Prime
JICHO LA MWEWE: Fei Toto atafika mbinguni amechoka hoi, tumpumzishe

Muktasari:
- Ukienda mitandaoni kuna mambo mawili. Lazima kurasa za wanahabari zimhusishe kwenda Simba au kurudi Yanga. Lakini hapo hapo lazima katika kurasa yake mwenyewe hata akiweka picha yake binafsi katika maisha yake binafsi, lazima maoni ya wengi katika picha hiyo ni kumtaka aende Simba au Yanga.
NA kama kuna mwanadamu ambaye atakuwa analala hoi basi ni Feisal Salum, 'Fei Toto'. Namna ambavyo siku yake nzima inaambatana na mambo mawili. Jambo la kwanza ni kufanya mazoezi au kucheza mechi. Jambo la pili ni kusoma ushauri wa kwenda Simba au kurudi Yanga.
Ukienda mitandaoni kuna mambo mawili. Lazima kurasa za wanahabari zimhusishe kwenda Simba au kurudi Yanga. Lakini hapo hapo lazima katika kurasa yake mwenyewe hata akiweka picha yake binafsi katika maisha yake binafsi, lazima maoni ya wengi katika picha hiyo ni kumtaka aende Simba au Yanga.
Ukifungua magazeti yetu ya kila siku lazima utasoma vichwa vya habari kama hivi. "Dili la Fei Toto kurudi Yanga liko hivi." "Ni suala la muda Simba kumalizana na Fei Toto". Lazima Fei atakuwa amelala akiwa hoi. Lazima.
Kwanini hii inatokea? Ni kwa sababu Watanzania hawaamini kwamba mchezaji mkubwa kama Fei anaweza kuondoka timu kama Yanga au Simba akiwa katika ubora wake na kwenda kucheza Azam. Iliwahi kutokea kwa Mrisho Ngassa na hali ilikuwa kama hivi.

Wakati ule hakukuwa na mitandao, lakini kila mahali ulikuwa ukikaa unaambiwa namna ambavyo watu wa Yanga walikuwa wanamtaka kijana arudi nyumbani kwake. Ilikuwa presha kubwa kutoka katika magazeti na vijiwe vya kahawa.
Zaidi ya hili ni kwamba nyota ya Fei imeendelea kung’ara akiwa na Azam. Kuna wale wataalamu wa kumuombea mchezaji mkubwa mabaya pindi anapoondoka Simba au Yanga na kuendelea kucheza hapa hapa nchini.
Kwa Fei jambo hili limekwama kwa sababu Fei ameendelea kuwa Fei yule yule tu. Ameendelea kuwa mtamu kama alivyo na kiwango chake kimeendelea kuwa juu. Anafunga mabao, anasaidia timu yake kufunga mabao katika kiwango kile kile ambacho alikuwa nacho wakati akiwa Yanga.

Simba na Yanga ni wabinafsi. Hawataki timu nyingine yoyote iwe kubwa nje ya wao. Zamani kidogo kulikuwa na simulizi ya uongo kwamba mashabiki wangependa zitokee timu nyingine kubwa zianzishe upinzani kwa Simba na Yanga. Kumbe mashabiki waliokuwa wanasema hivi walikuwa wanazidanganya nafsi zao.
Fei kwenda Azam ilileta chuki kutoka kwa mashabiki wa Yanga. Mchezaji wa Azam akienda Yanga haina shida. Mchezaji staa wa Yanga akienda Azam inaleta chuki. Jiulize kwanini Prince Dube hatazamwi kwa jicho la chuki.
Wachezaji kama Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula na John Bocco walipotoka Azam kwenda Simba haikuleta chuki lakini kama kundi hili la wachezaji wanne wangetoka Simba kwenda Azam ingeleta chuki kama ilivyo kwa Fei.

Na sasa ni rasmi kuna kampeni ya vyombo vya habari pamoja na mashabiki kuhakikisha Fei anarudi timu kubwa. Kila mtu anavutia kwake, lakini ilimradi Fei arudi Kariakoo. Ni kampeni hasa na ambayo wakati mwingine inaikosea heshima Azam.
Wakati huu Azam ikiwa inajikongoja, watoa hoja huwa hawatoi ushauri kwa familia ya Mzee Bakhresa apambane kumpelekea Fei wachezaji wa maana ili Azam iende juu. Hapana. Hoja ni za kumchomoa Azam aende katika timu zao.
Ni tatizo la kuwa na timu mbili kubwa pekee. Hispania hauwezi kulazimisha mchezaji wa Atletico Madrid aende Barcelona au Real Madrid kwa sababu Atletico wenyewe nao ni wakubwa. Pale England pia nako kuna wakubwa wengi na hauwezi kulazimisha mchezaji mmoja aende kwingineko.

Mpaka leo Harry Kane hajacheza Manchester United, Manchester City, Arsenal, Chelsea au Liverpool. Ni mchezaji mkubwa kweli kweli wa Kiingereza. Hata hivyo, England wakubwa ni wengi. Sisi tunalazimisha Fei lazima acheze Simba au Yanga.
Kitu kibaya kwa Azam ni kwamba baada ya presha kubwa kutoka kwa wanahabari na mashabiki ni lazima mchezaji mwenyewe aanze kubadili mawazo. Lazima mchezaji akumbwe na presha ya kuchukua uamuzi wa kurudi Kariakoo.
Wachezaji wa kigeni huwa wanapenda fedha zaidi kwa sababu wametoka katika nchi za Kibepari. Sisi wachezaji wetu huwa wanapenda mapenzi kuliko pesa. Ni rahisi kwa hili la kurudi Kariakoo kuwaingia bila ya kujali fedha. Ni kama wakati ule Ngassa alipobadili akili yake na kulazimisha kurudi Jangwani akipitia Mtaa wa Msimbazi. Haikuwa kwa sababu ya pesa. Kuna mtu ana pesa kuliko Bakhresa?

Nadhani presha ikiwa kubwa zaidi kwa Fei basi ataamua kurudi zake Jangwani au kwenda Msimbazi. Sababu zake zinaweza kuwa nyepesi tu kama hii ya kwamba akiwa Simba na Yanga atakuwa katika nafasi nzuri ya kucheza mechi za kimataifa kuliko akiwa Azam.
Lakini kuna ukweli kwamba Azam yenyewe nayo inasaidia kumpa sababu Fei kwenda Simba au Yanga. Inasuasua sana katika misimu ambayo Fei amepambana kwa hali na mali kuisaidia timu ifikie malengo yake. Fikiria kwamba msimu huu wanaweza kuambulia nafasi ya nne katika msimamo.
Tuendelee kutazama kwa makini filamu hii ya Fei Toto kurudi Kariakoo. Lazima itakuwa inamchosha kila siku. Binafsi natabiri mabaya kwa Azam kwa sababu hawa wakubwa wana tabia ya kupiga presha ambayo inakuja kukuingia katika damu.
Hata wao kwa wao kuna wakati wanaingia katika kampeni ambayo mwishowe inakuwa mbaya kwa mmoja wao. Ni kama ile kampeni ya Clatous Chama kwenda Yanga. Ilifanyika kampeni kubwa kutoka kwa viongozi hadi mashabiki na mwishowe ikamuingia Chama mwenyewe. Na hatimaye Chama alijikuta anavaa jezi ya njano na kijani kutimiza ndoto za wapiga kampeni.