Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA : Mleteeni Rodgers kikombe cha kahawa

Muktasari:

  • Najaribu kuwaza tu. Huyu ndiye mtu wa mwisho ambaye Rodgers angependa amuone anaondoka Anfield. Unajua kwa nini? Kimo chake. Kuna kitu Rodgers anataka kukifanya Liverpool.

YUKO na kikombe chake cha kahawa. Labda ni kahawa ya Ghana, Brazil au Tanzania. Ni kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, anavyoonekana msimu uliopita, siku moja alimpigia simu, Luis Suarez, wakutane katika ofisi yake iliyopo uwanja wa mazoezi wa Liverpool, Melwood.

Akiwa na sura mbili, usoni na kisogoni, Rodgers alimkaribisha Suarez kahawa kabla ya kuahidi kumuuza kama Liverpool ingeshindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

Alikuwa anacheza karata. Alikuwa ametupa kopa huku Suarez akiwa ameshikilia dume. Karata ya Rodgers imeangukia patupu.

Najaribu kuwaza tu. Huyu ndiye mtu wa mwisho ambaye Rodgers angependa amuone anaondoka Anfield. Unajua kwa nini? Kimo chake. Kuna kitu Rodgers anataka kukifanya Liverpool.

Anataka kitu hicho kimuibue kuwa shujaa miaka michache ijayo. Anaitaka Barcelona ya Anfield. Barcelona ambayo miaka ya karibuni mashabiki tumekuwa tukiwadhulumu wachezaji wake. Soka walilotuonyesha lina thamani zaidi ya viingilio vyetu na malipo yetu ya ving’amuzi.

Nawaza tu. Rodgers anataka mpira utembee kuliko wachezaji wanavyotembea. Unahitaji wachezaji wafupi wanaonyambulika kirahisi. Unamuhitaji Luis Suarez mwenye futi 5’11. Unamuhitaji Iago Aspas mwenye futi 5’9. Unamuhitaji Luis Alberto mwenye futi 5’11. Unamuhitaji Coutinho pia.

Nawaza tu, Rodgers hawataki watu warefu. Na ndio maana haishangazi kuona amewauza Jonjo Shalvey na Andy Carroll wenye futi zaidi ya sita ambao hawawezi kucheza mpira wa haraka haraka wa chini.

Na sasa wakati huu alipokuwa anatazamana na Suarez kumsihi abaki ili waishi katika ndoto moja, Rodgers alikuwa anajua kwamba Suarez ni aina ya mshambuliaji anayemhitaji kuliko mshambuliaji yeyote duniani kwa sasa kwa sababu ananyambulika na anaweza sana kucheza mipira ya chini.

Nawaza tu kuhusu Brendan Rodgers. Akiwa na Swansea alikuwa na wachezaji wa aina hii. Kina Wayne Routledge, Nathan Dyer, Scott Sinclair, Joe Allen  na wengineo. Wote walikuwa na futi 5 tu na hivyo kuwafanya wasitofautiane sana na Mwinyi Kazimoto wa Taifa Stars.

Na ndio maana Rodgers ameingia ganzi kuhusu Suarez kuhama. Tatizo ni kwamba asichojua ni kuwa mchezaji wa Amerika Kusini, Hispania au Italia hana habari na historia ya Liverpool. Wachezaji wanaoiheshimu Liverpool ni wale wa England, Wales, Ireland, Scotland na Ireland Kaskazini.

Hawa ndio wapo karibu na historia ya Liverpool. Wapo karibu na historia ya Bill Shankly. Wao ndio wanaoelewa kwa nini katika vyumba vya kubadilishia nguo wakati unaelekea dimbani, Shankly aliweka kibao kilichoandikwa ‘This is Anfield’.

Hawa wa Amerika Kusini kina Suarez, Carlos Tevez, Robinho na wengineo, wanachoangalia ni mshahara, kucheza Ligi ya Mabingwa na kutafuta nchi yenye fukwe nzuri kwa ajili ya kuogelea na familia.

Wakati huu Brendan Rodgers akijaribu kumsihi Suarez kubaki Liverpool, hapa walikutana watu wenye ndoto mbili tofauti. Huyu mmoja alikuwa anajaribu kutengeneza timu ya kufikirika kichwani.

Na huyu mwingine alikuwa anaufikiria wimbo wa Ligi ya Mabingwa unaopigwa kila Jumanne usiku na Jumatano usiku. Ule wimbo ambao Steven Gerrard hajausikia kwa miaka minne sasa, lakini ameamua kuwa mzalendo kwa kuendelea kuusikiliza zaidi wimbo wa You Will Never Walk Alone.

Nawaza tu jinsi Brendan Rodgers anavyoumia kuliko mabosi wa Liverpool. Kila siku namsikiliza anaposema Suarez hauzwi. Anaongea hili kwa dhati pengine kuliko Muammar Gaddafi alivyokuwa anaongea kuhusu kukerwa na uwepo wa askari wa Marekani katika ardhi ya Libya.

Mabosi wanajua kwamba Suarez anauzwa. Wanachofanya ni kumpandisha bei. Brendan Rodgers hana kauli yoyote ya maana kwa sababu uamuzi wa mauzo ya mchezaji unatoka katika Bodi ya Liverpool. Unatoka kwa tajiri wa Marekani John Henry ambaye ndiye mmiliki wa timu.

Namwonea huruma Rodgers. Kwa kitu anachokifiria basi inabidi kiendane na mafanikio kama anataka kubakiza wachezaji mahiri. Inabidi mafanikio yaje haraka. Niliwahi kuandika hapa kwamba mashabiki ni wazalendo kuliko wachezaji.

Vinginevyo wakati huu akiwa na kikombe cha kahawa pale Melwood akiwaza jinsi Liverpool itakavyocheza soka safi baada ya misimu miwili, anaweza kusikia mwakani Coutinho anahama baada ya kung’ara sana msimu ujao. Natabiri atakuwa moto.

Mbaya zaidi kwake ni kwamba Suarez akihamia Arsenal basi moja kwa moja atakuwa ameipa uhakika wa kuwepo Top Four msimu ujao. Chelsea yenye utatu mtakatifu chini ya Juan Mata, Oscar na Eden Hazard lazima iwepo.

Utaiondoaje Manchester City inayotumia pesa za usajili kuliko Serikali ya Somalia.   Wala sijawahi kuwaza kuwa Manchester United itaondoka Top Four ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo licha ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

Na sasa nawaza tu jinsi Rodgers anavyojisikia vibaya wakati huu akiendelea kunywa kikombe kingine cha kahawa katika kiti kile kile cha Melwood. Suarez anachafua mpango wake. Mpango wa kuitengeza Swansea nyingine ndani ya Anfield. Mpango wa kuitengeneza Barcelona ndani ya Anfield. Mleteeni kikombe kingine cha kahawa, nitalipa.