Viwalo vya pesa hivi hapa, timu zinazovalishwa jezi za bei mbaya EPL

Muktasari:
- Liverpool na kampuni hiyo ya adidas zimesaini mkataba wa miaka mitano utakaoanza Agosti 1 mwaka huu, wakiibadili kampuni nyingine ambao ni mahasimu wao, Nike.
LIVERPOOL, ENGLAND: DILI jipya la Liverpool la Pauni 300 milioni walilosaini na kampuni ya adidas kwa ajili ya kutengeneza jezi zao linatajwa kuwa moja ya dili tamu kabisa lililowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England.
Liverpool na kampuni hiyo ya adidas zimesaini mkataba wa miaka mitano utakaoanza Agosti 1 mwaka huu, wakiibadili kampuni nyingine ambao ni mahasimu wao, Nike.
Kwenye dili hilo, kampuni hiyo ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya Ujerumani itailipa Liverpool Pauni 30 milioni kwa msimu, pamoja na ziada ya asilimia 20 kwenye mauzo ya jezi na skafu za klabu hiyo na kufanya dili hilo kufikia Pauni 60 milioni kwa mwaka.
Liverpool itamaliza miaka yake mitano ya Nike na kurudi kwa adidas, ambayo pia inatengeneza jezi za miamba mingine kwenye Ligi Kuu England, Arsenal na Manchester United.
Kutokana na dili hilo la Liverpool ni klabu gani kwenye Ligi Kuu England imenasa dili safu la mkwanja mrefu kutoka kwa watengenezaji wa jezi zao? Mwanaspoti linakupa uhondo wote.

10 - West Ham (Umbro, Pauni 7 milioni)
Umbro itabaki kuwa kwenye kumbukumbu kubwa ya West Ham United katika mafanikio yao kama wadhamini wao wa jezi baada ya kushinda ubingwa wa Europa Conference League mwaka 2023. Klabu hiyo ya London Mashariki ilisaini dili la Umbro mwaka 2015 na iliripotiwa kuongeza muda wake miaka michache iliyopita. Mwaka 2020, West Ham ilitangaza kuwa na dili refu na kampuni hiyo ya mavazi ya michezo na inailipa klabu hiyo ya Ligi Kuu England, Pauni 7 milioni kwa mwaka.

9 - Aston Villa (adidas, Pauni 17 milioni)
Aston Villa ilitangaza dili lake la kwanza la adidas mwaka jana wakati klabu hiyo inayonolewa na Mhispaniola, Unai Emery kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya kumalizana na Castore, ambayo ililalamikiwa na wachezaji wa timu hiyo, kitambaa chake kilikuwa kinawafanya kutoka sana jasho, hatimaye miamba hiyo ya Villa Park iliingia dili safi na adidas, ambalo linaingizia timu hiyo mkwanja mrefu, Pauni 17 milioni kwa mwaka.

8 - Everton (Castore, Pauni 20milioni)
Kocha David Moyes amekuja kurudisha hali ya mambo kuwa nzuri Everton na sasa miamba hiyo inatarajia kuhamia kwenye uwanja mpya, lakini ikiendelea kutamba na watengeneza jezi wao, Castore. Kampuni hiyo ya mavazi ya michezo ya Uingereza ilisaini dili na Everton mwaka 2024 na ilikuwa patna wa kwanza wa kuchangia ujenzi wa uwanja mpya wa Everton. Kampuni hiyo ya Castore itasimamia masuala yote ya kibiashara na haki za matangazo ya habari mara tu uwanja utakapofunguliwa majira ya kiangazi 2025.

7 - Tottenham Hotspur (Nike, Pauni 30milioni)
Klabu hiyo ya London kaskazini mwaka 2017 ilisaini dili la kutengenezewa jezi na Nike, ambalo litafika ukomo 2033 baada ya kuboresha dili hilo mwaka 2018. wakati liliposainiwa dili hilo la miaka 15 lilionekana kuwa refu zaidi la kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya mchezo kuisaini mkataba na klabu ya soka hasa kwenye Ligi Kuu England. Spurs inanufaika vizuri na kampuni hiyo inayotengeneza jezi zake na kwa mwaka inawaingizia Pauni 30 milioni ambazo zimekuwa zikiwapa nguvu kubwa kwenye mapato yao.

6 - Newcastle (adidas, Pauni 30milioni)
Newcastle United iliamua kurudi adidas, ambayo inaipa kumbukumbu tamu ya mafanikio yao kwenye soka katika miaka ya 90 na 2000 ilipokuwa ikivaa jezi zilizotengeneza na kampuni hiyo. Katika kipindi hicho, Newcastle United ilikuwa timu ya kushindia mataji ikiwa chini ya kocha Kevin Keegan na hakika jezi zao zilikuwa maarufu kwa kuvaliwa na mashabiki mitaani. Na kuthibitisha kampuni hiyo imekuwa na zali na Newcastle baada ya kushinda ubingwa wa Kombe la Ligi kwa kuichapa Liverpool, Jumapili.

5 - Chelsea (Nike, Pauni 60milioni)
Mwaka 2016, Chelsea iliposaini dili na watengeneza jezi wa Nike ulitajwa kuwa mkataba mtamu kabisa wa kibiashara kuwahi kusainiwa kwenye historia ya klabu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge. Chelsea iliachana na adidas na kwenda kusaini mkataba huo wa miaka 15 wa Nike, ambao umekuwa ukiwaingizia Pauni 60 milioni kwa mwaka na kuwafanya kuwa na nguvu kubwa kwenye usajili. Kuvuna Pauni 60 milioni kupitia kampuni inayotengeneza jezi ni kitu ambacho kimeifanya Chelsea kuwa na jeuri ya kusajili.

4 - Liverpool (adidas, Pauni 60milioni)
Dili hilo lilitangazwa Machi 10 mwaka huu na mkurugenzi mtendaji mkuu wa Liverpool, Billy Hogan, ambaye kwenye taarifa alisema jambo hilo limemfurahisha kila mwanafamilia wa klabu hiyo. Liverpool inaamini inafanikiwa kunasa dili hilo tamu kutokana na matokeo mazuri ya ndani ya uwanja na hivyo kuvutia wawekezaji katika kuhakikisha timu hiyo inatangaza bidhaa yao kwa kuwa wazalishaji wakubwa wa jezi, huku miamba hiyo ya Anfield ikinufaika kwa kulipwa Pauni 60 milioni kwa mwaka.

3 - Manchester City (Puma, Pauni 65milioni)
Mwaka 2019, Manchester City iliamua kuachana na Nike na kuhamia kwa Puma kwa dili la miaka 10 la kuwatengenezea jezi zao. Dili hilo lilisimamiwa na kampuni ya City Football Group na lilihusisha timu sita zinazomilikiwa na kampuni hiyo ikiwamo Man City. Timu nyingine zilizohusishwa kwenye dili hilo ni Melbourne FC (Australia), Girona (Hispania), Atlético Torque (Uruguay), Sichuan Jiuniu FC (China) na Man City ya wasichana. Dili hilo la Puma linaifanya Man City kuingiza Pauni 65 milioni kwa mwaka.

2 - Arsenal (adidas, Pauni 75 milioni)
Arsenal iliingia mkataba na adidas mwaka 2019 kwa makubaliano ya Pauni 60 milioni mwaka, lakini iliporesha dili hilo na kuongeza muda hadi 2030, thamani yake iliongezeka kwa Pauni 15 milioni na kuifanya Arsenal kuvuna Pauni 75 milioni. Kabla ya dili hilo la pesa nyingi, Arsenal ilikuwa ikitengenezewa jezi zao na Nike kabla ya kuhamia kwa Puma kwa jumla ya miaka 25. Lakini, sasa miamba hiyo inayofukuzia ubingwa kwenye Ligi Kuu England jezi zao zinatengenezwa na adidas na inavuna mkwanja wa kutosha tu.

1 - Manchester United (adidas, Pauni 90 milioni)
Familia ya Glazer inayomiliki klabu ya Manchester United ilikubali dili la miaka 10 na kampuni ya utengenezaji ya jezi kwenye dili matata kabisa la Pauni 750 milioni. Man United ilibainisha dili lao jipya la kuongeza muda na kampuni hiyo litalenga zaidi kwenye timu ya wanawake, kama ilivyoelezwa mwaka 2018 na kusaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye Women’s Super League. Kwenye dili hilo la watengeneza jezi, Man United ndiyo timu inayovuna pesa nyingi zaidi, ikilipwa Pauni 90 milioni kwa mwaka.