Mastraika jifunzeni kwa kina Suarez na wenzake
Muktasari:
Sikatai, straika unaweza kuwa na hamu ya kuona filamu ila usipoteze muda wako mrefu katika filamu hizo.
WAKATI naingia mitamboni, Liverpool walikuwa kileleni mwa Ligi Kuu England baada ya kuipiku Arsenal.
Ni muda mrefu sana Liverpool wameweza kuandikisha matokeo kama haya kwa miaka za hivi karibuni. Kwa kusema kweli Liverpool wanastahili kuwa mahala walipo katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Hakuna msimu England ambao ligi itakuwa tamu kuliko msimu huu. Arsenal, Liverpool, Man City na Chelsea wote kufikia sasa wana nafasi nzuri za kushinda ligi.
Jambo la kufurahisha ni kuwa miamba wa soka Manchester United nao wameanza kurudisha makali yao pole pole. Muda si mrefu ndugu zangu msishangae wakipanda juu ya meza.
Nikirejea kwa Luis Suarez straika anayetisha duniani kwa wakati huu, nampa pongezi kwa sababu ligi inapokaribia kumalizika mzunguko wa kwanza ameshatia nyavuni mabao 19 na bado mechi kama tatu nne hivi mzunguko wa kwanza kukamilika.
Suarez amekuwa mwiba kwa timu karibu zote na ikumbukwe alirejea kusakata ngoma baada ya kutocheza mechi tano za kwanza za ligi msimu huu. Alikuwa anatumikia kifungo alichopewa baada ya kumtusi Patrice Evra, mchezaji wa Manchester United, matusi yenye mwelekeo wa ubaguzi wa rangi.
Jambo linalonifurahisha na Suarez ni ukamilifu wake uwanjani. Ni mchezaji ambaye yupo kila mahali uwanjani na punde tu anapopata mpira kichwa kipo juu kuangalia langoni. Mastraika wetu sijui hasa kama wao huangalia kanda zake? Nashangaa kwa mfano nchini kwetu ukikutana na wachezaji hasa mastraika ukimuuliza bosi wangu, kanda gani wewe huangalia anakuambia yeye hushinda akiangalia sinema za Hollywood, nyimbo za Rihanna na nyinginezo.
Cha kushangaza hana hata kanda moja ya wanasoka bora duniani, anakufanya ubaki ukijiuliza ndio maana tuna uhaba wa mastraika katika ukanda wetu.
Wakati nacheza mpira, kanda zangu nyingi zilikuwa za soka. Si soka tu bali zaidi ilikuwa ni kanda za washambuliaji hodari kina Ruud Van Nielstroy, Ronaldo de Lima, Samuel Eto’o, Rashid Yekini, Thierry Henry, Jurgen Klinsman, Frank Rijkaard, Eric Cantona, Ronaldinho na wengineo.
Kwa kusema ukweli hao ndio wachezaji walionijenga katika kuwa straika. Kila wakati nilikuwa nanunua kanda zao na kuangalia wanavyokimbia ndani ya eneo la hatari na nini wanachofanya wakati wanapopata mpira mahala popote uwanjani ama nini na wapi wanapokimbilia wakati mchezaji mwenzake anapokuwa na mpira.
Kuna kanda huuzwa mitaani za goli za msimu fulani za timu za Manchester United, Chelsea, Arsenal, Liverpool, Man City, Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich na nyinginezo.
Hizi ni kanda ambazo zinaweza kukusaidia kiuchezaji hasa straika kuangalia na kujifunza mengi kuhusu ushambuliaji. Fani ya uimbaji ina wenyewe, fani ya uigizaji filamu ina wenyewe, fani ya unenguaji viuno ina wenyewe.
Sikatai, straika unaweza kuwa na hamu ya kuona filamu ila usipoteze muda wako mrefu katika filamu hizo.
Mastraika wa zama hizi utampa nafasi tano katika mechi, atatumia moja pekee. Unashangaa na kujiuliza maswali mengi. Tatizo lipo wapi? Akifunga bao moja mechi ya leo, bao lingine litakuja baada ya mechi tano au sita hivi. Siku hizi kuhangaika kutafuta goli imekuwa ni haba. Uchunguzi wangu wa kina ni kwamba wengi wao baada ya mazoezi mambo ya soka wanayatia mvunguni mwa kitanda. Nimekuwa mfungaji bora kwa nchi zote nimesakata soka na si tu kwa kipaji nilichopewa na Mungu bali ni kwa kujitolea kutafuta kanda kama hizo nilizowatajia hapo awali. Muda mrefu nakaa chini kuziangalia.
Nikiona sikupata hilo goli sawasawa narudisha nyuma na kuweka ‘slow motion’. Cha pili ni kuwasoma mabeki. Ilikuwa inanichukua dakika moja tu kumsoma beki yeyote na mlinda lango anavyocheza na anavyosimama langoni na anapodaka.
Mastraika wa kizazi hiki mnaye Suarez, Rooney, Messi, Cristiano Ronaldo, Van Persie, Ramsey, Dzeko, Aguero, Ibrahimovic, Torres, Tevez na wengineo wa kuwaiga.
Hawa ni baadhi ya mstraika ambao kwa nafasi tatu pekee akipata atatia mpira nyavuni mara mbili.
Msimu huu Suarez ameamsha ulimwengu, amefunga mabao mazuri, ni raha kumuangalia anapocheza na itakuwa vigumu kwa straika yeyote kumpiku kwa kiatu cha dhahabu msimu huu.
Shida kubwa ya mastraika wetu ni kuwa hawaangalii kipa wanapokuwa uwanjani na mara mpira unapomfikia anakosa maarifa ya kumtungua kipa.
Kenya naweza kusema John Baraza na Dennis Oliech watakapostaafu soka hivi karibuni, labda Allan Wanga ndiye atakayechukua majukumu hayo. Angalia ukomavu walio nao Baraza na Oliech hata hivyo umri umewakimbiza kiasi.Tanzania nashangaa John Boko, Jerry Tegete na Mwaikimba alipotelea wapi, hata hivyo namuona Mbwana Samata anajaribu kuvivaa viatu vya mastraika kamili Bongo.
Straika mzuri kwa kweli ni yule ambaye kila msimu yupo tatu bora miongoni mwa wafungaji. Angalia msimu uliopita Suarez kabla ya kufungiwa alikuwa anamfukuzia Van Persie na Van Persie ashukuru, kifungo cha Suarez kilimsaidia kuwa mfungaji bora. Hata hivyo amerejea na makali yake msimu huu. Kwa kasi yake anaweza kufikisha zaidi ya mabao 30 akisaidiana na Danny Sturridge ingawa ni majeruhi.
Straika wa ukweli ni yule anayeweza piga bao akiwa mahala popote uwanjani. Na anafunga kila wakati. Kufunga si ishu kubwa kwake. Ishu kubwa kwake ni kukosa pasi sahihi kutoka kwa viungo wake. Suarez msimu huu na uliopita amenifurahisha kwa ustadi na ukamilifu alionao.
Ni msumbufu uwanjani na usumbufu wake hadi wa kuwauma mabeki masikio na mikono unamfanya kuogopwa na walinzi wa timu tofauti.
Straika mwengine ni Kun Aguero wa Man City. Na umbo lake dogo analitumia vyema. Ana kasi ya kutisha, nguvu alizonazo akiwa na mpira zinamuwezesha kuwa nambari moja Man City.
Mastraika wenzangu tusitake kuwa wasanii na fani yetu ni soka. Muuza chuma hawezi kuuza mboga. Mcheza Reggae hawezi kucheza Lingala na kumbuka wote ni wanamuziki. Itakuwaje unataka kujua sana ya Hollywood kuliko ya soka?