MIGWEDE: Vipigo, kufukuzwa chanzo cha ubondia

Muktasari:
- Katika kada ya mchezo wa ngumi za kulipwa, baadhi ya mabondia mashuhuri waliowahi kuweka mizizi katika eneo hilo ni Mada Maugo, Dullah Mbabe pamoja na mkongwe, Said Mbelwa.
CHANIKA jijini Dar es Salaam ni moja ya maeneo yenye watu wengi waliokuwa wakiishi katikati ya jiji hilo wakiwamo wanamichezo mbalimbali.
Katika kada ya mchezo wa ngumi za kulipwa, baadhi ya mabondia mashuhuri waliowahi kuweka mizizi katika eneo hilo ni Mada Maugo, Dullah Mbabe pamoja na mkongwe, Said Mbelwa.
Ni ngumu kuzungumzia mchezo wa ngumi za kulipwa katika kitongoji cha Chanika bila kutaja majina ya mabondia hao na wamekuwa nembo na wawakilishi wa eneo hilo na wana mashabiki wengi.
Uwepo wao umekuwa chachu kubwa ya kutengeneza na kuvuta mabondia wapya chipukizi wengi, akiwemo kijana Ramadhani Yusuph Mbegu 'Rama Migwede'.

Migwede ni mmoja wa mabondia wenye nidhamu kubwa nje na ndani ya ulingo aliyepanda ulingoni mara ya kwanza Desemba 24, 2016.
Ana rekodi ya kucheza mapambano 23, akishinda 16, huku 12 kwa knockout na kupigwa matano ambayo kati ya hayo matatu ni kwa knockout na ametoka sare mawili
Kwa sasa anakamata nafasi ya saba katika mabondia 27 wa uzani wa super walter wakati duniani akiwa nafasi ya 739 kati ya mabondia 2202 kwa uzani huo.
Bondia huyo aliyeishia kidato cha pili anasema alishindwa kuendelea na masomo kutokana na ugumu wa maisha baada ya baba yake kufariki dunia.
"Ukweli safari yangu ya maisha ya shule nimeishia kidato cha pili na nilishindwa kuendelea kwa sababu ya ugumu wa maisha ndani ya familia yetu, baada ya baba kufariki mambo hayakuwa mazuri upande wetu.
"Mama hakuwa na uwezo wa kutusomesha maana nakumbuka ilikuwa nalazimika kwenda kufanya vibarua vya saidia fundi kwenye ujenzi ndiyo niende shule au familia iweze kupata chakula.
"Kutokana na hali hiyo, nikajikuta naachana na shule nikafungua mabanda ya kuuza chips huku Chanika na biashara upande wangu ilikuwa nzuri, lakini ikaja ikayumba msingi ukafa, madeni yakawa mengi nikaamua kuachana na hayo mambo ya biashara.

Alichoka kuonewa akaingia ulingoni
"Zamani sikuwa kabisa na wazo kama itatokea wakati kama nitakuwa bondia lakini kilichosababisha niwe bondia ni tabia za kuonewa na watu waliokuwa wanaona wanajiweza.
"Unajua mimi mitaa ndiyo imenilea kwa hiyo nilikuwa kijana wa kijiweni kama vijana wengine sasa ukiwa kijiweni ukiwa mnyonge utatumwa na kila mtu, ukikataa unapigwa na kufukuzwa.
"Nimekutana na hali hiyo mara nyingi na wakati huo Said Mbelwa kwa huku Chanika alikuwa maarufu kwenye ngumi na katika mashabiki wake naweza kusema nilikuwa namba moja kwa sababu sikuwa nakosa kwenye mapambano yake.
"Kutokana na matendo ya kuonewa sana ikabidi niongee na Said Mbelwa ambaye kwangu ni kaka ingawa nilikuwa na hofu itakuwaje lakini lengo ni kujilinda na watesi wa mtaani.
"Nashukuru, Mbelwa anikubalia nikaanza mazoezi chini yake yeye akiwa kama mwalimu wangu wa kwanza kwenye ngumi za kulipwa hiyo ilikuwa ni mwaka 2009.
"Nakumbuka pambano langu la kwanza nilipigana na bondia wa kuitwa Said Ngumijiwe ambaye ndiyo alikuwa mtemi wa Chanika halafu nikapewa nipigane naye pambano la raundi nne.

"Nashukuru nilimpiga kwa pointi, ikabidi liandaliwe pambano la marudiano ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa Simon Sirro, unaitwa Butiama, nikampiga tena.
"Baada ya hilo pambano nikaanza kupata jina hapa Chanika na hata wale ambao walikuwa wakinionea walianza kuniogopa maana nilitamani wawe wananikosea lakini walivyokuwa wanajua nilichomfanya mtemi wao wakawa wananiogopa na uonevu ukaisha hivyo, nikaendelea na ngumi.
"Lakini kwa upande mwingine familia yangu hasa mama hakupenda kabisa nicheze ngumi kwa sababu wakati mwengine najikuta narudi kutoka mazoezini, jicho limefumba kabisa akawa ananikataza ila niliendea na juhudi za mazoezi.
"Kuhusu kufanikiwa naweza kusema bado sijafanikiwa lakini naamini ipo siku nitafanikiwa kutokana na juhudi ambazo nipo nazo pamoja na malengo."
Mapambano haya hatayasahau
"Unajua mapambano mengi kwangu, magumu yapo mawili, nakumbuka moja nilienda kupigana Tanga na bondia anaitwa Adamu Lazaro, nilipoteza kutokana na hali ya hofu niliyokutana nayo.
"Nakumbuka baada ya kupanda ulingoni, vilimwagwa vitu ambavyo naweza kusema ushirikina kwa sababu ulikuwa mchele na mtama ambao ulimwaga kwenye kona yangu, vikanitoa mchezoni nikapigwa raundi ya tatu.
"Pambano lingine nilicheza huku Chanika na Adam Ngange ambaye kwangu ni kaka maana amenizidi umri ila nilimtangulia kwenye ngumi japo mwalimu wetu wa kwanza alikuwa mmoja, nikapoteza pia."

Umewahi kupigwa ngumi,ukatamani kuacha?
"Hapana, kiukweli sijawahi kukutana na hali hiyo au kupigwa ngumi ya kunikatisha tamaa, haijawahi kutokea ila changamoto kubwa kwangu ni mazoezi.
"Unajua mazoezi hasa wakati wa kufanya sparing unaweza kupigana hadi na watu saba au nane ambao wamekuzunguka na kila mmoja anakuwa na nguvu yake, lakini kwenye pambano ni rahisi kwa sababu ya kupigana na mtu mmoja.
Huu ndo msosi wake
"Kwanza napenda sana kula wali na ndizi kwa maana zile ambazo zimeiva na ugali mara moja moja na huwa napendelea kula asubuhi.
"Ugali mara nyingi naanzia kula nusu ingawa naweza kubakisha kitonge kidogo na mboga yake ni kuku wa kienyeji.
"Nashukuru Mungu nawafuga mwenyewe na kupika naweza, hivyo sioni shida hasa wakati nikiwa nimeweka kambi na familia ipo mbali, naweza kumaliza kuku mzima ila kutokana na mambo ya bajeti mmoja namla siku moja peke yangu.
Pesa nyingi alizolipwa
"Kiukweli pesa nyingi niliyoipata kwenye ngumi ni 3.5 milioni na nilienda kupigana Dubai, kwa upande wa ndani niliwahi kulipwa Sh1.5 milioni."
Kuhusu ndoa yake
"Nashukuru nina mke na watoto wawili ambao wote ni wa kike ambao sitegemi kuona wanakuja kuwa mabondia labda kama nitapata mtoto wa kiume, ingawa kwa sasa najitahidi waweze kupata elimu zote mbili, maana nataka wasome."
Ni fundi wa marumaru
"Sasa hivi nimekuwa fundi, unajua baada ya kuacha kuuza chips nikawa najifunza na ufundi wa kuweka marumaru pamoja na kufanya skimi na ufungaji wa bodi kwenye majumba hivyo upande mwengine nje ya ngumi ni fundi."