Ushauri kwa Arteta, mabosi Arsenal!
Muktasari:
- Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kubwa mno na ina maana kubwa sana. Arsenal walikaribia kutimiza ndoto ya kila mchezaji katika kikosi hicho ya kuwa mabingwa wa Ulaya. Lakini hawakufanikiwa.
LONDON, ENGLAND: Mabadiliko ambayo Arsenal wanapaswa kufanya ili kupiga hatua Inayofuata baada ya kushindwa katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya timu yake kushindwa kutoa tamko kubwa lililohitajika, Mikel Arteta alionekana kuwa amekuwa akitafakari ujumbe tofauti wa kutoa. Kwanza alihitaji kupata maneno sahihi ya kuwaambia wachezaji wake.
Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kubwa mno na ina maana kubwa sana. Arsenal walikaribia kutimiza ndoto ya kila mchezaji katika kikosi hicho ya kuwa mabingwa wa Ulaya. Lakini hawakufanikiwa.
Kulikuwa na fahari, lakini pia maumivu makubwa kama Arteta alivyoeleza. Kwa kawaida, alizungumza kuhusu kutumia maumivu hayo kama "mafuta" ya mafanikio ya baadaye, jambo ambalo Arsenal wamekuwa wakifanya mara kwa mara chini ya uongozi wake.
Baada ya kumaliza nafasi ya tano msimu wa 2021-22 kufuatia kipigo dhidi ya Tottenham 3-0, walijibu kwa kuingia katika mbio za ubingwa. Baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo walifanikiwa hatimaye kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ulioisha.
Lakini kwa sasa ili kuwa mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu, Arteta anajua Arsenal wanahitaji kuwa wakali zaidi hasa katika safu ya ushambuliaji.
UJUMBE WAKE KWA WAMILIKI
Mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo dhidi ya PSG haukuwa tu kuhusu kujifunza kutokana na kushindwa, lakini ulikuwa ujumbe kwa viongozi na wamiliki wa klabu.
Sifa alizomimina kwa PSG zilionekana kuwa na maana kubwa. "Kwa maoni yangu, wao ndiyo timu bora zaidi duniani," alisema Arteta na kuongeza:
"Wanachoweza kufanya wakiwa na mpira pamoja na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, sijawahi kuona. Wanakulazimisha kucheza namna ambayo hukupanga kucheza."
Muhimu zaidi, Arteta alizungumza mara kadhaa kuhusu Arsenal kuhitaji "kuboresha kiwango na kufikia daraja jingine" pamoja na "kutatua tofauti ndogondogo zitakazoleta matokeo wanayotaka."
Kwa lugha rahisi, Arsenal wanahitaji washambuliaji bora zaidi.
PSG WANA KILE ARSENAL HAWANA
Arteta anaelewa kwamba PSG wana washambuliaji wa kiwango cha juu wanaoweza kubadilisha mchezo kwa sekunde chache. Mfano mzuri ni Khvicha Kvaratskhelia, ambaye alisababisha penalti ya kusawazisha licha ya kutokuwa katika kiwango chake bora.
Washambuliaji wa aina hiyo wanaweza kuamua mechi kubwa kwa muda mfupi. Kwa sasa, Arsenal hawana mshambuliaji wa kiwango hicho.
MPANGO ARSENAL ULIKUWA SAHIHI?
Licha ya lawama kuhusu mtindo wa kujihami katika fainali hiyo, ukweli ni kwamba hakuna timu nyingine iliyoweza kuizuia PSG kwa kiwango kile katika mechi kubwa za Ligi ya Mabingwa.
PSG walifunga mabao manane dhidi ya Chelsea, sita dhidi ya Bayern Munich na nne dhidi ya Liverpool.
Lakini, dhidi ya Arsenal walipata shida kubwa kutengeneza nafasi za wazi.
Kwa kiasi kikubwa, mpango wa Arteta ulifanya kazi, lakini tatizo lilikuwa penalti iliyotolewa na Cristhian Mosquera baada ya kufanya kazi nzuri kwa muda mwingi wa mchezo. Hata hivyo, hali hiyo pia ilionyesha tofauti ya ubora wa washambuliaji wa PSG.
Baada ya Kai Havertz kuipa Arsenal uongozi, PSG walionekana kuwa na hofu, na wakati Kvaratskhelia na Ousmane Dembele walipotolewa nje, PSG hawakuwa tena tishio kubwa kama mwanzoni. Hapo ndipo kunaweza kuwa na majuto kwa Arsenal.
Labda walipaswa kusukuma mbele zaidi mashambulizi na kujaribu kutawala mchezo badala ya kuendelea kujilinda kwa kiwango kikubwa. Lakini, kufanya hivyo kunahitaji kujiamini zaidi na ubora mkubwa wa kiufundi katika safu ya mbele.
Tatizo la mwisho kwa kikosi cha Arsenal ni kukosa makali ya ushambuliaji ingawa Havertz alifunga bao, lakini nje ya hilo, Arsenal hawakuwa na ubora wa kutosha katika eneo la mwisho.
Bukayo Saka alipoteza mipira kadhaa karibu na eneo la hatari. Gabriel Martinelli, Eberechi Eze na Noni Madueke waliharibu pasi rahisi wakati nafasi nzuri za kushambulia zilipojitokeza.
Kwa mara nyingine tena, Arsenal walionekana kukosa "muuaji" mbele ya lango. Katika mechi kubwa kama fainali ya Ligi ya Mabingwa, tofauti kati ya ushindi na kushindwa mara nyingi ni uwezo wa kutumia nafasi chache zinazopatikana.
Pamoja na hayo, kwa miaka kadhaa iliyopita, Arteta amejenga timu imara kwa kuwekeza zaidi katika safu ya ulinzi na kuongeza upana wa kikosi. Mkakati huo uliwasaidia kushinda Ligi Kuu England.
Lakini, kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya kunahitaji kitu kingine zaidi. Inahitajika washambuliaji wenye uwezo wa kuamua mechi peke yao. Kwa sasa, safu ya ushambuliaji inayojumuisha Martinelli, Madueke na Viktor Gyokeres bado haionekani kuwa katika kiwango kinachohitajika kushinda fainali dhidi ya timu kama PSG.
Hatua Inayofuata kwa Arsenal sasa ni kukiri udhaifu eneo al mwisho. Arsenal ni timu kubwa, imara na mabingwa wa England, lakini kuwa mabingwa wa Ulaya wanahitaji kuwa timu iliyokamilika zaidi.
Arteta anatambua hilo na anapaswa kuongeza ubora wa washambuliaji, ubunifu zaidi katika mfumo wa ushambuliaji,
kupunguza utegemezi wa kujihami kupita kiasi na kuipa timu uhuru zaidi wa kushambulia katika mechi kubwa.
Kwa kifupi, safari ya Arsenal haijaisha. Wameshinda ubingwa wa England na sasa changamoto kubwa ni kugeuka kutoka kuwa timu bora ya ndani ya nchi hadi kuwa bora Ulaya.
Na ili kufikia hilo, Arteta atalazimika kubadilisha gia kwa wachezaji na falsafa yake ya soka.