Prime
Mwamposa angeanza kwa kuwaombea Kibu na Mpanzu

Muktasari:
- Mwamposa aje kufanya nini uwanjani? Sijui. Labda kuiombea timu. Sawa, hapo nitakubali. Na aanzie pale mbele kwa rafiki zetu wawili, Elie Mpanzu na Kibu Dennis. Kwa mbali kidogo anaweza kumwombea na Moussa Camara.
SIMBA hawajaacha kitu katika pambano la kesho pale Temeke. Wazungu huwa wanasema ‘No stone unturned’. Hakuna jiwe ambalo halijageuzwa. Hawataki kufanya kosa. Na mwamemwalika hata Mtume wa Mungu, Boniface Mwamposa katika pambano hilo.
Mwamposa aje kufanya nini uwanjani? Sijui. Labda kuiombea timu. Sawa, hapo nitakubali. Na aanzie pale mbele kwa rafiki zetu wawili, Elie Mpanzu na Kibu Dennis. Kwa mbali kidogo anaweza kumwombea na Moussa Camara.
Hawa Kibu na Mpanzu waliinyima Simba ushindi katika pambano lile lililopita dhidi ya Al Masry. Narudia, hakuwacheza mpira rahisi. Kila mmoja alikuwa anacheza kivyake zaidi. kila mmoja alikuwa anausaka kivyake ufalme wa Simba.
Kibu kulia angeweza kujaribu kuingia ndani kulazimisha kupita katika msitu wa watu ili awe katika nafasi nzuri ya kupiga shuti. Kuna wakati aliwachomoka Al Masry vizuri tu lakini akapiga shuti badala ya kumpasia Leonel Ateba aliyekuwa karibu.
Kule kwa Mpanzu hadithi ilikuwa hii hii tu. Alikuwa na kasi nzuri huku akijaribu kuwachomoka mabeki lakini chaguo lake la kwanza lilikuwa kupiga shuti kwa kipa wa Al Masry na siyo kumuangalia mchezaji mwenzake aliyekuwa katika nafasi nzuri zaidi.
Kesho kuna mambo mawili matatu ambayo Simba wanapaswa kuyatarajia kabla ya dakika hazijaanza kuyoyoma katika uwanja wa Benjamin Mkapa. Jambo la kwanza ambalo kila mtu analifahamu ni Al Masry watakuja Kwa Mkapa huku wakijihami kwa kiasi kikubwa.
Wataweka watu wengi mbele ya mpira. Watakaa watu wengi mbele ya kipa wao. Kinachotakiwa kwa Simba ni kuwa na uvumilivu. Katika soka la kisasa timu inavyokaa mbele ya kipa wao kinachotakiwa ni uvumilivu wa namna ya kufungua msitu wa walinzi wa timu pinzani.
Hapo ndipo vita ya Pep Guardiola na Jose Mourinho ilikuwa tamu wakati wa ule. Huyu anaweka watu wengi mbele ya kipa na huyu mwingine bwana Guardiola anajaribu kuifungua safu ya ulinzi. Kinachotakiwa kwa Guardiola ndicho kinachotakiwa kwa Simba. uvumilivu wakati wa kutafuta suluhisho.
Kwa bwana Pep Guardiola hataki krosi ya lazima hata kama mpira umebakiza dakika mbili. Ni mwendo wa pasi, kisha pasi tena, kisha pasi nyingine. Ukipiga krosi ya lazima kwa kufuata mihemko ya mashabiki jukwaani walinzi wa Al Masry wataosha au kipa atadaka na kulala chini.
Ni hapa pia ambapo hata kina Kibu na Mpanzu wanapaswa kuwa wavumilivu. Siku ile Simba walimiliki mpira vema kuanzia nyuma hadi mbele. Walipofika mbele ndipo waliamua kuchukua maamuzi yao binafsi bila ya kuwa wavumilivu.
Sasa katika pambano hili wategemee Al Masry watajaa zaidi katika lango lao. Kadri dakika zitakavyokuwa zinayoyoma ndivyo Al Masry watajikita zaidi katika lango lao wakifurahia mchezo wa kujihami, pia wakifurahia papara ya Simba.
Hapa ndipo Clatous Chota Chama aliwateka Simba. Alikuwa mvumilivu na hana papara. Hesabu zake nyingi wakati huo zilitegemea zaidi uvumilivu. Angeweza kukaribia kuingia katika boksi lakini akili yake ingetulia zaidi kuona namna gani anaweza kuwafungua maadui zake kwa pasi murua.
Kitu kingine ambacho Simba wakitegemee katika pambano la kesho ni rafiki zetu Waarabu watakuwa wanajiangusha kila dakika. Ni vizuri kucheza na mwamuzi. Bahati nzuri na mwamuzi atakuwa anaelewa tabia hizo. Kila mchezaji akijiangusha Simba wamzunguke mwamuzi.
Kitu cha tatu ambacho Simba wanapaswa kuwa nacho makini katika pambano la kesho ni mipira mirefu ya Waarabu katika kuanzisha mashambulizi. Simba wasidhani Waarabu hawatakuwa na wazo la kupata bao, hapana. Watakuwa na wazo hilo ingawa litakuwa wazo la pili baada ya kujilinda.
Katika pambano la kwanza wakiwa nyumbani walikuwa wakipiga mipira mirefu kwenda kwa watu wao wa mbele. katika pambano hili watafanya hivi hivi. Wataacha watu wawili wenye kasi kwa ajili kusaka walau bao moja endapo Simba watazubaa.
Wakati unamfukuza mwizi hakikisha kwamba milango yako imefungwa. Simba wafunge milango yao vema wakati wanamfukuza mwizi. Iliwahi kutokea katika pambano la Al Ahly Tripoli. Simba walijikuta wametanguliwa bao la haraka bila ya kutarajia.
Ni kama tu lilivyokuwa bao la pili la Al Masry siku ile. Simba walikuwa wanalisakama lango la wenyeji wakitaka kusawazisha lakini ghafla ukapigwa mpira mrefu kwenda upande wa kushoto kwa mtu ambaye alikuwa amevunja mtego wa kuotea kwa Mohamed Husein. Krosi ilipopigwa ndani likaja bao la pili.
Kwa ninavyoitazama mechi, Simba wana uwezo mkubwa wa kupindua meza kama wakitulia. Waliwakamata vema Al Masry kule Misri. Ilinifikirisha pia kuhusu uwezo wa timu za Misri kwa sasa. Ningeshangaa kama wasingewakamata. Kama Al Ahly wenyewe tunacheza nao vizuri tu siku hizi bila ya hofu, vipi kwa Al Masry ambayo inashika nafasi ya nne.
Bado yale maswali mawili yanaendelea. Mpira wetu umekua au mpira wa Waarabu umeshuka kidogo? Sijui. Endapo Simba watabadilisha kibao kesho litakuwa jambo linalostahili ndani na nje ya uwanja. Timu ambayo iliwahi kuongoza katika kundi la Al Ahly kwa nini itolewe robo fainali na timu inayoshika nafasi ya nne Misri?
Kila la kheri kwa Mnyama pale Temeke kesho. Wachezaji wanaweza wasifahamu sana umuhimu wa mechi, lakini kwa mashabiki na viongozi hili ni pambano la kwenda nusu fainali kwa sababu misimu miwili nyuma watani zao walifika fainali za michuano hii. Unatolewaje katika hatua ya robo fainali? Utaishije mitaani?