Maisha ya kifahari wanavyoishi watoto wa bilionea Abramovich

LONDON, ENGLAND. VITA ya Russia na Ukraine inamsukuma bilionea Roman Abramovich kwenye kuipoteza klabu yake ya Chelsea baada ya serikali ya Uingereza kushikilia mali za tajiri huyo wa Russia kutokana na kitendo chake cha kumuunga mkono Rais Vladimir Putin.
Kitendo hicho kinamfanya bilionea Abramovich mwenye umri wa miaka 55 kulazimika kuipiga bei klabu yake ya Chelsea kutokana na kukumbana na kibano cha kiuchumi huko Uingereza.
Abramovich, mwenyewe alipanga kuiuza Chelsea kwa Pauni 3 bilioni, lakini serikali ya Uingereza inataka asipate pesa yoyote kwenye mauzo hayo kwa hofu kwamba anaweza kutumia kiasi hicho kwenye kumpa sapoti Putin kwenye kutekeleza jambo lake la uvamizi wa kivita Ukraine.
Abramovich, ambaye alizaliwa Saratov, ni mmoja kati ya mabilionea wengi wa Russia ambao wamekuwa wakisapoti serikali ya nchi hiyo, kitu ambacho kwa sasa wamekumbana na vikwazo vingi vya kiuchumi kutokana na ushirika wao kwa Putin.
Kuikosa pesa kwenye mauzo ya Chelsea inaweza kumtikisa kidogo, licha ya bilionea huyo kuripotiwa kuwa na utajiri unaofikia Pauni 9.3 bilioni (Dola 12.3 bilioni) kitu ambacho kinaelezwa kinaweza kuwaathiri watoto wake saba ambao wamekuwa wakiishi maisha ya kifahari.
Je, watoto wa Abramovich ni kina nani? Wanafanya nini na maisha yao yakoje? Hawa hapa warithi wa mali za bilionea huyo wa Russia.
Anna Abramovich, 30
Mhitimu wa shahaha ya falsafa kwenye Chuo Kikuu cha Columbia, mrembo Anna ndiye mtoto wa kwanza wa bilionea Abramovich katika ndoa yake ya pili kwa mrembo Irina, ambaye waliachana mwaka 2007 baada ya miaka 11 ya kuwa pamoja.
Mrembo Anna alikuwa gumzo kwenye vyombo vya habari baada ya kuchumbiwa na kijana Nikolai Lazarev wakati binti huyo wa Abramovic alipofikisha miaka 18 tu mwaka 2010, wakati huo bado anasoma na shule alikuwa akipelekwa kwa helikopta na wakati mwingine na dereva maalumu katika gari la kifahari.
Abramovich hakupenda binti yake kuchumbiwa kwenye umri huo na wawili hao, Anna na Lazarev waliachana kabla hata kuoana. Baadaye, binti huyo alionekana akila bata tu na kijana Calum Best. Kwa sasa ana umri wa miaka 30 na anaishi jijini New York, Marekani.
Arkadiy Abramovich, 28
Arkadiy alikuwa mtoto wa kwanza wa kiume wa Abramovich na ndiye anayeripotiwa kuwa msimamizi wa mali za baba yake.
Kama ilivyo kwa Anna, Arkadiy ni mtoto wa Roman na mkewe Irina Malandina, mwenye miaka 55, amekuwa na mafanikio yake mwenyewe mbali na utajiri wa baba yake.
Ndiye mwanzilishi na mmiliki wa ARA Capital, inayosimamia biashara ya mtandaoni na kampuni ya mafuta na gesi ya Gazprom Neft. Mara kadhaa amekuwa akionekana Stamford Bridge kwenye mechi za Chelsea. Huko Arkadiy alikuwa na mpango wa kumiliki klabu ya soka na iliripotiwa kuweka ofa ya kununua klabu ya CSKA Moscow, akashindwa.
Ilielezwa pia kutaka kuinunua klabu ya Denmark ya FC Copenhagen.
Sofia Abramovich, 27
Huyu anatajwa kuwa mpenda bata zaidi ya wengine wote kwenye familia hiyo ya bilionea Abramovich.
Mrembo, Sofia amekuwa maarufu pia kwenye mitandao ya kijamii, akipenda kutuma picha zake akionyesha umbo lake kwenye mtandao wa Instagram na amekuwa hodari kwenye matumizi kwa kadri anavyoweza.
Wakati anatimiza umri wa miaka 18, kwenye sherehe ya kufurahia siku hiyo, alifanya mambo makubwa ikiwamo bendi ya muziki wa pop ya McBusted kufanya shoo na ilifanyika kwenye klabu moja ya starehe za usiku huko Stamford Bridge.
Mara kadhaa amekuwa akifanya starehe na marafiki zake wakiwamo watoto wa David Beckham, ambapo siku za karibuni walikuwa zao huko Maldives kwenye hoteli moja ya One & Only Reethi Rah, ambayo kwa usiku mmoja gharama yake ya kulala hapo ni Pauni 3,000.
Sofia ni mhitimu wa shahada ya Utawala na Masoko kwenye Chuo Kikuu cha Royal Holloway. Sofia, 27, ana farasi wake watatu, wanaoitwa Dora, Billy Fraulein na Zanzibar.
Arina Abramovich, 21
Binti mwingine matata kabisa wa bilionea Abramovich. Arina mara kadhaa alionekana akishiriki kwenye mashindano ya farasi akiwa na farasi wake anayefahamika kwa jina la Pringle.
Bilionea Abramovich aliripotiwa kumnunua farasi huyo kwa Pauni 50,000 na aliwahi kushinda zawadi kweye maonyesha ya kimataifa ya farasi huko Olympia, Desemba 2013.
Mrembo Arina aliwahi kuripotiwa kuwa na mpango wa kuhamia Australia kwenda kujiunga na taasis ya elimu ya masuala ya wanyama na mazingira.
Ilya Abramovich, 19
Mtoto wa pili wa kiume wa bilionea Abramovich. Ilya ni mtoto wa mwisho kwa mrembo Irina na Abramovich kabla ya ndoa yake kufika tamati mwaka 2007.
Kuhusu Ilya, taarifa zake hazifahamiki sana, ambapo mtoto huyo alidaiwa kwamba ishu zake za masomo ziliingiliana na janga la virusi vya corona.
Kwa sasa haifahamiki kuhusu masuala yake ya elimu ya chuo ni wapi anasoma, wakati huu baba yake akiwa kwenye sakata la kibano cha kiuchumi huko Uingereza na kulazimika kuipiga bei Chlsea.
Hata hivyo, ni miongoni mwa watoto wanaofurahia maisha kutoka kwenye familia ya baba mwenye pesa nyingi na za kutosha.
Aaron, 12, na Leah Lou Abramovich, 8
Mtoto wa sita na saba wa bilionea Abramovich, Aaron, 12 na Leah Lou, 8 wote walizaliwa Manhattan, New York.
Bilionea Abramovich mara kwa mara amekuwa akitembelea kwenda kuwaona watoto wake hasa kutokana na kuwa na uhusiano mzuri na mrembo, Dasha.
Watoto hao walizaliwa kwenye ndoa ya tatu ya bilionea Abramovich na mrembo mwanamitindo na msanii, mrembo Dasha Zhukova, ambapo ndoa hiyo ilifika tamati pia mwaka 2017.
Aaron kuna wakati alionekana akiwa na jezi ya Chelsea iliyokuwa na jina la Alvaro Morata mgongoni.
Wakati huo huo, Leah Lou, mwenye umri wa miaka minane, anaishi na baba yake huko Big Apple na ameandikishwa kwenye shule ya kitajiri katika jiji hilo.