MAPIGANO YA MAJOGOO YANAVYOBAMBA DUNIANI

Muktasari:
Zipo sheria na kanuni za mchezo. Kwa mfano jogoo anayeshiriki mashindano anatakiwa awe na umri wa zaidi ya mwaka mmoja na miezi mitatu na uzito usiopungua kilo mbili.
Waswahili wana msemo marufu wa kukebehi watu wanaotoka nje ya miji hasa vijijini. Msemo huu ni ule wa ‘Jogoo wa shamba hawiki mjini’.
Katika msemo huo jogoo hutumika kupeleka ujumbe pale anapotokea kutamba huko alipo, lakini akifika mjini hujikuta amegonga mwamba.
Lakini ukweli ni kwamba tumeshuhudia miaka ya nyuma timu kama ya Kiwanda cha Sukari cha Arusha Chini (Moshi), Tanganyika Planting Company ikiwika Dar es Salaam na miji mengine ya Afrika Mashariki. Hii ilikuwa katika miaka ya 1960 na 1970.

Mseto ya Morogoro ilifanya makubwa Dar es Salaam na kuibuka klabu bingwa ya Tanzania miaka ya mwanzo ya 1980. Kumbukumbu zinaonyesha hata majogoo waliotoka shamba (nje ya Dar es Salaam) ndio waliowika katika timu ya taifa. Ukiachilia simulizi za majogoo katika kandanda yapo mashindano ya majogo wenyewe na katika hili wale waliotoka shamba ndio wakiibuka kidedea.
Huu ni mchezo wa kupiganisha majogoo ambao unapendwa katika nchi nyingi duniani na hata kwetu ambapo majogoo kuchi (asili yake Kutchi, India) ndio wanaotumika katika mapigano haya. Bei za majogoo mahiri ya aina ya kuchi Tanzania na hasa Zanzibar hufika Sh300,000, lakini katika baadhi ya nchi ambapo watu wengi hucheza kamari katika mchezo wa kupiganisha majogoo bei ya jogoo mahiri wa kupigana huzidi Sh6 milioni.
Jogoo mmoja kule Thailand miezi michache iliyopita akiwa na umri wa miezi 16 aliweka rekodi ya bei ya Sh33 milioni.
Kabla ya hapo jogoo aliyeuzwa kwa bei kubwa zaidi ni kule Irak Sh16.5 milioni. Mchezo wa kupiganisha majogoo unavutia wengi katika nchi za Asia, Ufilipino, Amerika Kusini na Visiwa vya Carribbean.
Katika baadhi ya nchi vipo viwanja maalumu vya mchezo huo. Kwa mfano vipo viwanja vinavyoingiza watu 20,000 katika visiwa vya Ufilipino na maelfu hufika kuangalia majogoo maarufu yanapopambana.
Ufilipino na Dominica ni nchi zinazosifika kuwa na mbegu nzuri za majogoo yanayopigana kwa umahiri na hata kuua majogoo pinzani. Huko Puetro Rico mchezo huu unatambulika kama wa taifa na unatoa ajira kwa watu 27,000. Katika nchi zenye mashabiki vipo vyama vya wapiganishaji majogoo na hufanyika mashindano, ikiwa ni pamoja na ya kimataifa. Makao makuu ya ya mchezo huo ni Kabul nchini Afghanistan.
Zipo sheria na kanuni za mchezo. Kwa mfano jogoo anayeshiriki mashindano anatakiwa awe na umri wa zaidi ya mwaka mmoja na miezi mitatu na uzito usiopungua kilo mbili.
Mashindano hufanyika kwa viwango vya uzito kama ulivyo katika ndondi na ipo ya mizunguko mitatu mitatu na tisa na majogoo huwa yamepata mafunzo ya kuelewa yanatakiwa yapigane mizunguko mingapi.
Mashindano haya yapo ya mtindo wa ligi na mtoano na kwa kawaida huwa ya nusu saa, lakini mara nyingi humalizika baaada ya dakika tano au 10. Yapo majogoo ambayo kabla ya kushiriki mashindano huonyeshwa videoni na wanaoyamiliki kuelewa mbinu za majogoo yatakaopambana nao. Katika baadhi ya nchi mapigano haya hutangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni. Utasikia Jogoo Santa ananyemelea pale, hatua ya kwanza …ya pili, anaruka na anapiga teke mpinzani huku akimdonoa.
Vilevile jogoo anaweza kuvalishwa visu au vijembe vinavyokubalika katika kucha zake, lakini visiwe vimepakwa sumu au dawa yoyote inayolevya au kuua.
Katika mchezo huo majogoo mawili huachiwa yapigane mpaka moja life au liwe hoi na haliwezi kuendelea kupigana au mwenyewe aseme kipigo lilichopata jogoo lake kimetosha na kulitoa kwenye mashindano.
Ni kawaida kuona mashabiki ambao jogoo waliyempenda amepigwa kuwaona wanalilia kana kwamba wamepoteza mwanafamilia. Wakati wa mapumziko jogoo huangaliwa kama ameumia na kutibiwa na ni kawaida kumuona mmiliki anazungumza kwa kunong’ona na jogoo wake, kama vile anampa ushauri wa kupigana vizuri.
Sheria za mchezo huu ni kwa jogoo kupigana sio zaidi ya mara mbili kwa mwezi, lakini mara nyingi hukiukwa. Mchezo wa kupiganisha majogoo ni moja ya michezo mikongwe na ulianza karibu miaka 6,000 iliyopita kule Uajemi (Iran). Baadaye ukasambaa hadi India, China, Ugiriki na Uturuki. Katika miaka ya nyuma mabaharia wa Ufilipino walichukua majogoo melini kupiganisha ikiwa sehemu ya burudani (kumbuka zama zile kulikuwa hakuna sinema, televisheni wala video).
Katika baadhi ya nchi mchezo wa kupiganisha majogoo umeingizwa katika Katiba. Lakini zipo nchi zilizoupiga marufuku kuwa unakiuka haki za wanyama kuishi kwa raha na furaha.
Lakini mashabiki wa mchezo huo wanasema ukatili mkubwa kwa hawa kuku hufanywa na walaji ambao huwaua kwa maelfu kila siku ili kuwala.
Wapo mashabiki wanaopenda majogoo zaidi ya wake au watoto wao. Watu hawa huwapeleka majogoo wao saluni maalumu kuogeshwa na kupulizwa dawa, kutengenezwa kucha na kuchuliwa misuli.
Mchezo wa kupiganisha majogoo ni maarufu katika ukanda wa Pwani wa Tanzania, Bara na Visiwani. Jogoo wanaotumika sana kwa mapigano haya ni wa aina ya kuchi. Ipo hadithi maarufu Zanzibar ya mzee mmoja kushuhudia mwanawe aliyepanda baiskeli akiwa amebeba jogoo anayetumika kupiganishwa akigongwa na mkokoteni na kuanguka. Yule mzee alikimbilia ilipotokea ajali. Badala ya kuangalia hai ya mwanawe aliyekuwa amelala chini kwanza alimshughulikia jogoo wake.
Baada ya kuona jogoo hajaumia ndipo alipogeuka kujua hali ya mwanawe. Tangu siku ile akageuzwa jina na kuitwa Jogoo. Kwa kweli dunia hii ina mambo katika kila fani, ikiwa pamoja na ya michezo.
Kijiwe cha Salim Said Salim