Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba wajanja, cheki walivyowapiga chenga ya mwili Yanga, Azam

Muktasari:

  • Ndio, ukisikia mtu amepigwa chenga ya mwili, hicho ndicho kilichofanywa na mabosi wa Simba kwa msimu huu na kila kinachoonekana kwa sasa ni sapraizi kwa wapinzani.

SIMBA wajanja sana. Walichokifanya katika Ligi Kuu Bara msimu huu unaweza kusema ni ‘danganya toto’.

Ndio, ukisikia mtu amepigwa chenga ya mwili, hicho ndicho kilichofanywa na mabosi wa Simba kwa msimu huu na kila kinachoonekana kwa sasa ni sapraizi kwa wapinzani.

Huenda bado hujaelewa! Hebu tulia kidogo rudi ukurasa wa pili uchungulie msimamo wa Ligi Kuu kwa msimu huu ulivyo. Umegundua nini. Ni wazi umeona namna Simba na Yanga zilivyokabana koo katika mbio za ubingwa.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 58, ilihali Simba ikiwa ya pili ikikusanya pointi 57. Pointi moja tu ndio iliyozitenganisha timu hizo kongwe zilizobaki katika mbio za ubingwa kwa msimu huu, baada ya Azam FC, Singida BS na Tabora United kujiengua kiaina kwa kushindwa kushikilia bomba tofauti na zilivyoanza.

Kwa wanaokumbuka kabla ya kuanza kwa msimu, mabosi wa Simba waliutangazia umma kwamba, usajili uliyofanywa kwa kikosi hicho kujaza zaidi wachezaji wenye umri mdogo na kocha asiyefahamika sana una lengo la kujenga timu.

Uliweka bayana kwamba kikosi chao kinajengwa kwa ajili ya misimu kadhaa ijayo na sio kwa msimu huu na kwa bahati mbaya wapinzani wa Simba wakaingia mkenge. Ilichokifanya Simba ni kama danganya toto kwa wapinzani, kwani hadi kufikia sasa zikiwa zimebaki mechi nane msimu kumalizika imewasapraizi wengi kwa kuipa presha Yanga inayopambana kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Tofauti na kauli za awali kwamba, Simba inajenga kikosi cha ushindani kwa misimu ya mbele na sio msimu huu, kocha Fadlu Davids na jeshi alilonalo Msimbazi, wameonyesha hawatanii katika mbio za ubingwa na sio ajabu Mei 25 mambo yakawa tofauti na matarajio ya wengi, kwani lolote linaweza kutokea na usije ukashangaa kuona Simba akitawazwa kuwa bingwa msimu huu.

Ni kweli Simba na Yanga zinalingana kwa idadi ya michezo iliyocheza hadi sasa katika Ligi, kila moja ikicheza 22, huku kukiwa na kiporo baina yao, kilichoahirishwa Machi 8, hivyo kila moja inapiga hesabu kwanza kwa mechi saba dhidi ya wapinzani wengine kabla ya kuja kumalizana wenyewe kwa wenyewe na hapo maajabu ndio yatatokea.

KWANINI?

Kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, wakati Simba ikiwa inalitolea macho taji la Ligi Kuu Bara, ilikuwa na watu wa maana kikosini waliojitoa kupambana vilivyo na Yanga iliyokuwa chini ya makocha, Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi.

Simba ilikuwa na wachezaji wazoefu na wenye majina makubwa katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla ambapo iliweka heshima katika michuano ya CAF chini ya makocha tofauti waliokuwa na uzoefu na heshima kubwa barani humo.

Hata hivyo, Simba ilichemsha mbele ya Yanga kwani vijana wa Jangwani walibeba mataji mara zote, huku Simba ikimaliza kinyonge.

Msimu wa 2021-22, Simba katika mechi 30, ilishinda mechi 17 pekee, huku 10 zikiisha kwa sare mbalimbali na ikapoteza michezo mitatu na kumaliza msimu ikiwa na pointi 61, huku ikifunga mabao mabao 41 tu na kufungwa 14.

Simba ilimaliza nyuma ya Yanga ambayo ilibeba ubingwa kwa kukusanya pointi 74, ikiwa imeshinda mechi 22 na kutoka sare nane, ikiweka rekodi ya kutopoteza mechi hata moja, ikifunga pia mabao 49 na kufungwa manane tu msimu mzima.

Msimu wa 2022-2023, Simba ikijitutumua na kuchuana na Yanga kwa staili kama ya Ubaya Ubwela na kumaliza msimu huo, ikicheza mechi 30 na kushinda mechi 22, ikitoka sare saba na kupoteza mchezo mmoja tu, huku ikifunga mabao 75 na kufungwa 17, ikiwa na pointi 73.

Hata kama Yanga ilitetea ubingwa, lakini kijasho kiliwatoka kwani ilimaliza msimu kwa tofauti na pointi tano tu dhidi na ilizonazo Simba. Yanga ilimaliza na pointi 78, mabao 61 na kufungwa 18, kupitia mechi 30, ikishinda 25, sare tatu na kupoteza mbili.

Kwa msimu uliopita, hali ya Simba ilikuwa mbaya zaidi, kwani ilimaliza nafasi ya tatu baada ya kuzidiwa ujanja na Azam iliyomaliza ikiwa na pili nyuma ya Yanga iliyotetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo.

Katika msimu huo, ndio ambapo Yanga iliandika historia ya kuinyoosha Simba kwa mabao 5-1 na kumaliza msimu ikikusanya pointi 80 kupitia mechi 30, ikishinda 26, sare mbili na kupoteza mbili.

Simba ilimaliza nafasi ya tatu, baada ya kucheza mechi 30 na kushinda 21, sare sita na kupoteza tatu kama ilivyokuwa kwa Azam FC iliyomaliza ya pili nyuma ya Yanga, lakini zikatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam ilimaliza na mabao 63 ya kufunga na kufungwa 21, wakati Simba ilikuwa na 59 na kufungwa 25 ikiwa ni rekodi mbaya kwao baada ya muda mrefu kuwa na ukuta mgumu uliowabeba katika Ligi Kuu, japo zote zilivuna jumla ya pointi 69.

Matokeo hayo ya kumaliza nafasi ya tatu iliifanya Simba kwa mara ya kwanza baada ya misimu mitano mfululizo nyuma kushindwa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika na kuziachia Azam na Yanga kuicheza michuano hiyo.


KILICHOFUATA

Mabosi wa Simba walionekana kuumizwa na matokeo hayo ya kumaliza nafasi ya tatu na kushindwa kucheza Ligi ya Mabingwa, michuano mikubwa kwa ngazi za klabu barani Afrika na yenye fedha za maana na kupanga mikakati mipya.

Moja ya mikakati ilikuwa ni kukifumua kikosi na kuwatema wachezaji nyota walio wengi na wenye umri mkubwa, ili kuleta damu changa.

Clatous Chama, John Bocco, Saido Ntibazonkiza, Henock Inonga, Saido Kanoute, Babacar Sarr, Willy Onana, Freddy Michael Koublan, Jean Baleke na Pa Omar Jobe walioonekana wameshindwa kuibeba timu hiyo, licha ya awali kubeba matumaini ya Msimbazi.

Fyagio hilo halikuwagusa wachezaji tu, bali lilishuka hadi kuwagusa hadi watu wa benchi la ufundi, kwani wengi walitemwa na kuletwa watu wapya akiwamo Fadlu ambaye amekuwa ni kocha msaidizi katika klabu nyingi alizowahi kuzifanyia kazi.

Fadlu alichukuliwa kutoka Raja Casablanca iliyokuwa imetoka kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco (Batola Pro) kimiujiza ikiizidi ujanja, FAR Rabat iliyokuwa chini ya Nasreddine Nabi aliyeweka heshima kubwa akiwa na Yanga hapa nchini.

Wakashushwa wachezaji wenye umri mdogo na wasio na majina makubwa kuanzia kwa Steven Mukwala, Leonel Ateba, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Omar Omar na Valentino Mashaka.

Pia kuna Moussa Camara, Abdulrazaq, Chamou Karabou, Valentin Nouma, Awesu Awesu kabla ya kuja kuongezwa kwa Ellie Mpanzu kupitia dirisha dogo ambao waliungana na vijana wengine waliobakishwa kikosini akiwamo Ally Salim, Ladack Chasambi na Edwin Balua waliokuwa wameingia kupitia dirisha dogo la msimu uliopita.


UPEPO UMEBADILIKA

Wekundu wanautaka ubingwa kiubaya ubwela, tofauti na zile kauli mbiu kwamba Simba ya Fadlu inajengwa na kuwa msimu huu wapo kuipa timu uzoefu kwanza.

Kauli ya “kujenga timu” ilisisitizwa kwa vitendo katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga wakati Simba ikilazwa bao 1-0 lililofungwa na Maxi Nzengeli katika dk44 na kung’oka ikishindwa kwenda fainali kucheza na Azam FC.

Mashabiki na wapenzi waliishangilia timu na kuipongeza kwa kufungwa bao 1-0, kwani hofu yao kwa mziki wa Yanga ya Gamondi iliyotoka kuinyoa msimu uliopita kwa jumla ya mabao 7-2, ikianza na zile 5-1 kisha 2-1 ziliporudiana huku Simba ikikimbizwa mwanzo mwisho, hivyo kipigo cha 1-0 katika mechi hiyo ya Ngao waliona ni nafuu sana.

Hata hivyo, ukweli huo ulikuwa ni mtego na wapinzani wa Simba katika Ligi Kuu na hata kimataifa, ikiwamo Yanga kwani hivi sasa upepo umebadilika.

Simba ndio timu pekee ya Tanzania iliyosalia katika michuano ya kimataifa, ikiwa hatua ya robo fainali ikijiandaa kuvaana na Al Masry ya Misri, lakini hata katika Ligi Kuu, ipo nafasi ya pili nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi moja tu.

Ndio, Yanga ina pointi 58 zilizotokana na michezo 22, ikishinda 19, ikipata sare moja na kupoteza michezo miwili mbele ya Azam FC na Tabora United, huku timu hiyo ikifunga mabao 58 na kufungwa tisa hadi sasa.

Simba katika nafasi ya pili iliyopo imevuna pointi 57 kupitia mechi 22, ikishinda 18, sare tatu na kupoteza mara moja tu dhidi ya Yanga iliyowafunga 1-0 katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Oktoba 19 mwaka jana, beki Kelvin Kijili akijifunga jioooni.

Timu hiyo, pia imefunga mabao 52 katika mechi 22, huku ikiwa ndio timu yenye ukuta mgumu, kwani imeruhusu mabao manane tu, huku ikiwa na mechi nane mkononi kama watani wao, ikiwamo kiporo cha Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8.

Ukiangalia kwa idadi ya mechi ilizocheza hadi sasa na pointi ilizovuna sambamba na mabao iliyofunga na kufungwa, ni wazi Simba imefanya vizuri zaidi kulinganisha na msimu uliopita na hadi msimu ukimalizika mambo yanaweza kuwa tofauti zaidi.

Kuanzia ushindi iliyopata msimu huu kupitia mechi 22 tu unawasha taa ya kijani kulinganisha na msimu uliopita ambapo ilishinda 21 katika mechi 30, wakati hadi sasa imeshinda 18 kupitia mechi 22 tu.

Sare ilizopata hadi sasa ni tatu ikiwa ni pungufu kwa zile zilizopata msimu msimu mzima ambapo zilikuwa ni sita, lakini hata idadi ya mechi ilizopoteza hadi sasa ni chache zaidi kulinganisha na msimu wa 2023-24 ilipopoteza tatu. Msimu huu imepoteza moja tu.

Pointi ilizonazo kwa sasa (57) kupitia mechi 22, zinatoa matumaini makubwa kwa timu hiyo kumaliza na idadi kubwa zaidi kulinganisha na zile 69 za msimu uliopita ilipomaliza mechi 30 za msimu. Pointi 57 ilizonazo sasa ni pungufu ya 12 na zile ilizokusanya msimu mzima ilipomaliza nafasi ya tatu.

Licha ya kwamba mbio za ubingwa bado zipo wazi hadi sasa na ngumu kwa yeyote kutabiri, lakini tayari Simba imejiweka katika nafasi ya kumaliza nafasi mbili za juu tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita na hivyo kuwa na uhakika wa kurejea tena katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.

Pia imeithibitishia Yanga kwamba ile kauli ya kwamba timu ya sasa inajengwa na sio ya kuwania ubingwa, ilikuwa ni DANGANYA TOTO na isipokaa vizuri sio ajabu ikatema taji la Ligi Kuu msimu huu na hata katika michuano ya Kombe la Shirikisho, zote zikiwa hatua ya 16 Bora zikijiandaa kucheza na timu za Ligi ya Championship. Yanga ikipangwa kukutana na Songea United na Simba kuvaana na BigMan (zamani Mwadui). Nini kitatokea Mei 25 Ligi ikifikia tamati? Tusubiri tuone!