Prime
Munthari: Najutia sana kukatisha soka la Nsa Job

Muktasari:
- “Nilianza kufanya tukio ambalo nilikatisha soka la mchezaji mwenzangu baada ya kumvunja mguu. Sio mwingine ni Nsa Job kipindi hicho akikipiga Coastal Union na mimi nikiwa JKT Ruvu ambayo kwa sasa ni JKT Tanzania. Niligongana naye akavunjika mguu, hilo tukio sitakaa nikalisahau.
“Nina matukio mawili makubwa ambayo licha ya soka kuniendesha linavyotaka lakini na mimi naendeshwa na hayo matukio kutokana na kutokuwa mazuri kwangu na hayawezi kufutika kwenye maisha yangu ya soka.
“Nilianza kufanya tukio ambalo nilikatisha soka la mchezaji mwenzangu baada ya kumvunja mguu. Sio mwingine ni Nsa Job kipindi hicho akikipiga Coastal Union na mimi nikiwa JKT Ruvu ambayo kwa sasa ni JKT Tanzania. Niligongana naye akavunjika mguu, hilo tukio sitakaa nikalisahau.
“Kabla hilo halijafutika nilikutana na changamoto kama hiyo tena dhidi ya Edward Songo tukio ambalo likaamsha hisia mbaya za miaka iliyopita,” anasema kipa wa Mashujaa FC, Patrick Munthary ambaye amefanya mahojiano na Mwanaspoti akizungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna alivyokuwa karibu na wachezaji hao baada ya kuwaumiza.
Anasema baada ya tukio la Songo kutokea, “unajua JKT Tanzania ndio timu ambayo nimekaa muda mrefu kuliko timu nyingine. Pale ni nyumbani hivyo siku ileile baada ya tukio nilifunga safari ya kwenda hospitali kwa ajili ya kumjulia hali, nilimuomba radhi kwa sababu sikudhamiria kufanya vile,” anasema.
“Songo ni mtu wangu wa karibu na hata tukiwa mapumziko lazima tutembeleane, hivyo nilichukua jukumu la kumjulia hali, lakini pia nilizungumza na daktari wa timu na viongozi kwa ajili ya kuwaomba radhi kwani sikukusudia.”
Munthary ambaye kwa mujibu wa rekodi za Bodi la Ligi (TPLB) ana umri wa miaka 31, anasema kwa upande wa Job mwanzo walikuwa wanawasiliana, lakini hivi sasa hana namba yake kwani alishapoteza mawasiliano.
“Hapo awali nilikuwa nazungumza naye, lakini kwa sasa sizungumzi naye kwa sababu nilipotezaga namba yake na yeye kwa sasa maisha yake ni China,” anasema Munthary aliyewahi kukipiga Kibangu Rangers, Simba B, JKT Ruvu, JKT Tanzania, Transit Camp na sasa Mashujaa FC.
MILIONI MBILI YA SIMBA IMEMPA BODA
Nyota wengi wa soka wanasimulia kuwa mwanzo wao kwenye maisha ya soka hasa kwenye fedha za usajili si mzuri, lakini sasa wanafurahia maisha ya mpira na kuuchukulia kuwa ajira kama anavyosema Munthary kwamba fedha zake za kwanza ya soka aliambulia Sh2 milioni kutoka Simba.
“Fedha zangu za kwanza za usajili ilikuwa ni milioni moja. Niliipata baada ya kusajiliwa na kikosi cha vijana cha Simba (Simba B), nakumbuka nilitumia kununua bodaboda kwa ajili ya biashara.

“Sikuishia hapo tu kwani licha ya kuamua kuwekeza nguvu kwenye soka, nilikuwa najiendeleza kielimu, hivyo baada ya kuwekeza kwenye biashara fedha nyingine nilinunua vitabu ili kujiendeleza kimasomo nikiwa nacheza,” anasema Munthary ambaye amepita kwenye timu tano hadi sasa akiitumikia Mashujaa.
KUSHAMBULIA HADI KUDAKA
Sio kila anayecheza nafasi aliyopo sasa kwenye kikosi chake alianzia hapo kwani kuna wengine wameamua kubadilisha nafasi kutokana na makocha wanavyowaona wanafiti kucheza nafasi walizopo sasa kama anavyothibitisha Munthary.
“Nilipokuwa najitafuta nilianza kucheza eneo la ushambuliaji ambalo ndilo nilikuwa nalipenda, lakini wachezaji wenzangu na mashabiki walikuwa wanapenda nikae langoni,” anasema na kuongeza:

“Licha ya mashabiki na wachezaji wenzangu kutamani niwe nakaa langoni sikufanya uamuzi huo kwa mapendekezo yao hadi hapo kocha mmoja aliponibadili nafasi ambayo ndio naicheza hadi sasa.”
YAW BERKO, DIDA WALIMVUTA
Licha ya kupenda kucheza eneo la ushambuliaji na baadaye kubadilishwa nafasi akiwa kipa, Munthary anasema nyota aliokuwa anawatazama zaidi kipindi hicho ni Yaw Berko kutoka Ghana, Deogratus Munishi ‘Dida’, hayati Abel Dhaira na Hussein Sharrif ‘Casillas’.
“Ni makipa wengi bora wamepita na walikuwa wananivutia kwa aina yao ya uchezaji, miongoni mwao ni hao niliowataja nilikuwa natumia wakati wangu kuwatazama ili niweze kufanya kazi yangu kwa ubora,” anasema.

“Kuna wengine baadhi yao nilipata nafasi ya kuzungumza nao nikiwaambia napenda aina ya uchezaji wao na walinipa moyo kuwa mimi pia nina kipaji ninaweza kufika mbali nikiwekeza juhudi na kutumia vizuri kimo nilicho nacho.”
Munthary anasema kipa bora ni yule ambaye anakubali kujifunza kutoka kwa aliyemtangulia na pia hata aliyemzidi uwezo kitu ambacho amekuwa akikifanya ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya ushindani.
BAO LA MIQUISSONE
Licha ya kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Luis Miquissone kuondoka nchini akiwa ameacha rekodi kibao ndani ya timu hiyo, Munthary anamtaja kuwa ndiye mchezaji aliyekuwa anampa wakati mgumu kipindi hicho akikipiga JKT Tanzania. “Ni washambuliaji wengi wamekuwa hatari langoni kwangu, lakini Miquissone ni habari nyingine. Alikuwa mchezaji msumbufu ndani ya boksi ambaye alikuwa anatumia akili,” anasema.
“Nakumbuka nikiwa JKT Tanzania alinifunga bao ambalo naweza kulitaja kuwa ndilo bao bora, mchezo ulichezwa uwanja wa Jamhuri - Dodoma ambao tuliutumia kama uwanja wa nyumbani.”
MASHUTI YA AZIZ KI
Kipa Aishi Manula anamfahamu vizuri Stephane Aziz Ki kutokana na kumtungua mara nyingi zaidi akiwa ligi ya Tanzania, lakini pia akiwa na timu yake ya Asec Mimosas sio huyo tu kumbe Munthary pia kapitia shuruba hiyo kama anavyothibitisha. “Kuna nyota wengi wanafanya vizuri wakijaribu mipira ya mbali kwa kupiga mashuti makali, lakini Aziz Ki ndiye mchezaji hatari zaidi japo sasa kazi yake imepungua, lakini ukitaka kulaumiwa fanya masihara na mashuri ya mchezaji huyo.

“Na siku zote tunaolaumiwa ni sisi makipa bila kujiuliza kuwa nini kinatufanya tunashindwa kuokoa mashuti ya aina kama hizo ninachotaka kuzungumza ni kwamba kabla ya kutulaumu wanatakiwa kumheshimu na mpigaji pia,” anasema.
Munthary anasema Aziz Ki tangu amejiunga na Ligi Kuu Bara amekuwa mchezaji hatari wa mipira ya kutenga na pia mabao ya nje ya 18 kutokana na ubora wa aina ya upigaji alionao huku akidai kuwa kwa siku za karibuni amepungua makali tofauti na mwanzo ambapo alikuwa anapeleka lawama kwa makipa wengi.
MWANA MAHESABU
Kama ilivyo kwa wachezaji wa ligi za wenzetu ikiwa Ligi Kuu England (EPL), basi na Ligi Kuu Bara ina mastaa wasomi ambao waliamua kuachana na fani walizosomea na kujikita katika soka.
Miongoni mwa wachezaji wasomi wa EPL walioweka kando taaluma zao ni pamoja aliyewahi kuwa kiungo wa Manchester United, Juan Mata ambaye alianza kuwa na shahada ya uandishi wa habari ambayo aliipata huko Madrid, Hispania.
Lakini kwa upande wa wachezaji wa Bara kuna kina Reliants Lusaja, Salmin Hoza, Ayub Semtawa, Paul Nonga na wengine wengi huku Munthary akidai kuwa kama isingekuwa soka ndoto yake ilikuwa kuwa rubani lakini amejikuta akiangukia katika masuala ya benki na fedha.
“Soka ni sehemu ya vitu ambavyo napenda kuvifanya, lakini mimi ni msomi ambaye ndoto yangu ilikuwa ni kuwa rubani lakini nimejikuta nikisomea masuala ya fedha na benki katika Chuo cha CBE (Chuo cha Elimu ya Biashara),” anasema.
“Mpango wangu siku moja nikiamua kuachana na mambo ya mpira nirudi kufanyia kazi taaluma yangu lakini pia kujiendeleza kwa sababu nina diploma ya masuala hayo ya fedha.”
YONA, DIARRA, CAMARA
Munthary anashika nafasi ya tatu kwa makipa walioruhusu mabao machache katika Ligi Kuu hadi sasa ikiwa imechezwa kati ya michezo 25 hadi 26 kwa baadhi ya timu, lakini kipa huyo anadai kwamba bado anaendelea kujifunza kwa wenzake.
“Ni kweli nipo nafasi ya tatu nikiwa sijaruhusu mabao kwenye mechi 11 kati ya 26 tulizocheza hadi sasa. Bado nahitaji kujifunza zaidi ili kufikia ubora wa wengine ambao ni Moussa Camara ambaye ndiye kinara akiwa hajaruhusu mabao kwenye mechi 15, namba mbili akiwa ni Djigui Diarra ambaye hajaruhusu kwenye mechi 14 lakini pia navutiwa na ubora wa Yona Amos,” anasema na kuongeza:

“Ili uwe bora unatakiwa kujifunza kwa watu unaoamini ni bora zaidi yako... kiukweli navutiwa na ubora wa makipa hao watatu kwenye ligi hivi sasa na nimekuwa nikiwafuatilia wananipa nguvu ya kujiamini na kuamini kuwa kuna nafasi ya kuwa bora zaidi ya nilipo sasa.”
BAO LA DIABY
Ukiondoa mabeki wanavyoteseka na chenga wakilishwa nyasi na washambuliaji kutoka timu pinzani, makipa na pia kuna shida wanapitia kama anavyosema Munthary.
“Sio uzembe, lakini naweza kutaja kuwa bao nililofungwa na beki wa Azam FC, Yoro Diaby alinifunga akiwa mbali sana na mimi nilikuwa nje ya eneo langu.

“Huu ndio uzembe ambao nimewahi kuufanya nikiwa kipa na nakumbuka mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Hilo bao lilinipa wakati mgumu sana siku hiyo kwa sababu nilijilaumu mwenyewe kufanya uzembe.”
MKUDE, CHANONGO
Munthary si mgeni kwenye soka, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kuanza kukipiga na mastaa waliohudumu kwenye soka kwa miaka zaidi ya 14 sasa kama anavyosema kwamba alianza mpira kitambo sana sambamba na Jonas Mkude, Haruna Chanongo na Dullah Hugo.
“Hao ni baadhi ya wachezaji ambao nawakumbuka nilianza nao kwenye kikosi cha timu ya Simba ya vijana miaka hiyo kabla ya kila mmoja kupata maisha mengine nje ya Simba,” anasema na kuongeza:

“Sikujulikana kwa sababu nilikuwa nacheza nafasi ngumu ambayo ilikuwa na wachezaji wengi wazuri hasa wa kigeni ambao ndio walikuwa wanaaminiwa zaidi kwa miaka hiyo.”
Munthary anasema licha ya kutofahamika akiwa Simba haiondoi kuwa ameanza maisha ndani ya kikosi hicho huku akiwataja Mkude na Chanongo kuwa ndio waliojulikana zaidi kutokana na kupata nafasi ya kucheza timu ya wakubwa.