Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Eti Wabrazili wanatembelea nyayo za Neymar

JUZI tu nilikuwa nakatiza katika vijiwe vya hapa Sao Paulo na kusimuliwa kisa ambacho sikuwahi kukisikia. Visa vingine havifiki katika vyombo vya habari vya Magharibi na ni vigumu kuvisikia mpaka ufike hapa Brazil nilipo.

Naambiwa familia ya Neymar iliwahi kupata ajali huku Neymar akiwa mtoto mdogo aliyekalishwa katika kiti cha nyuma cha gari. Wazazi wake walipata majeraha, lakini Neymar hakujua kilichokuwa kimeendelea na walipoenda kumtoa alikuwa akitabasamu. Bahati iliyoje!

Wakazi wa hapa Brazil wanaamini kuwa Neymar ana bahati na chochote anachogusa kinageuka kuwa bahati. Dada mmoja, Teme da Silva, niliyekutana naye eneo la Sao Joao hapa hapa Sao Paulo aliniambia kuwa Neymar hajawahi kushindwa kitu chochote maishani kwa sababu ana bahati ya mtende.

Hata baada ya pambano la juzi Alhamisi dhidi ya Croatia, Wabrazili waliokuwa wamezagaa baa mbalimbali walikuwa wanahesabu bahati za Neymar. Ukilinganisha walichokuwa wanafikiri ni kweli kwamba Neymar ana bahati ya mtende.

Kwanza kabisa alifunga mabao mawili katika mechi hiyo. Alikuwa amevaa jezi namba 10. Lakini tangu mwaka 2002 hakuna Mbrazili aliyevaa jezi namba 10 aliyefunga bao katika Kombe la Dunia.

Ni kweli. Rivaldo alikuwa Mbrazili wa mwisho kuvaa jezi namba 10 na kufunga bao katika Kombe la Dunia mwaka 2002. Baada ya hapo mwaka 2006, jezi namba 10 alivaliwa na Ronaldinho Gaucho katika fainali zilizochezwa Ujerumani lakini hakufunga.

Mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, jezi hiyo ilivaliwa na Ricardo Kaka lakini hakufunga. Mwaka huu, mechi ya kwanza tu Neymar ameitendea haki na kufunga. Lakini kutokana na bahati yake hata mabao yake yenyewe mawili yameshangaza.

Bao la kwanza lilionekana kuingia kwa njia za kizembe, bao la pili nusura shuti lake lidakwe na kipa wa Croatia ambaye aliupangulia mpira wavuni. Hiyo ndio bahati ya Neymar ambayo imekuwa ikizungumzwa mno katika jiji la Sao Paulo.

Neymar pia angeweza kupewa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko Luka Modric, lakini kwa bahati yake nzuri, mwamuzi Mjapan hakuona vizuri na badala yake akampa kadi ya njano.

Hata hivyo, mtu mmoja alinifurahisha zaidi wakati alipokwenda mbali zaidi na kudai kwamba Neymar alikuwa na bahati sana kwa kulelewa na wazazi wake wote wawili. Wachezaji wengi wa Brazil wamelelewa na mama zao tu.

Ronaldo de Lima, Robinho, Rivaldo na mastaa wengi wa Brazil wamelelewa na mama peke yake. Kisa? Inadaiwa kuwa wanaume wa Brazil pindi wanapompa ujauzito mwanamke huwa wanakimbia zao.

Wanaume wa Brazil hawafanyi ngono kwa kutafuta mtoto na badala yake mtoto anakuja kwa bahati mbaya. Baada ya hapo huwa wanakimbia. Kama kuna dhambi kubwa inayofanywa Brazil basi ni kutoa mimba.

Ni hapa ndipo inapotajwa kuwa bahati ya Neymar ilianzia tangu pale baba yake aliposhindwa kumkimbia mama yake na kuamua kuishi naye. Leo baba huyo ndiye anayepiga pesa tofauti na baba za mastaa wengine wa Brazil ambao waliwakimbia watoto wao.

Katika hoteli niliyofikia, Mbrazili mmoja ameniambia kuwa Brazil hawana timu ya uhakika sana na ndiyo maana wamehenyeshwa na Croatia, lakini watachukua ubingwa wa dunia kwa sababu ya kutembelea nyota ya Neymar.

Bahati nyingine inayonishangaza kutoka kwa Neymar ni jinsi ambavyo wachezaji wenzake wameshindwa kufikia kabisa hatua ya kumkaribia kwa kupendwa na mashabiki. Sawa Neymar ni staa, lakini ni vigumu kukuta mashabiki wamevaa jezi nyingine zaidi ya ile ya Neymar.

Maisha yanaonekana kuwa tofauti na zama za kina Ronaldinho. Sawa Ronaldinho alikuwa staa, lakini naambiwa kuwa bado jezi za mastaa wengine zilikuwa zinauzika tofauti na wakati huu.

Wakati Ronaldo de Lima akiwa staa, bado jezi za kina Rivaldo na Roberto Carlos zilikuwa zinauzwa. Lakini hapa Sao Paulo sijawahi kukuta shabiki amevaa jezi ya Oscar wala Thiago Silva. Jezi zote ni namba 10 hata zile ambazo hazina majina mgongoni.