Kumbe Gabriel alitaka mwenyewe
Muktasari:
- Ilikuwa mwisho wa kusikitisha kwa beki huyo katika fainali yake ya kwanza ya mashindano ya Ulaya. Penalti yake iliyopaa juu ya lango ndiyo iliyoamua hatma ya Arsenal ikipoteza katika mikwaju ya penalti na PSG ikifanikiwa kutetea taji lao.
LONDON, ENGLAND: PICHA iliyosambaa zaidi baada ya Arsenal kupoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa ya Gabriel akiwa ameshika kichwa kwa mikono huku akifarijiwa na nahodha wa Paris Saint-Germain na Mbrazili mwenzake, Marquinhos.
Ilikuwa mwisho wa kusikitisha kwa beki huyo katika fainali yake ya kwanza ya mashindano ya Ulaya. Penalti yake iliyopaa juu ya lango ndiyo iliyoamua hatma ya Arsenal ikipoteza katika mikwaju ya penalti na PSG ikifanikiwa kutetea taji lao.
Kwa mchezaji ambaye mara nyingi amekuwa na mchango kubwa kwa Arsenal msimu huu, huu haukuwa mchango ambao angeutarajia kabla ya fainali ya kwanza ya klabu hiyo katika Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2006.
Ilikuwa penalti ya kwanza kwa Gabriel kupiga akiwa Arsenal, huku kocha Mikel Arteta akifichua kuwa beki huyo alikuwa “amejiandaa na kufanya mazoezi kwa ajili ya wakati huu.”
“Alitaka kuipiga,” amesema Arteta. “Kwa kawaida wapigaji penalti ni Bukayo Saka, Martin Odegaard na Kai Havertz. Lakini tulijua kama mchezo ungeenda dakika za nyongeza na penalti, wachezaji wengine wangepaswa kujitokeza.”
Ilikuwa njia yenye maumivu kwa mmoja wa wachezaji bora wa Arsenal msimu huu kumaliza kampeni yake.
Beki wa zamani wa Arsenal, Matt Upson amesema ilikuwa “moja ya zile nyakati za John Terry”, akirejelea fainali ya Ligi ya Mabingwa ya mwaka 2008 ambapo nahodha wa Chelsea, Terry alipata nafasi ya kuipa timu yake ubingwa katika mikwaju ya penalti, lakini akateleza wakati akipiga mpira, ambao uliishia kugonga mwamba huku Manchester United ikitwaa taji.
“Nimekosa maneno ya kumuelezea kama mtu na kama mchezaji”
Usiku huo ulianza vizuri sana kwa Arsenal.
Dakika ya sita tu ya mchezo, Kai Havertz alipiga shuti kali lililoingia juu kabisa ya nyavu na kuwafanya mashabiki wa Arsenal waliokuwa kwenye Uwanja wa Puskas Arena mjini Budapest kuamini ndoto yao ilikuwa ikitimia.
Licha ya PSG kumiliki mpira kwa muda mrefu, walishindwa kutengeneza nafasi nyingi za wazi kwa washambuliaji wao hatari Khvicha Kvaratskhelia, Ousmane Dembele na Desire Doue, huku safu ya ulinzi ya Arsenal ikiwadhibiti kwa kiwango kikubwa.
Moyo wa ulinzi huo alikuwa Gabriel. Beki huyo alifanya uondoaji wa mipira 13, zaidi ya mchezaji mwingine yeyote uwanjani, wakati Arsenal ikisaka mafanikio adimu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa katika msimu mmoja.
Hata hivyo, baada ya Dembele kusawazisha kwa penalti, mchezo ukawa wa tahadhari kubwa kwa timu zote mbili. Hakukuwa na nafasi nyingi za wazi huku mvutano ukiongezeka na mchezo kuelekea kwenye mikwaju ya penalti.
PSG walipata faida mapema baada ya Eberechi Eze kukosa penalti yake kwa kupiga nje. Lakini kipa wa Arsenal, David Raya alirejesha matumaini kwa kuokoa penalti ya Nuno Mendes.
Baada ya mikwaju minne kufungwa kwa mafanikio, hakukuwa na nafasi ya kuokolewa kwa Gabriel ambaye alipiga penalti yake juu ya lango na kuelekea kwa mashabiki wa PSG waliokuwa wakishangilia kwa furaha.
“Kukosa penalti katika fainali ya Ligi ya Mabingwa si jambo zuri,” amesema kiungo wa Arsenal, Declan Rice.
“Lakini tunapendana na tuko pamoja nao. Haya hutokea kwenye soka. Hawatakuwa wachezaji wa mwisho kukosa penalti katika fainali.
“Kila mtu amewahi kukosa penalti, na bila hawa wawili msimu huu tusingeshinda Ligi Kuu England.
“Gabriel, nimekosa maneno ya kumuelezea kama mtu na kama mchezaji. Eze pia amefunga mabao muhimu sana kwetu msimu huu.
“Hii ndiyo soka. Ni mchezo wenye ukatili wakati mwingine. Tunachukua mazuri na kuendelea mbele.”
Arsenal isingefika hapa bila Gabriel
Taswira ya Gabriel akifuta machozi huku wachezaji wa PSG wakisherehekea kombe ni jambo ambalo mashabiki wa Arsenal hawatasahau kirahisi.
Mbrazili huyo, ambaye alikuwa mmoja wa usajili wa kwanza wa Arteta baada ya kuchukua timu mwaka 2019, amekuwa nguzo muhimu katika kurejea kwa Arsenal kileleni mwa soka la England na mafanikio yao ya msimu huu.
Alianza michezo 48 kati ya 63 ya Arsenal katika mashindano yote na alichangia mabao na pasi za mabao tisa, idadi kubwa kuliko ya Odegaard na Gabriel Jesus.
Ingawa mashabiki wa timu pinzani wanaweza kukumbuka penalti yake aliyokosa Budapest, mashabiki wa Arsenal watakumbuka mara nyingi alipoibeba timu hiyo mabegani mwake, ikiwemo bao la ushindi la dakika ya 96 dhidi ya Newcastle United mwezi Septemba.
Beki wa zamani wa Manchester City, Nedum Onuoha, amesema:
“Gabriel amekuwa muhimu kwa Arsenal msimu huu na katika miaka ya hivi karibuni. Kwa hiyo kuona yeye ndiye anayekosa penalti iliyowagharimu ubingwa wa Ligi ya Mabingwa ni jambo la kusikitisha.
“Lakini naamini kila mtu atakuwa upande wake kwa sababu Arsenal wasingeshinda Ligi Kuu bila yeye. Amekuwa mchezaji wa thamani kubwa sana na anastahili kutajwa katika kinyang'anyiro cha tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya PFA.
“Shinikizo katika mikwaju ya penalti huwa kubwa. Unaweza kufanya mazoezi mara nyingi mazoezini, lakini huwezi kujiandaa kikamilifu kwa wakati kama huu wa fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kwa bahati mbaya, amepitia kile ambacho kila mchezaji anaogopa, kukosa penalti ya kuamua bingwa.”
Upson aliongeza: “Hii ni moja ya nyakati zitakazokumbukwa kwa miaka mingi. Ni pigo kubwa kwa mchezaji ambaye amekuwa mwamba wa ulinzi wa Arsenal.
“Gabriel alijitolea kwa kila kitu kwa ajili ya timu yake. Alionyesha ujasiri na moyo wa kuwajibika kwa kujitokeza kupiga penalti, na hilo ndilo jambo pekee unaloweza kuomba kutoka kwa mchezaji.
“Inasikitisha sana kwake, lakini anaonekana kuwa mtu ambaye atarejea haraka na kutumia tukio hili kama motisha. Bado ana majukumu makubwa mbele yake akiwa na timu ya taifa ya Brazil.”
Kwa usiku mmoja, Gabriel alikuwa sura ya majonzi ya Arsenal. Hata hivyo, hilo halipaswi kufuta ukweli kwamba alikuwa mmoja wa sababu kuu zilizoifanya Arsenal kufika hatua hiyo ya fainali.