Rafael Leao airahisishia kazi Manchester United
Muktasari:
- Nyota huyo wa Ureno alisema alianza kuifuatilia United tangu akiwa mdogo kutokana na ushawishi mkubwa wa Cristiano Ronaldo ambaye amekuwa mchezaji wake wa kuigwa kwa muda mrefu.
WINGA nyota wa AC Milan, Rafael Leao, ameongeza moto kwenye tetesi za kujiunga na Manchester United baada ya kukiri ndiyo timu anayoipenda zaidi England.
Nyota huyo wa Ureno alisema alianza kuifuatilia United tangu akiwa mdogo kutokana na ushawishi mkubwa wa Cristiano Ronaldo ambaye amekuwa mchezaji wake wa kuigwa kwa muda mrefu.
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka barani Ulaya, hasa wakati ambapo mustakabali wake katika kikosi cha Milan unaendelea kuwa wa mashaka.
Rossoneri walishindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, jambo lililoathiri mapato ya klabu na kuongeza presha kwa viongozi kutafuta njia za kuboresha hali ya kifedha.
Kutokana na mazingira hayo, Milan inaweza kulazimika kuuza baadhi ya nyota wake wakubwa, huku Manchester United ikitajwa miongoni mwa klabu zinazofuatilia kwa karibu hali ya Leao dirisha la usajili la kiangazi.
Joao Palhinha
JOAO Palhinha yuko tayari kupunguza mshahara wake ili kurejea Sporting CP katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi. Kiungo huyo wa Bayern Munich aliyekuwa kwa mkopo Tottenham Hotspurs anaonekana kutanguliza mapenzi yake kwa klabu iliyomlea. Sporting inamwona kama mbadala sahihi wa Morten Hjulmand anayetarajiwa kuondoka dirisha hili la usajili, huku mazungumzo ya awali ya kurejesha nyota huyo yakidaiwa kuendelea.
Julian Alvarez
JULIAN Alvarez ameendelea kuhusishwa na kuondoka Atletico Madrid baada ya klabu hiyo kuripotiwa kuwa tayari kusikiliza ofa kubwa kwa ajili yake. Mabosi wa Atletico wanataka kupata fedha za kufanya maboresho makubwa kikosini ikiwamo kuwafuata Bernardo Silva na Cristian Romero. Hatua hiyo imeongeza sintofahamu kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo wa Argentina, ambaye pia anatakiwa na miamba ya La Liga, Barcelona.
Nathaniel Brown
NATHANIEL Brown ameongeza nguvu kwenye tetesi za kujiunga na Bayern Munich baada ya kukiri mwenyewe kuhitajika na mabingwa hao wa Bundesliga. Beki huyo wa Eintracht Frankfurt mwenye miaka 22 amekuwa katika kiwango bora msimu huu na kuvutia macho ya vigogo mbalimbali. Bayern inatajwa kumwona kama mrithi wa Alphonso Davies ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha katika misimu ya hivi karibuni.
Arijon Ibrahimovic
KIUNGO na beki wa Bayern Munich, Arijon Ibrahimovic anaendelea kuwaniwa na klabu kadhaa baada ya kumaliza mkopo wake Heidenheim. Hata hivyo, Bayern Munich bado haijaamua kama itambakiza kikosini au itamtoa kwa mkopo mwingine. Augsburg, Werder Bremen, Hoffenheim na Stuttgart zimeonyesha nia ya kumsajili, huku Brighton, Crystal Palace, Fulham na PSV Eindhoven nazo zikifuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Josko Gvardiol
BEKI wa Bayer Munich, Josko Gvardiol ameibuka kuwa mmoja wa mabeki wanaowindwa zaidi Ulaya baada ya Barcelona kuonyesha nia ya kumsajili kutoka Manchester City. Hata hivyo, Bayern Munich nayo inatajwa kufuatilia kwa karibu hali yake. Vigogo hao wa Hispania wanaamini beki huyo wa kimataifa wa Croatia anaweza kuwa sehemu muhimu ya mipango yao ya kuimarisha safu ya ulinzi.
Robert Lewandowski
ROBERT Lewandowski ameanza kuhusishwa na Manchester United baada ya nguli wa klabu hiyo, Rio Ferdinand, kuishauri timu hiyo kumsajili. Ferdinand anaamini mshambuliaji huyo wa Poland bado ana uwezo mkubwa wa kuisaidia United na kuwa mfano kwa vijana wa kikosi hicho. Mustakabali wake Barcelona unaendelea kuzua mijadala katika soko la usajili.
Piero Hincapie
PIERO Hincapie ameibuka kwenye rada za Barcelona huku Kocha Hansi Flick akitafuta beki wa kushoto wa kati. Nyota huyo wa Bayer Leverkusen anatajwa kuwa na sifa zinazolingana na mfumo wa Barca, lakini Arsenal inaonekana kuwa mbele katika mbio hizo kutokana na kuwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja. Hilo limeongeza ushindani wa usajili wake.