Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sungu Mtata 'ndondo' za ngumi mtaani zinavyomtoa

Muktasari:

  • Sungu Mtata huenda unapokutana naye mtaani kama hujaambiwa ni bondia, basi siyo rahisi kukubali kutokana na nidhamu ya upole ambayo amekuwa nayo hata mwonekano wake licha ya kuwa na mwili uliojazia kwa mazoezi.

KUTOKA Kibiti hadi Ikwiriri Mkoa wa Pwani, ndiyo mitaa ambayo bondia chipukizi wa ngumi za kulipwa kwenye uzani wa Super Walter, Ramadhan Mkwakwate maarufu zaidi kama Sungu Mtata ndiko anakotokea.

Sungu Mtata huenda unapokutana naye mtaani kama hujaambiwa ni bondia, basi siyo rahisi kukubali kutokana na nidhamu ya upole ambayo amekuwa nayo hata mwonekano wake licha ya kuwa na mwili uliojazia kwa mazoezi.

Bondia huyo Aprili 26, mwaka huu, anatarajia kupanda ulingoni katika Pambano la Ngumi Kitaa chini ya menejimenti inayomsimamia ya Mitra Sports Prommotion litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar.

Sungu Mtata mwenye rekodi ya kucheza mapambano 11 ya ngumi za kulipwa akiwa ameshinda manane kati ya hayo matano kwa Knockout, pia amepigwa mara mbili huku akitoka sare moja.

Bondia huyo wa uzani wa superwalter, anakamata nafasi ya kwanza katika mabondia 27 wa uzani huo hapa nchini wakati duniani ni bondia wa 348 kati ya mabondia 2201.

Mpaka sasa ametumia raundi 46 ikiwa kila raundi ina dakika tatu pekee za kupigana katika mapambano 11 aliyofanikiwa kucheza kabla ya pambano lake la Aprili 26, mwaka huu.

Bondia huyo amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti ambapo amefichua safari yake katika mchezo wa ngumi ilivyoanza, huku ikichangiwa na kaka yake aliyekuwa anakwenda Ikwiriri mara kwa mara akimuona anafanya mazoezi ya mchezo huo.

"Unajua huko nyuma sikuwahi kuwa na mpango wa kutaka kuwa bondia kabisa kwa sababu nilikuwa najishughulisha na shughuli za ufundi wa ujenzi na uchimbaji wa visima vya maringi kupitia kaka zangu. Lakini kuna kaka yangu mmoja anaitwa Kinole, alikuwa anaishi Dar ila mara kwa mara alikuwa anakuja Ikwiriri kwa shughuli zake binafsi lakini wakati huohuo akawa anafanya mazoezi ya ngumi, nikawa namuona.

"Sasa ile hali kusema ukweli ikawa inanivutia kutaka kufanya mazoezi, nakumbuka kuna siku nilimuomba niamshe naye mazoezi kweli akaniamsha kufanya mazoezi, ile hali iliendelea ila anapokuwa amerejea Dar huwa nalazimika kusimama hadi anaporejea yeye kwa sababu nilikuwa sijui chochote.

"Katika kipindi hicho nafanya mazoezi ndiyo nilianza kucheza mapambano ya mtaani yaani kama vile kwenye mpira wanasema ndondo kwa sababu ilikuwa inafungwa kamba chini unakuwa ulingo halafu zinapigwa.

"Kaka yangu alikuwa akicheza ngumi za ridhaa wakati mwingine anakuja Ikwiriri kwa ajili ya mabonanza ambayo ndiyo sehemu nilianza kupigana baada kuambiwa nikapigane ila nilifanya mazoezi, pambano nikapigwa.

"Wakati huo watu waliokuwa wakiniona napigana walikuwa wakisema kwamba naweza sitakiwi kuacha ila kupigwa ilitokana kuwa sehemu ya mchezo kutokana na kusema sikuwa na upepo wa kutosha.

"Nikapata pambano lingine, nikashinda na baada ya hapo ngumi zikawa zimeingia kwenye damu na mashabiki wakawa wananikubali sana ila changamoto tukawa tunafanya mazoezi hatuna mwalimu wala nini lakini tukawa tunaendelea kucheza mabonanza.

"Baadaye nilipata nafasi ya kuja kuishi Dar nikawa nikipata nafasi ya kwenda kucheza bonanza halafu narejea Dar.

Swali: Ulikuwa unalipwa kiasi gani kwenye bonanza moja

Jibu: "Kiukweli malipo yalikuwa kawaida sana maana kuna wakati unapewa shilingi 40,000 au 50,000 wakati mwingine chakula na nauli, yaani tunaenda tunacheza halafu inakuwa sawa tu.

"Sasa nakumbuka miaka minne au mitatu nyuma, Mitra wakaanda pambano Kibiti, kuna mzee wetu mmoja anaitwa Matimbwa alimpigia Said Hofu ambaye ni Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa 'JKT' aniombee nicheze kwenye pambano waliokuwa wameandaa.

"Alimwambia ana kijana wake ambaye ni mimi, anaitwa Sungu Mtata ananiombea nicheze hilo pambano.

"Basi nilipewa pambano nicheze na Sebastian Deo, nilicheza vizuri bila shida halafu wakanipa pambano lingine ambalo nilitakiwa nicheze na Kenedy Ayoo, kwa bahati mbaya Ayoo aling'atwa na mbwa nikapewa mtu mwingine ambaye pia nilifanya vizuri.

"Sasa baada ya lile pambano, Hofu alivutiwa na uwezo wangu akanishawishi nijiunge na menejimenti yao kwa sababu Mitra ilikuwa inatafuta mabondia ambao watakuwa chini yake.

"Kutoka hapo ndiyo nikawa chini yao kwa sababu ngumi bila ya kuwa na mtu anayekushika mkono huwezi kutoboa kwenda popote kabisa."

Swali: Jambo gani gumu ambalo umeshakutana nalo kwenye ngumi?

Jibu: "Mambo mengi magumu yanatokea kwa sababu huu ni mchezo lakini jambo kubwa gumu ambalo nimekutana nalo ilikuwa kwenye pambano langu na Amiri Matumla, mtoto wa Rashid Matumla.

"Kwanza pambano lilikuwa jepesi halafu likawa gumu kwa sababu baada ya lile pambano ambalo nilipoteza nikatokwa na mapele na vidonda, nikaumwa kama wiki hivi.

"Sikujua kama ni mambo ya kishirikina au upepo mbaya ulipita kwangu, ukweli niliumwa sana na ndiyo pambano lilinipa changamoto kubwa."

Swali: Ulishawahi kupigwa ngumi ukatamani kuachana na mchezo huo?

Jibu: "Hapana, hilo halijawahi kutokea isipokuwa  kupigwa ngumi halafu ukalewa hilo ni jambo la kawaida maana kila unayecheza naye anakuwa na ujuzi wake maana kuna wakati unapigwa ngumi unaona mawasiliano yamekatika lakini mtu unakaza na kuendelea kupigana."

Swali: Wewe kama bondia unakula kiasi gani?

Jibu: "Unajua uzani ambao nacheza ni mkubwa hivyo suala la kula ni muhimu, nakula nusu au nusu na robo ya ugali, wali siyo sana kabisa.

"Hiyo nusu na robo au nusu huo ni mlo mmoja ingawa hiyo nusu na robo mara nyingi kama nakuwa na pambano la kutakiwa kuongeza kilo zangu yaani kupanda uzito lakini kama la kawaida basi huwa na nusu kilo ya ugali peke yangu."

Swali: Sasa hivi nje ya ngumi unafanya nini?

Jibu: "Naendelea na shughuli zangu za uchimbaji wa visima pamoja ujenzi wa nyumba na mara nyingi nakuwa na kaka yangu maana yeye ndiye aliyenifundisha."

Swali: Tangu uanze kucheza ngumi umelipwa pesa nyingi kiasi gani?

Jibu: "Kiukweli kiasi kikubwa cha pesa ambacho nimewahi kulipwa mpaka sasa ilikuwa ni Sh1 milioni ambayo nilifanyia mambo mbalimbali ya nyumbani."

Swali: Una malengo gani baadaye katika ngumi za kulipwa?

Jibu: "Unajua siyo rahisi kusema ambacho haujakipata na mimi nipo hivyo maana naweza kusema halafu nikawa siwezi kufikia lakini jambo kubwa kwangu katika kipindi hiki ni kuangalia pambano langu la Aprili 26 pale Dar Live ili nishinde."