SAID JR Aeleze kilichomwondoa Serbia

Muktasari:
- Mmmoja wao ni Said Khamis na amezunguka timu mbalimbali duniani kucheza soka akitamba eneo la ushambuliaji na aliwahi kupita Mbao FC kwa msimu mmoja mwaka 2019, kabla ya kusajiliwa na Baniyas iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Falme za Kiarabu akianzia timu ya vijana na msimu uliofuata akapandikwa timu kubwa.
NYOTA wengi wanaokipiga nje ya nchi wanatajwa kupita katika timu kubwa za Kariakoo, Yanga na Simba na wachache sana wametokea kwenye timu za kawaida au wameanzia huko na kucheza soka la kulipwa.
Mmmoja wao ni Said Khamis na amezunguka timu mbalimbali duniani kucheza soka akitamba eneo la ushambuliaji na aliwahi kupita Mbao FC kwa msimu mmoja mwaka 2019, kabla ya kusajiliwa na Baniyas iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Falme za Kiarabu akianzia timu ya vijana na msimu uliofuata akapandikwa timu kubwa.
Alicheza katika timu hiyo kwa mwaka mmoja, kisha akajiunga na Hatta huko huko Uarabuni na kabla ya kutolewa kwa mkopo Fujairah alikomaliza akifunga mabao mawili kisha kutimkia Serbia na kujiunga na FK Jedinstvo UB mwaka 2023.
MASILAHI YAMWONDOA SERBIA
Akizungumza na Mwanaspoti mapema wiki hii, mshambuliaji huyo anasema yupo huru baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo akibainisha hakutaka kuendelea kutokana na migogoro ya kimkataba.
"Kwa sasa nipo Dar nasikilizia ofa, si unajua mambo ya soka ni mengi hasa yanapokuja mambo ya kimasilahi, lakini tumepambana nayo na kupata haki zangu," anasema Said Jr ambaye hakutaka kuweka wazi ni changamoto gani za kimasilahi alizokutana nazo lakini tayari amemalizana nao na yupo huru sasa.
"Kabla hata ya mkataba wangu kuisha nilitaka kuhama ile timu lakini ilivyotokea changamoto ya kimasilahi nikaona ndiyo muda sahihi wa kutafuta maisha sehemu nyingine," anasema Said Jr.
"Sehemu yoyote changamoto haziwezi kukosekana hivyo kama mchezaji unapambana kuhakikisha unatatua kwa kuwa sisi tunapitia mambo mengi."
AIPANDISHA LIGI KUU
Anasema timu hiyo ilikuwa ikishiriki Ligi daraja la kwanza msimu uliopita na kuipandisha Ligi Kuu ambayo itaanza kucheza msimu huu.
"Ligi ya Serbia ni ngumu sana tulipambana msimu uliopita kuhakikisha tunacheza Ligi Kuu na tunashukuru hilo ingawa sitakuwa sehemu ya wachezaji msimu ujao."
LIGI ILIVYO
Said anafafanua soka la Serbia ni tofauti na nchi nyingine kwani wanatumia nguvu sana na kama hautaendana na kasi yao unaweza kuambulia benchi.
"Wenzetu nadhani wanatuzidi zaidi kwenye engo ya kiufundi muda mwingi pia wanatumia kutengeneza timu na kisha wanafanyia mazoezini," anasema na kuongeza
"Nilifika Serbia ligi inakaribia mzunguko wa pili kwa hiyo sikupata mechi nyingi lakini nashukuru nimecheza mechi 10 nikafunga mabao matatu na assisti mbili ingawa sikucheza kama straika bali kiungo mshambuliaji."
OFA ULAYA NA ASIA
Baada ya kuondoka Serbia, Said anasema tayari ana ofa mbili kutoka klabu mbalimbali Ulaya na Asia japo hakutaka kuweka wazi ni timu gani.
"Napambana nipate timu moja wapo kulingana na ofa zilizokuja mezani na naamini kwa maandalizi ya mapema niliyofanya nitakuwa bora na kuendeleza kiwango changu."
KUCHEZA TANZANIA
Mshambuliaji huyo tangu aanze kucheza soka la kulipwa mwaka 2019 amecheza timu moja tu Tanzania, Mbao ya vijana iliyopo Mwanza kabla ya kusajiliwa Baniyas ilikuwa inashiriki Ligi za Falme za Kiarabu.
Alipoulizwa kama ana mpango wa kucheza timu za Tanzania kwa sasa alisema mawazo yake yapo kimataifa lakini lolote linaweza kutokea na watu wakamuona akicheza nchini.
"Kwa sasa sina mpango acha nitafute pesa na kukua kwa karia yangu nje lakini inshaallah ikitokea ofa nzuri lolote linaweza kutokea," anasema Said na kuongeza;
"Matarajio yangu ni kufanikisha dili zuri litakalosapoti muendelezo wangu wa kucheza."