Samatta, Msuva wanatembea na mgodi wao

Muktasari:
- Wanasoka wa zamani wameliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji hao wanafanya kazi kubwa na wataacha deni kwa wanaokuja nyuma kufanya makubwa kuwakilisha nchi ili wawe msaada Taifa Stars.
WANASOKA Watanzania wanaocheza nje Mbwana Samatta, Simon Msuva na Himid Mao wanatajwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kulinda viwango na heshima.
Wanasoka wa zamani wameliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji hao wanafanya kazi kubwa na wataacha deni kwa wanaokuja nyuma kufanya makubwa kuwakilisha nchi ili wawe msaada Taifa Stars.
Aliyekuwa beki wa Simba na Stars, Boniface Pawasa anasema ifike mahala Samatta, Msuva na Mao wapewe heshima haijalishi kutosikika mara kwa mara kwa sasa kwani wanaweza kuwa na sababu nyingi nyuma ya pazia.
“Kuna mambo ya mifumo huenda wakati Samatta anang’ara kuna kocha alikuwa anapenda ashambulie zaidi mfano mzuri soka la kocha Jose Mourinho ni kuzuia inaweza ikawa ngumu kung’ara mshambuliaji chini yake,” anasema Pawasa.
“Namkubali sana Msuva hakati tamaa, anapata changamoto anarejea Tanzania anafanya mazoezi akipata timu anakwenda kupambana,” anasema nyota huyo wa zamani.
“Mao asingekuwa na kiwango kizuri asingekaa nje muda wote huo. Kwa wachezaji waliopo nje wanapaswa kupambana kulinda viwango vitakavyofanya majina yao kuwa makubwa, lakini kwa wale waliopo ndani wawe na wivu wa maendeleo wa kutamani kulipwa pesa nyingi kama wenzao waliopo nje.”
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anasema mastaa hao wameonyesha njia kwa vijana wenzao kwamba kila kitu kinawezekana.
“Kuna vipaji vikubwa hapa nchini. Ifikie hatua wawe na wivu wa kutamani changamoto mpya waangalie heshima wanayopata wenzao. Pia watamani kufanya makubwa katika soka waache uvivu na kuridhika mapema,” anasema Mmachinga ambaye rekodi yake ya mabao 26 Ligi Kuu Bara haijavunjwa.
Winga wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garrincha’ anasema Samatta amewaachia mtihani vijana wengi kufanyia kazi aliyofanya nje.
“Kama ilifikia hatua TP Mazembe walimtengenezea sanamu lake ni kwa Sababu ya alichofanya, timu alizopita na alichoonyesha anastahili heshima. Hivyo kutovuma kwa sasa yapo mambo mengi, ipo mifumo ya makocha. Kwa Msuva anapambana sana hakati tamaa anawaonyesha wenzake kwa matendo,” anasema Garrincha.
HALI ILIVYO MASTAA NJE
Samatta, 32, anayecheza Ugiriki hana nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha PAOK Salonika ambapo msimu huu amecheza michezo minne kwa dakika 96 na hajafunga wala kutoa asisti. Mkataba wake unamalizika Juni, mwaka huu.
Kwa mujibu wa takwimu, Samatta ana asilimia sifuri kuanza kwenye kikosi, tano kupata nafasi ya kucheza huku uhusika wake wa mabao ukiwa pia asilimia 0.
Simon Msuva, 31, ndiye mshambuliaji anayepata nafasi ya kutosha ukimtofautisha na Samatta. Nyota huyo wa zamani wa Yanga msimu huu huko Irak akiwa Al-Talaba SC ametumika katika michezo 16 Ligi Kuu akifunga mabao matatu na asisti tatu.
Msuva ana uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza kwa asilimia 94, kutumika dakika 89 na asilimia 43 kuhusika kwenye mabao.
Upande wa Himid, 32, ambaye yupo kwenye kundi la Samatta na Msuva ambao ni kama wanaondoka kwenye soka la ushindani kutokana na umri, bado anakomaa huko Misri akiwa na Talaea El Gaish akitumika michezo saba msimu huu akiwa na uhakika wa kuanza kwa asilimia 70. Msimu huu ana kadi moja ya njano na nyekundu.
Novatus Miroshi ndiye Mtanzania anayecheza soka la ushindani katika kiwango cha juu kwa sasa. Kiraka huyo anayecheza Ligi Kuu Uturuki (Super Lig) akiwa na timu ya Göztepe ameifungia mabao matatu na kutoa asisti moja.
Msimu huu, Novatus mwenye miaka 22, ametumika katika michezo 13 akiwa na uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza kwa asilimia 45, huku akitumika kama beki wa kati, kushoto au kiungo mkabaji na wikiendi iliyopita alifunga katika ligi dhidi Fenerbahce licha ya timu yake kupoteza 3-2.
Haji Mnoga mwenye miaka 22, anafanya vizuri huko England akiwa na Salford inayoshiriki League Two na siku chache zilizopita alicheza dhidi ya Manchester City - moja ya timu kubwa Ulaya katika Kombe la FA ambalo walitolewa kwa kuchapwa mabao 8-0.
Mnoga ambaye baba yake ni Mzanzibari na mama Mwingereza ana uhakika wa kuanza kwenye kikosi cha Salford kwa asilimia 70 na msimu huu ametumika katika michezo 21 ya League Two England kama beki wa kulia akifunga bao moja na kuasisti mara mbili.
Mbali na Haji, Tarryn Allarakhia ni mchezaji mwingine wa Kitanzania anayefanya vizuri England akiwa Rochdale ya National League. Kiungo huyo mwenye miaka 27 amefunga mabao mawili na kuasisti manne akiwa na uhakika wa kuanza kwa asilimia 79 kikosini.
Tofauti na Haji pamoja na Allarakhia ambao angalau ligi zao zinatazamika, Ben Starkie anayecheza ligi ya chini katika michezo ya awali ya Kombe la FA alitoa asisti moja kwenye mechi mbili akiwa na Harborough.
Kwa upande wake Kelvin John ambaye ni mmoja wa wachezaji ambao walikuwa wanatabiriwa makubwa akiwa Denmark kwa sasa ana uhakika kwa asilimia sita kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Aalborg BK.
Msimu huu ametumika katika michezo 13 ya ligi nchini humo ambayo ni maarufu kama Superliga. Hajafunga wala kutoa asisti.
Nyota mwingine Mtanzania, Omary Mvungi anajitafuta n huko Ufaransa mambo yakionekana kuwa magumu kwake akiwa na Wasquehal inayoshiriki Ligi ya National 2 kwa mkopo akitokea Nantes akiwa ametumika katika michezo miwili, hajafunga wala kutoa asisti.
Cyprian Kachwele, 19, ambaye alitua msimu uliopita huko Canada kujiunga na Vancouver Whitecaps akitokea Azam FC ameonyesha kuwa na kitu kiasi cha kupandishwa hadi kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Alianzia kwa vijana ambako alifunga mabao manne katika michezo 20.
Kwa Marekani kuna Bernard Kamungo aliyeishika ligi ya huko akionekana kufanya vizuri akiwa na Dallas kiasi cha kupewa mkataba mpya ambao utatamika Desemba 2027. Bado anaweza kutumika Taifa Stars kwani ni mzaliwa wa Kigoma aliyekulia Marekani.
Msimu uliopita katika michezo 34 ya mashindano yote alifunga mabao matano na kutoa asisti mbili.
Miano van den Bos, 21, kwa sasa yupo zake Sweden akiwa na Orebro Syr. Huyo ni kati wachezaji ambao walionekana kwa mara ya kwanza kwenye Afcon nchini Ivory Coast wakati huo akicheza soka la kulipwa Hispania. Jamaa ni beki wa kulia mwenye uwezo mzuri wa kupanda na kushuka na msimu huu ametumika katika michezo 11 akicheza kwa dakika 841.
Baraka Majogoro ndiye mchezaji pekee wa Kitanzania aliyesalia Afrika Kusini baada ya Abdi Banda na Gadiel Michael kurejea Tanzania. Katika msimu huu ametumika kwenye michezo minane akiwa na uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza kwa asilimia 33 ndani ya Chippa United.