiduku.

Mbabe mwenye rekodi ya kucheza mapambano 51 ikiwa sawa na raundi 232, amefanikiwa kushinda 34 kati ya hayo 29 ni kwa knockout (KO) na amepigwa mara 15 kati ya hizo ni mara tatu ndiyo ameonja kichapo cha KO huku akitoka sare mara moja.

Pambano hilo lilikuwa ni moja kati ya mapambano ya kisasa lenye upinzani mkubwa ambalo lilishuhudiwa na watoto wa 2000 tofauti na wakati wa upinzani wa Francis Cheka na Rashid Mtamla au Maneno Osward ‘Mtambo wa Gongo’ na Rashid Matumla.

Ukubwa wa pambano lao ulitokana na promosheni ya Peaktime Media ambayo ilikuwa ikifanya vizuri wakati huo kuwawekea mabondia gari aina ya Toyota Crown ambayo ilibatizwa Crown mtoa roho.

DULL 01

Ukweli ambao Mwanaspoti linaufahamu pambano hilo ndilo lilimmaliza Dullah Mbabe licha ya mwenyewe kushindwa kuweka wazi kwa kuwa ndilo lilimfanya apotee kwenye mchezo kutokana na kichapo alichopokea katika pambano ambalo aliamini ameshinda, lakini tu zilifanyika hila.

Hadi kesho ukimuuliza Dullah Mbabe anaamini ndiye mshindi wa pambano kati yake na Twaha Kiduku, lakini mwamuzi aliyechezesha Pendo Njau hakuweza kumhesabia Kiduku alivyondondoka bila ya sababu ya msingi na matokeo yake mwisho akapigwa yeye.

Kupigwa kwake kulikuwa gumzo na mwenyewe hakutaka kukubali ukweli wa kupigwa hali ambayo ilimfanya akubali kusaini pambano lingine gumu la kimataifa dhidi Alex Kabangu katika kipindi cha siku 90 ambazo ukweli ilikuwa hatari kwake.

Mbabe alikubali kusaini kupigana kwenye pambano ili tu kuzima kelele za kupigwa kwake na Kiduku, lakini alisahau muda mwingi alioutumia kufanya maandalizi ya pambano lake na Kiduku ambao umekuwa ukimhukumu.

Matokeo yake, Mbabe akabadilishiwa bondia juu kwa juu kutoka Kabangu na kuja Tshimanga Katompa ambaye alimuongezea yale maumivu ya Kiduku.

DULL 02

Mbaya zaidi katika pambano hilo, Mbabe alipigwa hasa huku mguu wake wa kushoto ukiwa mzito. Hakuwa tena Mbabe aliyemstaafisha ngumi Francis Cheka, alipigwa na kejeli za mashabiki zikawa juu dhidi yake.

Kipigo cha pointi kutoka kwa Katompa kilimfanya ajitokeze hadharani na kudai kuwa ataachana  na ngumi kwa muda kwa ajili ya kuweka mwili wake kuwa sawa pamoja na kuwaomba radhi Watanzania na mashabiki wake kwa matokeo mabaya mfululizo.

Itakumbukwa kutoka kwenye kinywa chake akiongea kwa uchungu akisema: “Nimeenda kupambana kama mwanaume na kama bondia na ukweli kwa nguvu za Mwenyezi Mungu, nimepambana hadi mwisho na matokeo yametokea hayo.

DULL 03

“Sema niwaambie Watanzania kwamba samahani kama kuna mtu yeyote amekasirika au nimemkwaza kwa matokeo yaliyotokea. “Hata mimi ni mpambanaji, natamani nipate matokeo chanya, nina mechi zaidi ya 26 nimewapiga watu, (lakini) kwa hizi mechi mbili nilizopoteza nawaomba Watanzania tupeane moyo, tuache lugha ya matusi kwenye mitandao ya kijamii, tuache kashfa, tufanye kazi, hizi ni ngumi na kama ukiona nakosea panda wewe ulingoni halafu utaelewa kama kachumbari mboga au inasaidia siku za shida.”

Lakini baada ya hapo, Mbabe hakuwahi kujipa muda wa kutosha kumaliza tatizo la mguu wake ambaye aliwahi kukiri ulikuwa na changamoto wakati wa maandalizi ya pambano lake dhidi ya Kiduku kutokana na ugumu wa mazoezi aliyokuwa akifanya kwani aliendelea kupanda ulingoni katika mapambano ya kujiweka sawa ambayo ukweli hayakuwa msaada wa kumrudishia ubora wake.

Licha ya mwenyewe kuamini ubora wake umerudi akaomba arudiane na Katompa, Arusha, matokeo yake alipigwa lakini ajabu alipoulizwa akazungumzia kuwa ameshinda bila shida huku akitoa lawama kwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kwamba imekuwa ikimchukia lakini baadaye aliomba radhi.

Bondia huyo mguu wa kushoto aliouangukia wakati akipigwa na Katompa ndiyo huohuo aliuangukia katika pambano dhidi Callum Simpson ambalo alipigwa kwa knockout ya raundi nne nchini Uingereza ambayo ilikuwa gumzo kiasi cha bondia mwenzake, Hassan Mwakinyo kutoa kauli akimshauri ajiimarishe zaidi.

DULL 04

Katika makala ya  Mwanaspoti Aprili 12, mwaka jana, Mbabe alipoulizwa suala kama aliwahi kutumia mihadarati kama tuhuma zilivyokuwa zilivyoshushwa kwake na bondia maarufu nchini, haya ndiyo yalikuwa majibu yake: “Kwanza neno mihadarati lina maana gani? (akafafanuliwa na mwandishi), hilo moja halafu jambo la pili mimi sina vikundi vya ajabu, lakini jambo la tatu situmii kilevi cha aina yoyote yaani siyo mtumiaji kwa sababu kama ni pombe naweza kukaa mpaka miaka miwili bila  kutumia ingawa kuna siku naweza kunywa bia zangu mbili au moja.

“Lakini kuhusu sijui mirungi sijawahi kabisa kutumia ila bangi siwezi kukataa kwa sababu niliwahi kuvuta nikiwa darasa la pili wakati nipo kwetu nasoma, ingawa sasa watu wengi wanajuaga mimi navuta bangi au wanajua mimi mhuni sana.

“Binafsi siyo mhuni wala mvuta bangi, mimi ni mtu wa kawaida kabisa na ndiyo maana nina mashabiki wengi na wala hujawahi kusikia nina kesi ya kumkaba mtu.

“Unajua kila mtu anaongea lake ila kama kuna mtu ameshaniona labda natumia hiyo mihadarati kama bangi, basi alete ushahidi ingawa Waswahili wanasema anapokufa nyani miti yote huteleza hivyo waache waongee.

“Kwangu ngumi ndiyo mchezo ambao umebadilisha mambo mengi maana nilipotokea na nilipo ni maisha tofauti. Najua kuna watu wananiongelea vibaya lakini hawafikii hata robo ya maisha yangu.

“Nataka nikwambie kwamba nauheshimu sana huu mchezo kwa sababu nimetoka katika kukata mkaa, kuchoma na kuuza, nimetengeneza sana majiko pale Kijitonyama na hadi bodaboda nimeendesha hivyo siwashangai.

“Hawajui tu ila kwanza sijapanga naishi kwangu, watoto wangu wanasoma katika shule ya English medium na nina usafiri wangu naweza kwenda ninapotaka wakati wowote. Kifupi siwezi kuwazuia watu kuongea wanachotaka.

“Binafsi bado naamini mchezo wa ngumi ndiyo umenifanya wanijue, umesababisha niende Ulaya mara nyingi na ndiyo umenipa mafanikio makubwa ya kimaisha.”

DULL 05

Lakini Mwanaspoti lilikuwepo katika pambano la wikiendi iliyopita la ‘Knockout ya Mama’ ambalo Mbabe alipigwa kwa pointi za majaji wawili kwa moja na mpinzani wake kutoka Zambia, Mbachi Kaonga.

Kabla ya pambano hilo, Mbabe alichelewa kufika na pambano lake lilikuwa la tano kufanyika kati ya mapambano 14 yaliyofanyika siku hiyo jambo ambalo lilifanya apande ulingoni bila kufanya  ‘warm up’ kitu ambacho kilikuwa faida kwa mpinzani wake aliyeanza kupasha misuli saa moja usiku alipowasili ukumbini na baada ya kupigwa alijiliza kwa aibu inayoendelea kumuandama kila anapotaka kuinuka.

Lakini, Mwanaspoti lilishangazwa zaidi na bondia huyo juu ya kuzungumzia suala la matatizo ya miguu yake mbele ya msemaji mkuu wa Serikali na katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa wakati alipokuwa akipokea zawadi ya Sh2 milioni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na mchango wake kwenye mchezo huo kama bondia mkongwe anayeendelea kuhamasisha vijana kucheza.

Mbabe hakuishia hapo kwani aliposhuka alionyesha hadi picha kwenye simu yake kwa waandishi wa habari kuwa anasumbuliwa na miguu na ametoka kufungua plasta ngumu (POP) wiki moja kabla ya pambano, huku watu wake wa karibu wakidai kuwa siku hizi siyo mtu wa kupenda mazoezi.

Yote katika yote ni kwamba, Mbabe ni jina kubwa katika ngumi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na anastahili kuendelea kulilinda ili hadhi yake isiendelee kushuka.