Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PUMZI YA MOTO: Tuhuma za Tabora United zitaachwa zipite?

Muktasari:

  • Kuelekea mechi ya Tabora United na Yanga, sauti kadhaa za kurekodiwa ambazo klabu ya Tabora United ilizithibitisha, zilivuja zikiwahusisha wachezaji na viongozi wa klabu hiyo na watu wanaosikika wakijitambulisha ni kutoka Yanga.

KWA mara nyingine tena mpira wa Tanzania umekumbwa na matukio yenye kuashiria ushawishi wa rushwa na upangaji matokeo.

Kuelekea mechi ya Tabora United na Yanga, sauti kadhaa za kurekodiwa ambazo zilivuja zikidaiwa kuwahusisha wachezaji na viongozi wa klabu hiyo na watu wanaosikika wakijitambulisha ni kutoka Yanga.

Watu hao walikuwa wakitamka maneno yenye kuashiria rushwa na upangaji matokeo kwa kuwataka wahusika wa Tabora United kuisadia Yanga ishinde mchezo huo.

Kwa kuwa hakuna aliyethibitisha, huwezi kuihukumu Yanga moja kwa moja kuwa inahusika (wanaweza kuwa ni wapinzani wa Yanga walioamua kutengeneza tukio la kuipaka matope timu hiyo kwa nia ovu), ni hadi uchunguzi ufanyike ndio ukweli utajulikana.

Hapo kwenye uchunguzi ndipo kwenye shida.

Viashiria kama hivi vimekuwa vikipatikana mara kwa mara lakini uchunguzi haufanyiki na au ukifanyika basi utakuja na majibu siyo.

Nitaweka hapa ushahidi wa matukio kadhaa ya aina hiyo ambayo aidha yalipotezewa juu kwa juu au uchunguzi haukuja na majibu yenye kunyooka.


1. MKASA WA ULIMBOKA MWAKINGWE

Septemba 2010 Simba walikuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar dimbani Jamhuri Morogoro.

Siku moja kabla ya mechi, kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado, akaripoti kwa uongozi wa klabu yake kwamba amepigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Ulimboka Mwakingwe akimtaka acheze chini ya kiwango kwenye mchezo huo.

Mtu huyo alimuahidi Kado kwamba kiongozi mmoja wa Simba ametoa shilingi laki nne za Tanzania kwa kazi hiyo na atampelekea yeye mwenyewe huko huko kambini.

Viongozi wa Mtibwa Sugar wakaweka mtego, na kweli mtu akanaswa.

Wakamkamata Mwakingwe akiwa ndani ya kambi ya Mtibwa Sugar akiwa na fedha taslimu laki nne, kama Kado alivyouambia uongozi wake.

Mwakingwe alipohojiwa, akasema hizo fedha ni za Shaaban Kado na alikuwa akimpelekea fedha zake.

Akapelekwa kituo cha polisi cha Manungu na baadaye kuachiwa kwa dhamana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro wa wakati huo, Thobias Andengenye, alilithibitishia gazeti la Mwananchi tuhuma hizo.

Lakini hakuna chochote kilichofuata baada ya hapo...hadi Mwakingwe alipokutwa tena na hatia ya rushwa mwaka 2023 akiwa na timu nyingine, na kufungiwa maisha na TFF.


2. MKASA WA WACHEZAJI WA AZAM FC

Mwaka 2012 Azam FC ilisimamisha wachezaji wake wanne waandamizi kwa tuhuma za rushwa baada ya mchezo dhidi ya Simba.

Wachezaji hao, Aggrey Morris, Deogratius Munishi, Said Murad na Erasto Nyoni, walituhumiwa kuihujumu timu hiyo na kupoteza 3-1.

Taarifa za ndani ya Azam FC zilisema wakati ule kwamba mmoja wa wachezaji hao alikamatwa na arafa za mawasiliano yake na kiongozi mkubwa Simba.

Mawasiliano hayo yalienda mbali na kuwataja wachezaji wenzake, na ndiyo maana wote wakahusishwa.

Kesi ikaenda TAKUKURU kwa uchanguzi ambao ulichukua takribani miezi 6, hakukuwa na majibu...yakapita.


3. KUKIRI KWA NSA JOB

Mwaka 2013, mchezaji wa zamani wa Azam FC, Yanga, Moro United, Coastal Union na Villa Squad, Nsa Job Mahinya, alikiri kwa mdomo wake kwamba kuna wakati akiwa moja ya timu zake, alihongwa yeye na wachezaji wenzake wacheze chini ya kiwango.

Pesa wakachukua lakini wakacheza kwa uwezo wao wote na mechi ikaisha kwa sare...yule aliyewahonga akarudi kuwadai pesa zake.

Japo Nsa Job alikiri mwenyewe lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Zaidi, TFF ikatoa taarifa ya kumtaka mchezaji huyo kumtaja kiongozi aliyewahonga...ikaishia hapo hapo.


4. KUKIRI KWA KABWILI

Mwaka 2020, kipa wa Yanga Ramadhan Kabwili, alikiri kwenye mahojiano na kituo cha redio cha East Africa, akisema aliwahi kujaribiwa kuhongwa na watu wa Simba ili apate kadi ya njano kuelekea mchezo wa watani wa jadi ili aukose mchezo huo.

Hizi zilikuwa tuhuma kubwa sana lakini hakuna hatua iliyochukuliwa zaidi ya matamko ya taarifa kwa umma ya TFF kwamba watachunguza.

Hakuna kilichoendelea tena baada ya hapo.


5. TUHUMA ZA BENJAMIN ASUKILE

Mwaka 2021, Benjamin Asukile wa Tanzania Prisons alitoa tuhuma za rushwa na upangaji matokeo zikiihusisha klabu ya Yanga.

Akizungumza mbashara baada ya mechi yao ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports wakati huo, sasa CRDB, iliyofanyika mjini Sumbawanga, Asukile alisema Yanga waliwatafuta wachezaji wa Tanzania Prisons wawahonge Sh40 milioni.

Tuhuma hizi zilikuwa kubwa sana....lakini hazikuwahi kuchukuliwa hatua yoyote.

Kwa hiyo hata sasa Tabora United wanapotoa tuhuma nzito kuhusu upangaji matokeo, ni ngumu kutarajia kama kuna hatua zozote zitakazochukuliwa.

Vinginevyo, hili nalo litaachwa lipite!