Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RIPOTI MAALUM: Janga, Watoto katika uraibu wa michezo ya kamari

Muktasari:

  • Ndani, watu wazima na watoto wanakusanyika karibu na mashine za kupangia pesa (slot machines), macho yao yakielekezwa kwenye skrini, wakiwa na matumaini ya kupata pesa za haraka kupitia mchezo wa kubahatisha.

KATIKATI ya eneo la Mwandege Magengeni, wilayani Mkuranga mita 20 tu kutoka msikitini, kuna kituo cha michezo ya kubahatisha kinachoonekana kuwa cha kawaida.

Ndani, watu wazima na watoto wanakusanyika karibu na mashine za kupangia pesa (slot machines), macho yao yakielekezwa kwenye skrini, wakiwa na matumaini ya kupata pesa za haraka kupitia mchezo wa kubahatisha.

Mahali hapo katika Wilaya ya Mkuranga, Pwani, ni moja ya vituo vya michezo ya kubahatisha ambavyo havizuii watu kucheza bila kujali umri wao. Uchezaji wake unamtaka mtu kubonyeza vitufe vya mashine hiyo.

Watoto wawili wenye umri kati ya miaka 10 na 15 wanaketi, wakielekeza macho yao kwenye skrini ya mashine hiyo na kufuatilia kwa ukaribu jinsi mchezo unavyokwenda.

“Kama ningekuwa mimi, ningekwenda nyumbani mfuko wangu ukiwa umejaa,” anasikika mtoto mmoja baada ya mtu aliyekuwa akicheza kushinda sarafu zenye thamani ya Sh4,000 na kutaka kuendelea na kamari.

Baada ya kuhojiwa, watoto hao waliweka wazi kwamba wamekuwa wakicheza katika mashine hiyo mara kadhaa, wakitumia pesa wanazopewa na wazazi kwa ajili ya kutumia wakati wa shule.

“Nimepata ushindi mara kadhaa,” anasema mmoja wa watoto hao.

Mwandishi wa makala hii alitaka kufahamu zaidi kuhusu watoto wanaoshiriki katika michezo ya kubahatisha, licha ya sheria kuzuia sio tu kucheza bali hata kuwepo mahali kama hapo, na hapa kuna sehemu ya mazungumzo hayo.

Mwandishi: Kwa nini mnacheza mchezo wa kubahatisha?

Kijana: Tunataka pesa zaidi za kutumia shuleni.

Mwandishi: Je, nini kitatokea ikiwa baba yako atakukuta hapa, kwa sababu wewe hauruhusiwi kufanya hivi?

Kijana: Baba yangu haishi hapa.

Mwandishi: Unakaa na nani?

Kijana: Naishi na mama yangu.

Mwandishi: Je, itakuwaje ikiwa atakukuta hapa?

Kijana: Kawaida haji karibu na mahali hapa.

Mwandishi: Mnatoa wapi pesa za kamari?

Kijana: Kwa kawaida tunapewa pesa za kutumia wakati wa masomo na huo ndio mtaji wetu.

Msimamizi wa mashine hii ya mchezo wa kubahatisha ni kijana mdogo, hiyo ikaibua shauku ya kutaka kufahamu kama anastahili kujihusisha na aina hiyo ya biashara.

“Niko hapa kwa muda, nimekaa kwa niaba ya kaka yangu. Inamilikiwa na Mchina, lakini yeye ndiye msimamizi wa mashine hii,” anasema kijana huyo aliyedai kuwa na umri wa miaka 17.

Hali ya Mwandege ni mfano halisi katika maeneo mengi ya Dar es Salaam na vitongoji vya jirani ambavyo vinakumbwa na ongezeko kubwa la sekta ya michezo ya kubahatisha.

Mashine za michezo ya kubahatisha kwa namna ya pekee, zinaenea sana katika mitaa ya jiji na ukiukaji mkubwa wa sheria na kanuni, ukiwa na tishio la uraibu miongoni mwa kizazi kipya ambacho sasa kinavutwa katika michezo hiyo kwa ajili ya kupata pesa za haraka.


WATOTO WAKIRI

Utafiti huru uliofanywa katika maeneo ya Mwandege, Buguruni, Temeke, Manzese na Tabata jijini Dar, ulifichua kuhusu kuenea kwa mashine hizo maarufu kama ’Dubwi’.

Maeneo kama Buguruni, katika Barabara ya Mandela, si rahisi kugundua mashine hizo wakati wa mchana lakini jioni, zinaonekana kando ya barabara, karibu na daraja la kivuko cha watembea kwa miguu.

Nyingine zinapatikana katika maduka ya rejareja ambapo hata watoto wanaweza kuzifikia mashine hizo kwa urahisi.

Martin Bernard (14) wa eneo la Tabata anasema, alivutwa na marafiki zake ambao walikuwa wakipata pesa kupitia kubeti.

“Nilidhani naweza kufanya hivyo ili nipate pesa zaidi. Walikuwa wakizungumzia dau walizoweka na ushindi waliopata, ilinifanya niwe na hamu. Kwa hiyo, nilitaka kuhisi hiyo furaha na kuwa na uwezo wa kununua vitu bila kuhitaji kuomba wazazi wangu,” anasema mtoto huyo.

Mandela Onesmo, mwenye umri wa miaka 12 kutoka Manzese, anasema pia anabashiri mechi za michezo mbalimbali ili kupata pesa zaidi za kununua vitafunwa na vitu vya kuchezea ambavyo wazazi wake kwa kawaida hawampatii.

“Mara nyingi naona watoto shuleni wakinunua vitafunwa vyenye ladha nzuri, na mimi najisikia kuachwa nyuma,” anasema Mandela, huku Ibrahim Mwenda (15), pia kutoka Manzese, anafafanua alishawishiwa na marafiki kabla ya kuwa na shauku ya kujiunga nao.

“Nilitaka kuona kama ningeweza kupata pesa haraka kama marafiki zangu walivyofanya, lakini nilishinda mara tatu tu kati ya bet nyingi nilizoweka kwenye programu za kubeti,” anasema.


SHERIA YAZUIA WATOTO

Michezo ya kubahatisha inaruhusiwa Tanzania, lakini kuna mipaka kuhusu umri wa washiriki, usajili, na maeneo ya michezo hiyo.

Kipengele cha 70 cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya Mwaka 2003 inazuia watoto chini ya umri wa miaka 18, sio tu kushiriki katika kamari bali pia kuonekana mahali popote ambapo shughuli yoyote ya michezo ya kubahatisha inafanyika.

“Mtu hatopaswa kuruhusu au kusababisha mwenye umri wa chini ya miaka kumi na nane kuendelea kuwepo katika maeneo ya michezo ya kubahatisha; (b) kukaa kwenye kiti au kuwepo kwenye meza ya michezo ya kubahatisha, mashine za kupangia pesa, au eneo lingine ambalo michezo ya kubahatisha inafanyika; au (c) kushiriki, kucheza, kuruhusiwa kucheza, kuweka dau, au kukusanya ushindi, iwe kwa kibinafsi au kwa njia ya wakala, katika au kutoka kwenye shughuli yoyote ya michezo ya kubahatisha,” sheria inasema.

“Mtu yeyote atakayekiuka mojawapo ya vifungu vya sehemu hii atakuwa amefanya kosa na akipatikana na hatia, atahukumiwa faini isiyo chini ya Sh1 milioni lakini isiyo zaidi ya Sh5 milioni au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote viwili,”  inaongeza.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwani watoto wanashiriki licha ya uwepo wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ya Tanzania (GBT) ambayo kwa mujibu wa sheria inahusika na usimamizi, ufuatiliaji, na udhibiti wa shughuli za michezo ya kubahatisha nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe, anasema uvunjaji wa masharti ya leseni, shughuli haramu, na ushiriki wa watoto ni kati ya changamoto ambazo wakala huyo anashughulikia.

‘Ni kweli kwamba watoto hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli za michezo ya kubahatisha lakini changamoto ni kwamba kuna waendeshaji haramu ambao hawajali kizazi kijacho,” anasema Mbalwe ns kuongeza kuwa, bodi imekuwa ikifanya ukaguzi wa ghafla kwa lengo la kukamata wakiukaji.

Baada ya kufahamishwa kuhusu mashine za kupangia pesa kuruhusu watoto kucheza mchezo huo, Mbalwe aliahidi kuchukua hatua.

Baadhi ya maofisa kutoka bodi walipiga simu kurudi kujua mahali na maelezo ya kina ya hali hiyo, wakiahidi pia kukagua eneo hilo na kuchukua hatua.

Hata hivyo, karibu mwezi mmoja baadaye, biashara inaendelea kama kawaida.

Bodi hiyo inasimamia aina tofauti za michezo ya kubahatisha kama vile kasino, bahati nasibu, mashine za kupangia pesa, kubeti michezo na shughuli nyingine za michezo ya kubahatisha.

Bodi hiyo pia inasajili maeneo ya michezo ya kubahatisha ambayo hayaruhusiwi kuwa karibu na nyumba za ibada, shule, maeneo yaliyozuiwa na maeneo ambayo si rahisi kufikiwa.

Mwaka jana, bodi ilisitisha kwa muda utoaji wa leseni za mashine za kupangia pesa kwa waombaji wapya ikidai kuwa inaanzisha Mfumo wa Ufuatiliaji wa Kielektroniki ambao unalenga kusimamia operesheni za mashine za kupangia pesa. Fursa hiyo itatumika pia kutatua masuala ya shughuli haramu za mashine za kupangia pesa ambazo “zimeathiri sana taswira ya tasnia ya michezo ya kubahatisha.”

Hadi Mei mwaka huu, utoaji wa leseni za mashine za kupangia pesa haukuwa umerejelewa.

Baadhi ya waendeshaji wa michezo ya kubahatisha pia wanalaumu waendeshaji haramu ambao wanachafua taswira ya tasnia.

“Waendeshaji waliosajiliwa kawaida wanajua kuwa wao wanawajibika kulinda watoto kutoka katika michezo ya kubahatisha,”  anasema Meneja wa Operesheni wa Kampuni ya Kimataifa ya Kubeti ya Betway, Jimmy Kennedy.

“Kwa kiasi kikubwa, waendeshaji haramu wanatuharibia sisi,” anasema Kennedy ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Kulingana naye, waendeshaji wanapitia ukaguzi mkali na wanapewa masharti makali kabla ya kupata leseni ya uendeshaji.

“Kwa mwendeshaji ambaye anapitia taratibu za kisheria kupata leseni, hawezi kuhatarisha kufutwa kwa leseni kwa kuruhusu watoto kushiriki,” anaongeza Kennedy.


DAWATI LA JINSIA

Dawati la Jinsia la Polisi ambalo linahusika na masuala ya ubaguzi wa jinsia na unyanyasaji wa watoto, linakiri tatizo la kamari kwa watoto, na kuwaomba wazazi na wanajamii kutimiza jukumu lao la kuongoza.

Mwongozo wa Kituo cha Amana One Stop kinachoshughulikia kesi kama hizo, Inspekta Christina Onyango, anasema kubeti kwa watoto ni tatizo kubwa ambalo linahitaji jitihada za pamoja kutoka kwa maafisa wa sheria, wazazi na jamii kwa ujumla.

“Ni tatizo kubwa ambalo linafanya baadhi ya watoto washindwe kwenda shule. Kwa kawaida tunakamata waendeshaji wa mashine za kupangia pesa na kuwashtaki mahakamani lakini fahamu kwamba matukio haya hufanyika kwa siri,” anasema Dk Onyango.

“Watoto wetu wanaharibika,” anaongeza, akisema kuwa wanajamii wanapaswa kuripoti matukio kama hayo kwa polisi kwa hatua zaidi.

Kulingana naye, wazazi wanapaswa kufuatilia kwa karibu harakati za watoto wao ili kugundua mapema changamoto zozote.


UKUAJI MICHEZO YA KUBAHATISHA

Kulingana na bodi ya michezo ya kubahatisha, kampuni 91 zilisajiliwa kufanya shughuli tofauti za michezo ya kubahatisha hadi kufikia Juni 2023.

Katika mwaka wa 2022/23, bodi ilipanga kutoa leseni 7,697, ikiwa ni pamoja na leseni 1,923 mpya na 5,774 zilizorejeshwa, kulingana na hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha kwa mwaka wa 2023/24 iliyowasilishwa mwaka jana.

Hata hivyo, hadi kufikia Aprili 2023 bodi ilikuwa imetoa leseni 8,778, ikiwa ni pamoja na 3,658 mpya. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi leseni 11,880 katika mwaka wa 2023/24, anasema Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Sekta hiyo ambayo inaajiri takribani watu 25,000, kulingana na bodi, pia imeongeza mchango wake kwa mapato ya serikali kwa asilimia 407.1 kati ya 2016/17 na 2022/23 kufikia Sh170.4 bilioni.

Mashine hizo zinapatikana wapi, athari yake ni nini kwa kuenea kwa mashine hizo za kamari na viongozi wa dini wanasemaje na hali ipoje kwa mataifa mengine ya jirani? Usikose kesho Jumapili...!