MAONO: Kuna ngumi nilipigwa, nikaona ‘mvua’ ulingoni

Muktasari:
- Maono Ally Daudi ambaye ni mmoja kati vijana waliowahi kujaribu katika uvuvi kama ilivyo desturi ya vijana wengi wa Bagamoyo, akili na mapenzi yake yalikuwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa.
LICHA ya kuonekana mmoja kati ya vijana wapole kutoka katika mitaa ya Bagamoyo mjini, eneo maarufu zaidi kama mji wa kale wa kihostori huku vijana wake wengi wakijihusisha na shughuli za uvuvi na wengine wakiwa ‘Beach Boy’ wakiwa na mipango kupata wadada wa Kizungu ili kwenda kuishi Ulaya, lakini ni mkali wa ulingo.
Maono Ally Daudi ambaye ni mmoja kati vijana waliowahi kujaribu katika uvuvi kama ilivyo desturi ya vijana wengi wa Bagamoyo, akili na mapenzi yake yalikuwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa.
Mapenzi kwa mchezo huo yalimfanya Maono kuwa bondia wa kwanza kutoka Tanzania kushinda mkanda wa ubingwa wa Baraza la Ngumi Duniani (WBC) maarufu kama WBC Youth Silver kwa kumchapa Luka Pupek nchini Afrika Kusini kwa knockout ya raundi ya pili katika pambano la raundi 10 lililopigwa 2018.
Ushindi huo ulimfanya aliyekuwa wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kumualika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupeleka mkanda wake wa ubingwa akiwa na mabondia wengine waliokuwa wametoka kushinda mapambano ya ubingwa nchini.
Maono ana rekodi ya kupanda ulingoni katika mapambano 27 akiwa amefanikiwa kushinda 17 kati ya hayo 11 ni kwa knockout, amepigwa mara tisa kati ya hizo tano ni knockout na ametoka sare mara moja.
Bondia huyo wa uzani wa super walter anakamata nafasi ya tatu katika mabondia 30 wa uzani huo nchini wakati duniani akiwa bondia wa 476 katika mabondia 2238, huku uwezo wake wa kushinda kwa knockout ukiwa ni asilimia 68.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na bondia huyo ambaye amefichua licha ya kupitia katika shughuli za uvuvi na ufundi wa pikipiki, lakini mapenzi yake yalikuwa katika mchezo huo tangu alipokuwa mdogo.
“Ukweli kuhusu mchezo wa ngumi nimeanza kuupenda tangu nikiwa kijana mdogo ambapo nilikuwa natoroka nyumbani kwenda kuangalia ngumi hata kama sina pesa. Nilichokuwa nafanya nawahi kufika mapema kisha naomba kuingia sasa kwa udogo wangu walikuwa wakiniruhusu.
“Nilikuwa napenda sana huu mchezo yaani nikiona mtu anapiga ngumi nilikuwa natamani awe kaka yangu, hivyo wakati nipo Bagamoyo ndiyo nikaenda kwa Sharif Muhsin wa Sharif Boxing Gym ndiyo sehemu niliyojifunza ngumi,” anasema Maono.
SWALI: Nini kilitokea ukashindwa kutetea ubingwa wako wa WBC Youth?
JIBU: “Unajua ule ubingwa nilishindwa kutetea kwa sababu baada ya kurudi nao hapa nchini sikuweza kupata promota wa kuweza kuniandalia pambano kwa sababu gharama zilikuwa kubwa sana hadi ukatolewa kwenye rekodi kutokana na WBC walinivua kwa kuwa sikuweza kuutetea.”

SWALI: Lakini mkanda wako ulifika bungeni?
JIBU: “Ni kweli mkanda wangu nilipeleka bungeni kwa sababu ya waziri wetu kwenye michezo wakati ule Dk Mwakyembe (Harrison) alitualika kwa lengo kuonyesha taifa namna mchezo wangu unavyopiga hatua kimataifa na kuipa nchi heshima lakini hakukuwa na kitu kingine.”.
SWALI: Kitu gani cha tofauti unajivunia kwenye ngumi?
JIBU: “Kikubwa ambacho nakiona cha tofauti mwenye kazi ana kazi yaani najivunia kwa sababu kinapatikana kitu cha kuweza kuendesha familia, ukweli namshukuru Mungu. Siwezi kusema nina vikubwa wakati bado naendelea kupambana na bado sijavipata ila namuomba Mungu ili niweze kufikia hivyo vikubwa.”
SWALI: Pambano gani huwezi kulisahau?
JIBU: “Unajua asilimia kubwa mapambano yangu huwa ni magumu. Nakumbuka pambano langu la Ujerumani lilikuwa gumu lakini halijawekwa matokeo yake hadi leo na nilimaliza japo nilipoteza kwa pointi, raundi 12 tena nilicheza na bondia mkubwa ambaye ametoka kupigwa na Chris Eubank jr juzi tu.
“Nakumbuka raundi ya saba nilipigwa ngumi nikaona ulingoni kama kuna mvua ila nilijisemea siyo kweli nitamaliza maana mabondia tukienda Ulaya mara nyingi tunapigwa kwa hofu au unakuta hapa unapigana na bondia mkali zaidi ya uliyepigana naye Ulaya ila tu ukipigwa ngumi kali unaacha. Nashukuru Mungu japo ya kupigwa kwa sababu ya kwao lakini walijua nimefanya kitu gani.”

SWALI: Upi utofaufi wa kushinda nje ya Tanzania?
JIBU: “Uzuri wa ushindi wa nje kwanza unakuwa umewakilisha nchi, lakini pia unakuwa umejenga heshima yako kwa kuweza kuonyesha uwezo mkubwa nje ya mipaka ya nchi tofauti tukicheza hapa.”
SWALI: Kitu gani kimekuhamishia Chanika kutoka Bagamoyo?
JIBU: “Kikubwa nimebadilisha upepo kwa kukaa karibu na mchezo wa ngumi ili niweze kupata mapambano kwa wakati kwa sababu kwa Bagamoyo kwa mwaka najikuta nacheza pambano moja na kawaida bondia ukikaa muda mrefu kuna vitu unapoteza.”
SWALI: Unatamani kukutana na bondia gani mkubwa duniani?
JIBU: “Binafsi nilikuwa na ndoto ya kukutana na Mike Tyson na Evander (Holyfied), lakini nashukuru Mungu nimeweza kukutana na Michael Maidana ambaye nilikutana naye Dubai.
“Nilichokipata kutoka kwa Maidana hata ningekutana na Tyson akiwa na Evander ni hamasa kwa sababu hatukuweza kupata muda wa kuongea chochote.
“Nimekutana na Maidana wakati napigana Dubai, zaidi nilifurahia ikanipa hamasa ya kufanya vizuri ambapo nilishinda kwa technical knockout ya raundi ya pili na hiyo ilitokana na furaha yangu ya kupigana mbele ya Maidana.
“Lakini hata ilivyokuwa kwa Tyson na Evander wao ilikuwa Ujerumani, nilicheza na yule aliyempiga Twaha Kiduku Ujerumani. Kikubwa nilikaza na kupigana kweli kwa sababu sikutaka kuwaangusha rangi nyeusi wenzangu japokuwa kwa sababu ya pambano kuisha kwa pointi wakampa ushindi bondia mwenyeji.”

SWALI: Umewahi kulipwa pesa nyingi kiasi gani?
JIBU: “Binafsi hilo labda kwa mapambano ya nje ya Tanzania lakini hapa ndani sijawahi kulipwa pesa nyingi katika pambano lolote zaidi nikienda nje hata nikilipwa milioni moja kwangu naona nyingi kwa sababu siwezi kuipata kwa mapambano ya ndani.
“Unajua hapa ndani mabondia wakubwa hawawezi kukubali kucheza na bondia ambaye wanaamini mdogo. Unaweza kumtaka bondia mkubwa na yeye akataka hela nyingi au hawataki kabisa hivyo ni ngumu kuweza kupata pesa nyingi.”
SWALI: Una mipango gani katika ngumi?
JIBU: “Nawaomba sana mapromota waniwekee mapambano ya mikanda ya ubingwa, nimechoka kupigana mapambano ya kawaida, hawezekani mikanda ya ubingwa nikapigane nje ya nchi halafu ndani inashindikana.”