JICHO LA MWEWE: Samatta hadi Diamond, iko wapi sapoti ya mastaa?
Muktasari:
Sio lazima upende ambacho staa mwingine anakifanya. Lakini wenzetu wana mitandao ya kupeana sapoti. Kitu muhimu ni kuchangia wimbo wa taifa, lugha ya taifa, hisia za kitaifa na kila kitu kinachowaunganisha kama raia wa nchi moja.
SEPTEMBA 7, 1996, Mwanamuziki maarufu wa Marekani, Tupac Shakur alipigwa risasi wakati akitokea katika Ukumbi wa MGM Grand jijini Las Vegas Jimbo la Nevada. Alikuwa akitokea kutazama pambano la ngumi la uzito wa juu kati ya Mike ‘Iron’ Tyson dhidi ya Bruce Seldon. Alikufa siku sita baadaye. Tupac alikuwa mshikaji wa Tyson, asingeweza kukosa pambano lile. Ndio utamaduni wa mastaa wa Kimarakeni na kwingineko. Leo akipigana Flyod Mayweather utawaona kina Lil Wayne, Beyonce, Jay Z na wengineo.
Sio lazima upende ambacho staa mwingine anakifanya. Lakini wenzetu wana mitandao ya kupeana sapoti. Kitu muhimu ni kuchangia wimbo wa taifa, lugha ya taifa, hisia za kitaifa na kila kitu kinachowaunganisha kama raia wa nchi moja.
Haishangazi kuona mwaka 1994, Tiger Woods alidaiwa kutofahamu kuwa Kombe la Dunia lilikuwa linachezwa katika nchi yao ya Marekani. Lakini alipoulizwa anadhani ni nchi gani ambayo ilikuwa na nafasi ya kutwaa taji hilo akajibu kwa kifupi “Marekani”. Akabeba fimbo yake ya kuchezea gofu na kuondoka zake.
Ni hisia tofauti na Tanzania. Jana jioni, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walikuwa Watanzania waliokuwa wanakaribia kuweka historia. Mbwana alikuwa anakaribia kuweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kuwa Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Na kwa jumla, yeye na Ulimwengu walikuwa wanakaribia kuweka rekodi ya kuwa wachezaji wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa. Mpaka juzi nilikuwa sioni sapoti yoyote kutoka kwa mastaa wenzao wa fani mbalimbali.
Umewahi kusikia Diamond Platinum akitaja jina la Samatta katika wimbo wake wowote ule? Haijalishi kama anapenda soka au hapendi, yeye au watu wake wa karibu walipaswa kujua kuwa kuna Mtanzania yupo sehemu fulani anafanya fani fulani na anafanya vizuri sana.
Lakini kwanini umlaumu Diamond? Uliwahi kusikia Samatta au Ulimwengu wakiandika maelezo katika kurasa zao binafsi wakiomba Diamond apigiwe kura kwa wingi katika tuzo nyingi anazoshiriki? Labda nina bahati mbaya sijawahi kuona.
Umewahi kuona Diamond akilitaja jina la Hasheem Thabeet katika nyimbo zake? Umewahi kumsikia Wema Sepetu na maelfu ya mashabiki wake akimpa sapoti Samatta kupitia ukurasa wake wa Facebook au Instagram?
Wachezaji, wasanii, wanamitindo, wanamuziki wanaishi katika dunia tofauti Tanzania. Hakuna mwenye habari na tukio kubwa la mwenzake. Kila mtu anaishi na watu wa fani yake. Bahati nzuri wana timu ya wasimamizi wao ambao wanajua kinachoendelea lakini hawawasimamii vema watu wao. Wenzetu huwa wanaishi maisha haya. Hata kama akitokea staa wa mchezo ambao haupendi kabisa lakini unatoa sapoti kwa sababu ni Mtanzania tu na anafanya vizuri. Hata kama akiwa staa wa mchezo wa Hockey na haujui hata unavyochezwa, lakini kama staa wa mchezo huo anatoka Tanzania inabidi ujivunie tu na kumsapoti.
Maisha ya kawaida ya mastaa wa Tanzania yametawaliwa na umbea wa mitandaoni, fitina na chuki. Ni tofauti na tamaduni za nchi mbalimbali. Jaribu kufikiria marehemu Pepe Kalle alipokiimba kikosi cha Cameroon kilichofanya vizuri katika michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 1990 iliyofanyika Italia.
Pepe Kalle anasikika akiwataja akina Cyrille Makanaky, Roger Milla, Emmanuel Kundé, François Omam-Biyik na wengineo. Hapo alikuwa akionyesha sapoti kwa Bara la Afrika. Na ndio maana haishangazi sana kuona kuna urafiki mkubwa kati ya Didier Drogba na Fally Ipupa.
Umewahi kusikia Mwanamuziki wa Congo akiwataja kina Lionel Messi au Cristiano Ronaldo katika nyimbo zake? Hapana, anaangalia kwanza wachezaji wa taifa lake, kisha anahamia katika wachezaji wa bara lake.
Hii ndio tofauti kubwa iliyopo kati ya ushamba wa mastaa wetu wa fani mbalimbali na uweledi wa mastaa wa nje. Huwa wanatoa sapoti katika ngazi za nchi yao kisha wanatoa sapoti katika ngazi ya bara lao. Na wala haitashangaza kuona wanamuziki wa Congo wakiimba nyimbo za kuwatukuza Samatta na Ulimwengu kabla ya Wanamuziki wa Tanzania kufanya hivyo.
Msingi wa yote haya unatokana na kupotea kwa tabia ya uzalendo nchini. Sijui tulijikwaa wapi, lakini hata wageni wanaokuja hapa nchini kuiba rasilimali zetu wanatumia ukosefu wa uzalendo miongoni mwetu kupata mianya ya kuiba.
Ni rahisi kwa mgeni kuiba huku Mtanzania akishirikishwa na kuikomoa nchi yake. Na ndipo tulipofika. Ukosefu wa misingi hii ya uzalendo unaanza kuiona katika vitu vya kawaida machoni kama hili nililolizungumzia.
Hivi unaaamini kuna Watanzania ambao huwa wanapiga kura zao kwa wanamuziki wa Nigeria kama Davido kwa ajili ya kumkomoa Diamond Platinum? Huku ndiko tulikofika. Unadhani Mtanzania wa namna hii hawezi kushirikiana na Davido kuiba rasilimali za nchi yetu endapo Davido ataamua kufanya hivyo. Hii ni tafakuri thabiti.