Prime
PUMZI YA MOTO: Ulegevu Simba, Yanga siyo kwa Karia tu, hata Tenga na wengine

Muktasari:
- Ni timu kubwa ambazo kusema kweli, hata serikali yenyewe inaziangalia kwa umakini mkubwa kwa sababau serikali nia na madhumuni yake ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani.
SAKATA la kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi bado linaendelea na kufunika kila kitu kinachoibuka katikati yake.
Kila siku sakata hili linarudi kwa namna yake.
Hivi karibuni hali ya hewa ilichafuka kutokana na kauli ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Bara, Steven Mguto.
Akiongea na Mwananchi Digital, Mguto alisema wamekuwa wakilazimika kutumia busara zaidi ili kukwepa kuzishusha daraja Yanga na Simba kwa sababu ni timu zenye ushawishi mkubwa.
"Nikubali tunaongoza timu ambazo kusema kweli ziko na umaarufu mkubwa...hiyo hakuna mtu anaweza kukataa.
Ni timu kubwa ambazo kusema kweli, hata serikali yenyewe inaziangalia kwa umakini mkubwa kwa sababau serikali nia na madhumuni yake ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani.

Piga picha umeishusha Yanga, umeishusha Simba...hebu piga picha.
Lakini ni kutokana, tumekuwa na maelezo mabaya tangu tuko nyuma, unaona!
Sasa ni tatizo kubwa kurekebisha mambo sasa hivi."
Kwa namna alivyomalizia hapo, Mguto alimaanisha haya matatizo ambayo Yanga na Simba wanayasababisha, ni muendelezo wa 'kudekezwa' na mamlaka zote zilizotangulia za mpira wetu.
Hata hivyo, maneno haya yakaurudisha upya mjadala wa sakata la watani.
Miongoni mwa wadau wakubwa wa mpira waliotoa kauli ngumu dhidi ya viongozi wa sasa ni katibu mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah.
Katika mfululizo wake wa mahojiano na vituo mbalimbali vya habari hapa nchini, Osiah amekuwa akirejea kauli yake ya kuwa uongozi wa sasa wa mpira umekuwa legevu sana tofauti na zamani.

Akatolea mfano utawala wa Leodeger Tenga kama Rais wa TFF na yeye akiwa katibu mkuu wake wa mwisho, akasema Yanga na Simba wasingeweza kufanya haya wanayoyafanya sasa.
Angetile ambaye alikuwa katibu mkuu wa TFF kuanzia Desemba 2010 hadi Desemba 2013, alitolea mfano mkasa wa Yanga kugomea mechi ya mshindi wa tatu Kombe la Kagame mwaka 2008, na adhabu waliyokutana nayo.
Angetile alikuwa sahihi kwenye mfano huo. Hata hivyo, kuna mikasa mingine ya hawa pacha ilitokea katika utawala wa Tenga na kuitingisha TFF kiasi cha kuibebesha lawama kama hizi za sasa, hata wakati yeye mwenyewe akiwa katibu mkuu.
MKASA WA MTIBWA 2011/12
Azam FC ilichukua ubingwa wa Kigi Kuu Bara msimu wa 2013/14, hata hivyo ingeweza kuchukua kabla ya hapo kama siyo TFF ya Tenga na katibu wake Osiah kuwa legelege.
Msimu wa 2011/12, Azam FC ilikuwa ikifukuzana na Simba kwenye mbio za ubingwa, tofauti ikiwa alama tatu tu hadi michezo mitatu ya mwisho.

Aprili 18, 2012, Simba walicheza na JKT Ruvu na kushinda 3-0, hivyo kuongeza pengo la alama hadi sita. Siku iliyofuata, Azam FC ikawakaribisha Mtibwa Sugar dimbani Azam Complex.
Matokeo yakiwa 1-1, Azam FC ikapata penalti dakika za jioni na Mtibwa wakagoma na kutoka uwanjani.
Mwamuzi akasubiri kwa muda wa kikanuni...hawakurudi, akamaliza mchezo.
Adhabu ya kosa la Mtibwa, kwa kanuni za msimu ule, ilikuwa kushushwa daraja na matokeo yao yote kufutwa.
Simba walikuwa wamewafunga Mtibwa mechi zote mbili, kufuta matokeo ya Mtibwa ilikuwa na maana ya kuinyang'anya Simba alama sita.
Azam FC ilipoteza kwa Mtibwa mchezo wa kwanza...maana yake isingeathirika na adhabu hii.
TFF ambayo Osiah alikuwa katibu mkuu, ilifanya maamuzi tofauti na kanuni zilivyoelekeza. Wakasema mechi irudiwe, tena kwenye uwanja huru. Unarudiaje mechi ambayo timu moja imetoka uwanjani kwa kugomea maamuzi?

Na mechi hiyo inarudiwaje kwenye uwanja mwingine ilhali uwanja uliotumika haukuwa na tatizo kwenye kugoma kwao?
Taarifa kutoka ndani ya kamati iliyoamua sakata hili zilisema kanuni zilipindishwa makusudi ili kuokoa alama sita za Simba.
Matokeo ya Mtibwa yangefutwa kama kanuni zilivyoelekeza, Simba ingepoteza alama sita na kuangukia nafasi ya pili, alama tatu nyuma ya Azam FC...mechi mbili kabla ya msimu kuisha.
Hii maana yake ubingwa ungepotea Simba na kwenda Azam FC.
Wajumbe wa kamati hawakutaka hili litokee hata kidogo.
Siku ya kwanza ya kikao ilikuwa ngumu na ndefu, hadi saa nane usiku hakukuwa na muafaka.
Siku iliyofuata ambayo kikao kilitakiwa kuendelea, wajumbe wawili, mkurugenzi wa ufundi Sunday Kayuni na mkurugenzi wa mashindano, Saad Kawemba wakasafiri.
Huku nyuma kina Osiah wakafanikisha jambo lao kwa sababu wawili wale ndiyo walikuwa kikwazo.
Mwenyekiti wa Azam FC wakati ule, Mzee Said Mohamed (marehemu) alilia kama mtoto kikaoni kulalamikia maamuzi haya lakini hakuna aliyemsikiliza.

Kwanza hakutakiwa kuchangia chochote kwa sababu alikuwa na masilahi ya upande mmoja.
Osiah anayajua haya kwa sababu yeye ndiyo alikuwa mtendaji mkuu wa TFF.
Kwa hiyo kama kweli anaona viongozi wa sasa wako legelege kwa Simba na Yanga, basi hali hiyo hata wao iliwakuta.
MKASA WA NGAO YA JAMII
Mwaka 2001, Simba ilikuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara lakini haikupata zawadi yao baada ya mdhamini mkuu, Safari Lager, kujitoa katikati ya msimu.
FAT chini ya mwenyekiti Muhidin Ndolanga (marehemu) iliahidi kuwapa zawadi yao pindi mdhamini mpya atakapopatikana.
Mwaka 2002 wakaja Vodacom lakini Simba hawakupewa zawadi yao.
Mwaka 2004 Ndolanga akaondoka, akaingia Tenga na FAT ikabadilika na kuwa TFF...lakini Simba hawakupewa zawadi yao.
Wakaendelea kucheza ligi bila kulalamikia zawadi yao hadi mwaka 2009.
Mwaka huo TFF ilirudisha mechi ya ngao ya hisani kwa jina jipya la Ngao ya Jamii, kama kiashiria cha ufunguzi wa msimu mpya.
Mechi hii ilifanyika kwa mara kwanza mwaka 2001 lakini haikufanyika tena hadi Tenga alipoirudisha mwaka 2009.
Kanuni zilitaka mabingwa na makamu bingwa wa msimu uliotangulia kukutana, ambao walikuwa Yanga na Simba mtawalia.
Lakini Simba waligoma kupeleka timu uwanjani wakishinikiza kulipwa kwanza zawadi yao ya 2001.
Yaani timu haikupewa zawadi ya ligi 2001, lakini iliendelea kucheza hadi 2009 ikaja kugomea mechi ya ngao ya jamii.
TFF ya Tenga ambayo Osiah anasema ilikuwa haichezwi, haikuchukua hatua yoyote ya kinidhamu dhidi ya Simba, zaidi tu iliwapa nafasi hiyo Mtibwa Sugar waliomaliza nafasi ya tatu.
Mtibwa nao hawakufanya ajizi, wakaichapa Yanga 1-0 kwa bao la Pius Kisambale na kuwa mabingwa.
Osiah hakuwepo TFF wakati huo kwa hiyo siyo sehemu ya ulegelege kwenye sakata hili.
Hata hivyo, vipi aukumbuke mkasa wa Yanga 2008 na siyo Simba 2008?