NYUMA YA PAZIA : Perez na peni yake ya Almasi
Muktasari:
- Baadaye akaniambia wakati mwingine ukienda disko lazima upigane kuonyesha umwamba wako na ufahari wako. Hata kama hakuna sababu. Hata Fiorentino Perez ameuonyesha ufahari wake kwa kumsajili Gareth Bale.
NDEGE ya kifahari zaidi duniani Air Force One anapanda Rais wa Marekani. Haikutengenezwa kwa ajili ya usalama wa Rais wao tu pia ilitengenezwa kwa ajili ya kuonyesha ufahari wa Taifa la Marekani.
Wakati mwingine inabidi uonyeshe ufahari wako duniani bila ya kujali gharama nyingine. Ndiyo maana Rais Richard Nixon alimwalika katika ndege hiyo kiongozi wa Soviet wakati huo, Leonid Brezhnev.
Ndiyo maana Rais Ronald Reagan aliwahi kumwalika katika ndege hiyo, Malkia Elizabeth. Aione tu inakuaje na raha zake.
Ndiyo maana Rais Obama alimwalika Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron aipande mpaka Ohio kutazama mechi ya kikapu. Wakati mwingine unahitaji kuonyesha ufahari wako na tena wakati mwingine unauonyesha bila ya sababu.
Rafiki yangu mmoja anaitwa Johnnie. Mwanamuziki wa kundi la Kalamashaka la Kenya niliwahi kwenda naye klabu moja ya usiku jijini Nairobi kwa ajili ya starehe, lakini yeye akajiingiza katika ugomvi usio na sababu.
Baadaye akaniambia wakati mwingine ukienda disko lazima upigane kuonyesha umwamba wako na ufahari wako. Hata kama hakuna sababu. Hata Fiorentino Perez ameuonyesha ufahari wake kwa kumsajili Gareth Bale. Ilimradi atimize sera zake za ‘Ugalactico’ ambazo zinaitaka Real Madrid imsajili mchezaji mmoja ghali duniani bila ya kuzingatia mambo mengine ndani na nje ya uwanja.
Unaonyesha tu ufahari. Akaunti yake binafsi ina dola 1 bilioni za Marekani, ni tajiri. Wakati mwingine inabidi uonyeshe hilo kwa mashabiki, hasa unapokuwa Fiorentino Perez. Lazima mashabiki wa Madrid wakuone una jipya hata kama haihitajiki. Ameipiku rekodi yake mwenyewe aliyoweka kwa kumnunua Cristiano Ronaldo mwaka 2009 kwa kiasi cha pauni 80 milioni kutoka Manchester United. Wakati ule kulikuwa na umuhimu wake, lakini safari hii ilikuwa ni kama vile Obama alivyotaka kumwonyesha Cameroon ndege ya Air Force One.
Mtu aliyepisha ujio wa Bale ndiye ameonyesha kwamba kulikuwa hakuna umuhimu wa Bale kuja Santiago Bernabeu kama ni kweli yeye alipaswa kuondoka. Mesut Ozil ni fundi wa Kituruki, aliyezaliwa Ujerumani, akapikwa Hispania.
Unawezaje kumwondoa Ozil kwa gharama za ujio wa Bale? Hapa unamzungumzia mchezaji aliyepika mabao mengi zaidi kuliko mchezaji mwingine yoyote katika Ligi Kuu tano kubwa Ulaya, Hispania, England, Ufaransa, Ujerumani na Italia.
Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa Perez kufanya hivi. Wakati mwingine anakuwa anataka tu kuwaonyesha watu jinsi Real Madrid ilivyo. Ni kama Marekani na Air Force One yao. Huyu ndiye mtu ambaye aliwahi kumuuza Claude Makelele na kumnunua David Beckham.
Tatizo halikuwa kununuliwa kwa David Beckham. Tatizo ni nani angekaba badala ya Makelele? Kikosi kilikuwa na Luis Figo, Beckham, Zinedine Zidane na Ronaldo De Lima. Nani angekaba sasa? Hakuna. Lakini katika kutaka kuonyesha ufahari, ilikuwa lazima Makelele auzwe. Ufahari unakuja na gharama zake.
Kuna kundi pia la Galactico lilikwenda Santiago Bernabeu wakiwamo Ricardo Kaka na Ronaldo, kwa gharama za kuondoka kwa Wesley Sneijder na Arjen Robben. Wote hawa baadaye wakaenda timu tofauti na wakatwaa ubingwa wa Ulaya huku Real Madrid mpaka sasa ikiwa haijatwaa ubingwa wa Ulaya tangu mwaka 2000 kwa lile shuti la Zinedine Zidane dhidi ya Bayer Leverkusen.
Hata hivyo, Perez lazima atuonyeshe ufahari wake bila ya kujali gharama zozote. Lazima atukumbushe Real Madrid ni kitu gani, hasa baada ya Barcelona kumsajili Neymar. Lazima aionyeshe dunia kwamba Real Madrid ina uwezo wa kumsajili mchezaji mwenye gharama mara mbili ya Neymar, hata kama ni kwa gharama za kumpoteza Ozil. Sioni kama Bale ni mchezaji wa kibiashara kama ilivyokuwa kwa Beckham. Hana sura yenye mvuto. Anatoka katika taifa la Wales. Hatimaye mchango wake uwanjani hauwezi kufikia pasi ambazo Ozil amepika mabao kwa Ronaldo, Higuain na Benzema kwa miaka mitatu iliyopita.
Ina maana Perez anatushawishi kwamba Bale ana thamani mara mbili ya Ozil, mara mbili ya Neymar, mara mbili ya Oscar Moura, mara tatu ya Santiago Cazorla, mara tatu ya Roberto Lewandowski. Inahitaji akili ya kawaida kukubali hili.
Kama akili ya kawaida ikigoma kukubali, kama akili yangu ilivyofanya basi unachoweza kusema ni kwamba Perez ameamua tu kutuonyesha ufahari wake.
Kwangu mimi, Bale anabakia kuwa mchezaji wa kwanza ghali zaidi duniani katika miaka ya karibu ambaye hana kipaji kikubwa. Ana kasi na mashuti basi. Na kwa wakati huu yupo fomu. Inakera kidogo kujikumbusha kuwa uanasoka bora wa dunia umetoka kwa Zinedine Zidane na leo umefika kwa Bale. Mbingu na ardhi.
Hata hivyo acha tu Perez atuonyeshe ubabe wake wa pesa. Mwandishi mmoja wa Hispania aliwahi kusema kuwa Perez huwa anatembea na Peni ya Almasi kuandika hundi zake za uhamisho wa Galacticoz. Hata ya Bale alitumia hiyo hiyo. Acha aonyeshe ufahari wake!