Kwa Mtanzania mwaka 2022 ni mbali sana!
Muktasari:
Jana nilikuwa napitia majina ya wachezaji walioitwa kujaribu kuikoa timu yetu ya Taifa. Wapo akina John Bocco, Hassan Dilunga, Oscar Joshua, Elius Muguli na wengineo. Ndio majina ambayo tumeyazoea, hata kama hayana mafanikio katika medani ya kimataifa.
MWANADAMU ameendelea kuishi maisha ya kibinafsi, hasa katika nchi inayoitwa Tanzania. Anaiwaza zaidi siku ya leo. Anaitazama vema jioni ya leo. Kesho ni siku nyingine. Hana habari nayo.
Jana nilikuwa napitia majina ya wachezaji walioitwa kujaribu kuikoa timu yetu ya Taifa. Wapo akina John Bocco, Hassan Dilunga, Oscar Joshua, Elius Muguli na wengineo. Ndio majina ambayo tumeyazoea, hata kama hayana mafanikio katika medani ya kimataifa.
Nadhani wamerudishwa kuungana na akina Mbwana Samatta katika mpango wa kujaribu kuipeleka Taifa Stars katika michuano ya AFCON mwakani nchini Morocco.
Mpango wa kwanza wa kukusanya vipaji katika kila kona ya Tanzania umehitimishwa katika pambano dhidi ya Burundi Jumamosi jioni. Kila aliye na macho ameshuhudia jinsi mpango ule ulivyofeli na kutoweka mithili ya siagi katika kisu cha moto.
Ubinafsi wa Mtanzania naona pale jinsi ambavyo mamilioni ya shilingi za wadhamini wa TFF yameteketea katika mpango usio na kichwa wala miguu katika kuendeleza soka nchini. Tungeweza kufanya kitu zaidi katika mamilioni hayo.
Kwa sasa, kwa jinsi ninavyoitazama Tanzania, kama ina mawazo ya kucheza Kombe la Dunia nadhani yanapaswa kuelekezwa katika fainali za michuano hiyo itakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022.
Ni vigumu kwa Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwenda Russia 2018.
Mamilioni yaliyotumika katika mradi huu usio na kichwa wala miguu yalipaswa kujikita katika kung’amua vipaji vya watoto wenye umri wa miaka 14 nchini kote kwa ajili ya kuviunganisha na kuvilea kwa maandalizi ya miaka tisa ijayo.
Mradi huo ungekwenda sambamba na kuchomekea watoto hao katika shule za soka za klabu mbalimbali kubwa na ndogo barani Ulaya. Ndivyo Senegal walivyofanya katika mchakato wa kupata timu iliyofika Robo Fainali ya Kombe la Dunia nchini Japan na Korea Kusini mwaka 2002.
Lakini mwanadamu wa Tanzania amejaliwa ubinafsi. Mpango wa maboresho ya timu ya taifa uliojaa fikra za haraka haraka za mafanikio na sifa binafsi kwa watawala wakiwa wanaamini kuwa safari ya Morocco ingepatikana kwa kumchukua kijeba wa Kijiji cha Mbozi na kumuunganisha na Mbwana Samatta.
Wengi tunawaza kwamba kama mtu ukifa leo basi hauwezi kukumbukwa kwa misingi uliyoiweka. Hata wadhamini wanaamini katika hilo. Wanaamini kuwa kama wakiondoka katika udhamini wa Taifa Stars leo, basi hawawezi kukumbukwa kwa msingi wa mafanikio ya miaka 20 ijayo.
TFF zote zilizopita zilifanya makosa haya. Pia hata TFF iliyopo inajaribu kurudia makosa haya. Watu wanaiwaza zaidi siku ya leo na ufalme wa saa 12 zilizopo kuliko heshima (legacy) ya muda mrefu ujao.
Matokeo yake soka letu limeendelea kuwa la viraka kila kukicha. Mamilioni yaliyoteketea kwa kusambaza watu mikoani kisha baadaye wakakutana Lushoto, halafu baadaye timu ikaweka kambi Tukuyu yamepotea ndani ya dakika 90 za pambano dhidi ya Burundi.
Hata hivyo kama tungeachana na sifa za ghafla, kisha tukajikita katika mipango ya muda mrefu ambayo tungeweza kuvuna hata wakati tumekufa, nadhani ufalme wa kumbukumbu ungebaki kwa muda mrefu uliopo.
Ni kama ambavyo leo, Victor Stanculescu anakumbukwa kwa kutengeneza kizazi cha akina Juma Pondamali. Ni kitu kitakachodumu milele.